26.9 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Jerry awataka wazazi kusimamia maendeleo ya watoto wao

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Mbunge wa Ukonga, Jerry Silaa, amewataka wazazi na walezi kuongeza juhudi katika kusimamia maendeleo ya watoto wao badala ya kuwaachia walimu pekee.

Mbunge wa Ukonga, Jerry Silaa, akimkabidhi cheti cha uongozi Isaka Simon ambaye alikuwa Kaka Mkuu wa Shule ya Sekondari Sangara wakati wa mahafali ya kidato cha nne yaliyofanyika shuleni hapo.

Ametoa ushauri huo wakati wa mahafali ya 12 ya Kidato cha Nne katika Shule ya Sekondari Sangara iliyopo Kata ya Msongola ambapo wanafunzi 150 wamehitimu.

“Kuna wazazi vikao vya shule hawaji, fedha za chakula hawatoi tukubali jukumu la kusimamia elimu ya watoto wetu ni la kwetu wenyewe bodi ikiita vikao tuhudhurie…manufaa ya baadaye ni makubwa zaidi,” amesema Silaa.

Aidha amewataka wanafunzi kutojihusisha na mahusiano ya kimapenzi kwani athari zake ni kubwa hasa kwa watoto wa kike endapo watapata ujauzito watashindwa kuendelea na masomo.

“Wakati natembelea maonyesho kwenye maabara ya Fizikia na Kemia nimepata picha ya kazi inayofanywa hapa shuleni. Wanafunzi wameonyesha kazi nzuri sana, muendelee kuongeza bidii kwenye masomo yenu mbegu iliyopandwa isiishie njiani,” amesema.

Mbunge huyo pia ameahidi kutoa Sh milioni 5 kupitia mfuko wa jimbo kutatua changamoto mbalimbali za shule hiyo huku akiahidi pia katika bajeti ya 2022/23 watatenga fedha kutatua changamoto zingine zinazoikabili shule hiyo.

Aidha amesema atatoa jezi seti mbili na mipira miwili kukuza vipaji vya michezo shuleni hapo.

Naye Mkuu wa Shule ya Sekondari Sangara, Frida Nyoni, amesema wanakabiliwa na changamoto za uchakavu wa ofisi za walimu, uhaba wa samani, kutokuwepo kwa ukumbi na utoro kwa wanafunzi.

Hata hivyo amesema mipango yao ni kuendelea kutoa elimu bora ili shule hiyo ifanye vizuri kitaaluma.

Akisoma risala kwa niaba ya wahitimu wenzake Jemima Mwalimu, amesema uhaba wa viti na meza umesababisha baadhi ya wanafunzi kukaa chini na kupata ugumu katika kujifunza.

Katika mahafali hayo wanafunzi waliofanya vizuri kitaaluma na kwenye maeneo mengine walizawadiwa vyeti huku Mwenyekiti wa Bodi ya Taaluma ya shule hiyo, Profesa Lukumay akiwazawadia Sh 100,000 wanafunzi walioshiriki katika maonyesho ya Sayansi ili iwe chachu ya kufanya vizuri zaidi kwa wanafunzi wengine.

Shule hiyo iliyoanzishwa Aprili 15,2007 mpaka sasa ina wanafunzi 813 na kati yao wasichana ni 500 na wavulana ni 313.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles