28.2 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Jezi ya Pogba yarudisha gharama za usajili wake

Paul Pogba
Paul Pogba

BADI MCHOMOLO NA MITANDAO,

ILIKUWA jioni ya Agosti 9, mwaka huu, mashabiki wa klabu ya Manchester United walipata habari njema kwamba mchezaji wao wa zamani, Paul Pogba ambaye alikuwa anakipiga katika klabu ya Juventus, amekubali kusaini mkataba wa kuitumikia klabu hiyo ya Old Trafford.

Wengi walikuwa wanasubiri ukweli wa biashara hiyo ya kiungo huyo ambaye alikuwa anawindwa na klabu mbalimbali kama vile Manchester United, Barcelona, Real Madrid na klabu nyingine, hivyo mashabiki hao wa United walikuwa na hamu ya kutaka kujua kama kweli mchezaji huyo anaweza kujiunga na United.

Baada ya kusikia kwamba yupo njiani kwenye ndege akielekea jijini Manchester kwa ajili ya kumalizana na klabu hiyo, mashabiki kupitia mitandao ya kijamii walikuwa wanasambaza ujumbe ambao ulikuwa unasema #POGBACK.

Ujumbe huo ambao ulisambaa sana kwa muda mfupi ulikuwa na maana kwamba mchezaji huyo anarudi katika klabu yake ya zamani ambayo aliondoka tangu mwaka 2012 baada ya kucheza michezo mitatu ya Ligi Kuu bila kufunga bao.

Kutokana na kile ambacho alikuwa anakifanya katika klabu yake ya Juventus ya nchini Italia, mchezaji huyo ghafla thamani yake ikawa juu kuliko mchezaji mwingine duniani katika kipindi hiki cha usajili.

Thamani ya mchezaji huyo ilifikia kiasi cha pauni milioni 100, ambapo haijawahi kutokea kwa mchezaji yeyote katika ulimwengu wa soka.

Kikubwa ambacho watu wengi walikuwa na wasiwasi ni kwamba thamani ya mchezaji huyo kuwa kubwa wakati huo anaweza akaanza kucheza michezo ya awali na akaumia na kumfanya awe nje ya uwanja kwa muda mrefu.

Lakini wataalamu wa biashara ndani ya klabu ya Manchester United hawakulifikiria hilo na wala hawakuwa na lengo la mchezaji huyo kuisaidia klabu hiyo, ingewezekana kwa kiasi hicho cha fedha wakanunua wachezaji zaidi ya watatu ambao wangeweza kutoa mchango mkubwa ndani ya klabu hiyo katika kuhakikisha inaweza kutwaa ubingwa.

Lakini ukweli ni kwamba, mchezaji huyo ana uwezo mkubwa, ila thamani yake imezidi kuwa kubwa zaidi tofauti na uwezo alionao.

Kwa sasa Manchester United wanaweza kuachana na mchezaji huyo kama ingewezekana bila ya kujali michezo aliyocheza kwa kuwa wafanyabiashara wa klabu hiyo wameweza kufikisha malengo yao.

Kikubwa ambacho wanakiangalia mchezaji akisajiliwa ni kwamba wawe na uwezo wa jezi yake kuuzwa kwa mashabiki, sasa kwa upande wa Pogba ambaye amesajiliwa kwa kiasi cha pauni milioni 100 hadi sasa fedha hiyo imerudi kutokana na mauzo ya jezi yake.

Tangu siku ya kwanza anasajiliwa mchezaji hiyo na jezi yake namba 6 kuanza kuuzwa kwa wiki tatu za mwanzo tangu amejiunga tayari amefikisha zaidi ya pauni milioni 200 kwa mauzo ya jezi yake peke yake ambaye amenunuliwa kwa pauni milioni 100.

Hii inaonesha ni jinsi gani watu wanajua biashara kwa kuwa United hawakuangalia ni jinsi gani mchezaji huyo ataweza kutoa mchango wake katika kikosi hicho katika michezo yao, lakini walichokiangalia ni kwamba hata kama wangemnunua kwa kiasi cha pauni milioni 150 bado United ingeweza kuwa na faida kubwa kwa mauzo ya jezi yake.

Hata hivyo, kwa michezo michache ya Ligi Kuu ambayo amecheza mchezaji huyo tayari mashabiki wamekubali uwezo wake na wanaamini ataendelea kuwa na mchango mkubwa kwa michezo inayofuata.

Mbali na mchezaji huyo kurudisha gharama za usajili wake kupitia mauzo ya jezi, pia nyota mwingine wa timu hiyo, Zlatan Ibrahimovic, naye ameifanyia biashara klabu hiyo kwa mauzo makubwa ya jezi yake ambayo wiki ya kwanza kuingia sokoni ilifanikiwa kuuza mauzo ya jumla ya pauni milioni 76.

Bila ya kujali fedha ambazo wamezitumia katika usajili wao, wachezaji hao wameweza kuzalisha fedha mara mbili ya gharama ya fedha zao za usajili.

Kwa upande wa Ibrahimovic, tayari ameonesha mchango mkubwa katika kuhakikisha timu hiyo inafanya vizuri, huku akiwa ameifungia jumla ya mabao matatu katika michezo mitatu aliyocheza, huku akiwa sawa na mshambuliaji wa Manchester City, Sergio Aguero, ambaye na yeye ana jumla ya mabao matatu kwa michezo mitatu aliyocheza.

Kuna baadhi ya makocha nchini England kama vile Pep Guardiola, Arsene Wenger na wengine walimuona kocha wa Manchester United, Jose Mourinho ni mjinga kwa kukubali dau la pauni milioni 100 kwa ajili ya kumsajili mchezaji mmoja.

Lakini klabu hiyo kwa sasa inasubiri kuona mchango wa mchezaji huyo katika michezo yake ijayo ya Ligi Kuu na michuano mingine, hivyo hadi sasa wanasubiri matunda kwa mchezaji huyo na wengine ambao wamesajiliwa kwa kiasi kikubwa cha fedha. Kikubwa ambacho kimebaki ni kuona jinsi gani wanaweza kutwaa ubingwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles