ALLAN VICENT – TABORA
Askari wa Jeshi la Zimamoto na uokoaji nchini wameagizwa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika majengo ya umma na ya wananchi na kuhakikisha yanafungwa ving’amuzi vya moto na vifaa vya kuuzimia ili kuepusha madhara na uharibifu moto unapotokea.
Agizo hilo limetolewa leo Juni 17, na Kamishna Jenerali wa Jeshi hilo Thobias Andengenye alipokutana na waandishi wa habari mkoani hapa akiwa katika ziara yake ya kukagua utekelezaji majukumu ya jeshi hilo.
Andengenye amewataka askari wa jeshi
hilo kuhakikisha wanakagua majengo yote katika mkoa huo ili kuangalia kama
wahusika wanazingatia matakwa ya kikanuni na kisheria ya kuzuia majanga ya
moto katika majengo hayo.
Ameitaka jamii kutambua umuhimu wa kuwa na ving’amuzi vya majanga ya moto
katika majengo yao na vifaa vya kuuzimia yao ambavyo havina gharama kubwa ili
kufanikisha mapambano dhidi ya majanga hayo.
“Askari wa Jeshi la zimamoto elimisheni jamii kuhusu majanga ya moto,
hamasisheni wanafunzi na jamii kwa ujumla kuanzisha klabu za kuzuia,
kuzima na kuokoa wahanga wa majanga ya moto’, amesema.
Aidha ndengenye amewataka wakurugenzi watendaji wa halmashauri zote nchini kulipa kipaumbele suala la kutenga maeneo ya kujenga vituo vya zima moto na uokoaji katika halmashauri zao ili kuongeza ulinzi wa mali na miundombinu iliyopo dhidi ya ajali za moto.