23.2 C
Dar es Salaam
Saturday, July 27, 2024

Contact us: [email protected]

Miaka 60 mapinduzi sekta ya maji nchini

*Kazi kubwa imefanyika

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Wakati Tanzania inapata uhuru mwaka 1961 huduma ya maji haikuwa nzuri na kwa kipindi cha ukoloni ilitolewa kwa matakwa ya serikali ya kikoloni.

Upatikanaji wa majisafi kwa wananchi mara baada ya Uhuru ilikuwa asilimia 25 tu lakini kutokana na kazi kubwa iliyofanywa na Serikali hivi sasa ni wastani wa zaidi ya asilimia 75 ya upatikana maji.

Katika kipindi cha mwaka 1961 hadi 2021, Serikali kwa kushirikiana na Washirika wa Maendeleo (Development Partners) kupitia Mpango wa Maendeleo wa Sekta ya Maji (WSDP) pamoja na taasisi mbalimbali nchini imetekeleza miradi mikubwa ya majisafi na usafi wa mazingira nchini.

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, akizungumza kuhusu mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya maji tangu nchi ilipopata Uhuru.

Miradi hiyo imekamilika na mingine inaendelea kutekelezwa. Utekelezaji wa miradi mikubwa ya maji umefanyika kati ya mwaka 1961 na 2021.

Serikali katika kipindi cha mwaka 2005 hadi 2009, ilikamilisha kazi za ujenzi wa mradi mkubwa wa maji kutoka Ziwa Victoria hadi miji ya Kahama na Shinyanga iliyogharimu Sh bilioni 252. Utekelezaji wa mradi huo mkubwa kuliko yote nchini ulitekelezwa kwa fedha za Serikali.

Kukamilika kwa mradi huo kumeboresha huduma ya maji katika miji ya Shinyanga, Kahama na vijiji 76 kando ya bomba kuu.

Sanjari na utekelezaji huo, Serikali kwa kushirikiana na Serikali ya India imekamilisha ujenzi wa bomba kuu lenye urefu wa kilomita 281 kutoka Kijiji cha Solwa (Shinyanga) kwenda katika miji ya Tabora, Nzega na Igunga. Mradi umelenga kusambaza maji mita za ujazo 54,145 kwa siku na kuongeza upatikanaji wa maji katika Miji ya Tabora, Nzega, Igunga kwa asilimia 100, na jumla ya vijiji 142 katika Wilaya za Shinyanga Vijijini, Nzega, Igunga na Uyui. Gharama ya mradi ni Dola za Marekani milioni 268.35.

Mradi huo ulizinduliwa na aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dk. John Magufuli Februari 23, 2020 na unahudumia zaidi ya wakazi milioni 1.2 katika miji hiyo.

Mradi wa maji wa Chalinze ulijengwa kwa ajili ya kusambaza maji katika vijiji vya Wilaya za Bagamoyo na Morogoro Vijijini. Awamu ya kwanza iliyogharimu Sh bilioni 23.4 iliyohusisha vijiji 20 wilayani Bagamoyo imekamilika. Ujenzi wa awamu ya pili inayohusisha vijiji 48 umekamilika.

Aidha Serikali kwa kushirikiana na Serikali ya India inaendelea kutekeleza awamu ya tatu kwa gharama ya Sh bilioni 41.3. Mradi wa Chalinze awamu ya tatu umelenga kunufaisha vijiji 68 ambapo vijiji 19 viko kaskazini na 49 viko kusini mwa mto Wami.

Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Arabuni ya Maendeleo ya Kiuchumi kwa Bara la Afrika (BADEA), OFID, SAUDI Fund na Kuwait Fund inatekeleza mradi wa maji wa Same – Mwanga – Korogwe katika miji ya Same na Mwanga pamoja na vijiji 38 vilivyomo kandokando ya bomba kuu katika Wilaya za Same, Mwanga na Korogwe.

Mradi huo utakapokamilika utazalisha maji lita milioni 103.7 kwa siku na utawanufaisha wananchi 438,930 katika Wilaya za Same 246,790, Mwanga 177,090 na Korogwe 15,050. Mradi huo unatarajiwa kukamilika Desemba 2021 na utaondoa kero ya maji ya muda mrefu kwa wananchi wa maeneo husika.

Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) inatekeleza mradi wa ujenzi wa Miundombinu ya usambazaji majisafi na uboreshaji wa huduma ya uondoshaji wa majitaka katika Jiji la Arusha unaogharimu Sh bilioni 520 ambapo AfDB inatoa Sh bilioni 492.612 na Serikali Sh bilioni 53.59.

Kukamilika kwa mradi huo kutaongeza uzalishaji wa maji kutoka lita milioni 40 hadi lita milioni 200 kwa siku, muda wa upatikanaji wa huduma ya majisafi kutoka saa 12 za sasa hadi saa 24 kwa siku pamoja na kuongeza huduma ya uondoshaji wa majitaka kutoka asilimia 7.6 za sasa hadi asilimia 30.

Vilevile Serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi ya majisafi katika miji mikuu ya mikoa nchini kwa dhumuni la uboreshaji wa upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama kwa wananchi kupitia mradi wa kuboresha huduma ya maji katika Jiji la Dodoma kwa kutekeleza miradi mbalimbali.

Wizara pia imeanza utekelezaji wa mradi wa kutoa maji katika visima vya Ihumwa kwenda tanki la Njedengwa ambao unagharimu Sh bilioni 2.4. Hadi Machi 2021, visima nane vimechimbwa na vitatu vya zamani vimekarabatiwa. Kazi ya ufungaji wa miundombinu inaendelea na itakapokamilika inatarajia kuongeza muda wa upatikanaji wa maji kwa wakazi wa Dodoma.

Pamoja na mradi wa uboreshaji wa upatikanaji wa huduma ya majisafi Dodoma, Serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi ya kuboresha huduma ya majisafi na usafi wa mazingira katika Mji wa Morogoro, miji ya mikoa ya Mwanza, Iringa, Mbeya, Singida, Babati, Kigoma, Lindi na Sumbawanga.

Pia Serikali kupitia mpango wa Maendeleo wa Sekta ya Maji (WSDP) inatekeleza mradi wa kuboresha huduma ya upatikanaji wa maji katika Miji ya Kigoma, Lindi na Sumbawanga. Kukamilika kwa miradi hiyo kumeongeza uzalishaji wa maji katika miji hiyo na kuwezesha wananchi zaidi 500,000 kupata huduma ya majisafi na salama.

Aidha Serikali kupitia WSDP imeendelea kuboresha huduma za maji katika miji mikuu ya wilaya na miji midogo katika miji ya Orkesumet-Manyara, Longido – Arusha, Utete, Kibiti na Ikwiriri – Pwani, Kilosa, Mvomero, Turiani na Gairo – Morogoro pamoja na Kibaigwa na Mpwapwa – Dodoma.

Pia katika miji ya Nansio, Sengerema na Magu – Mwanza, Geita na Lamadi – Simiyu. Aidha, Miradi ya majisafi ya miji ya Bunda, Tarime na Mugumu – Mara imefanyiwa ukarabati na imeongeza kiwango cha upatikanaji wa huduma ya maji hadi kufikia asilimia 99 ya wakazi wote wa Bunda, Tarime na Mugumu na vijiji ambavyo vipo kwenye chanzo na maeneo linapopita bomba kuu.

Serikali imefanya ukarabati na kupanua huduma za maji katika miradi ya maji ya kitaifa ambayo huduma zake zilianza kuzorota kutokana na uchakavu katika miradi ya maji ya Mugango/Kiabakari/Butiama – Mara, Maswa – Simiyu, Wanging’ombe – Njombe na Masasi/Nachingwea – Mtwara/Lindi.

Katika kuhakikisha inaboresha huduma za maji nchini, Serikali kwa kushirikiana na washirika wa maendeleo imeendelea kuibua miradi kwa ajili ya utekelezaji ili kuboresha huduma za maji nchini kupitia Mradi wa Kukabiliana na Athari za Mabadiliko ya Tabianchi katika Mkoa wa Simiyu.

Katika mkoa huo Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KfW) na Mfuko wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (Green Climate Fund – GCF) na Serikali ya Ujerumani wenye thamani ya bilioni 414 kwa lengo la kuboresha afya na kuongeza uzalishaji maji ili kuinua hali ya maisha ya wananchi walioathirika na mabadiliko ya tabianchi kwa kuimarisha huduma za maji.

Pia mradi wa kuboresha huduma ya maji katika Miji 28 ya Tanzania bara na Visiwani ambapo Serikali kupitia mkopo wa Dola za Marekani milioni 500 kutoka Serikali ya India kupitia Benki ya Exim India inatarajia kuanza utekelezaji wake hivi karibuni.

Aidha Serikali imeendelea kuchukua hatua ya uboreshaji wa miundombinu ya majitaka mijini kwa kujenga miradi mipya na baadhi yake kupanuliwa katika miji ya Arusha, Dodoma, Mbeya, Morogoro, Mwanza, Tabora, Moshi, Tanga, Songea na Iringa. Hii imeongeza huduma ya uondoaji majitaka kufikia asilimia 20 ya wakazi wanaoishi kwenye miji hiyo tangu Desemba, 2020.

Kwa miji ambayo haina miundombinu ya majitaka huduma ya uondoshaji wa majitaka hufanyika kwa kutumia magari maalumu. Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo imekamilisa ujenzi wa mabwawa ya kutibu na kusafisha majitaka katika Miji ya Sumbawanga, Kahama, Misungwi, Lindi, Magu, Kigoma, Nansio na Lamadi.

Vilevile Serikali inaendelea kuboresha huduma kwa kujenga na kupanua mifumo pamoja na ununuzi wa magari ya uondoshaji majitaka kwa lengo la kufikisha wastani wa asilimia 30 ifikapo mwaka 2025.

Aidha Serikali imefanya uwekezaji mkubwa kupitia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kuhakikisha wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam wenye wakazi wengi na viwanda vingi huduma ya maji inaimarika na kuwa toshelevu kwa kutekeleza miradi takriban 16 (12 imekamilika na miradi 4 inaendelea ikiwa katika hatua mbalimbali) yenye jumla ya Sh 127,416,346,397.33.

Mikakati mikubwa inaendelea kutekelezwa kuhakikisha lengo la Serikali la kufikisha huduma ya maji kwa wakazi wa mijini kwa asilimia 95 ifikapo mwaka 2025 linafikiwa na baadhi ya maeneo tayari yamefikia asilimia 100 ya upatikanaji wa huduma.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles