23 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

JE WAJUA KUWA NYAMA YA TWIGA NI TAMU HAINA MFANO

TWIGA ni mnyama anayekula majani tu, ni mrefu kuliko wanyama wote waishio juu ya uso wa dunia. Urefu wake ni zaidi ya futi 15, lakini mkia wake ni mfupi hauwezi kuzidi cm 90 yaani rula tatu. Si mkia tu, hata miguu yake ya nyuma ni mifupi kuliko ya mbele, lakini kwa ujumla miguu yake na shingo ndio humfanya aonekane mrefu zaidi.

Hubeba mimba ndani ya miezi kumi na tano, huzaa mtoto mmoja baada ya kipindi hicho, twiga huzaa akiwa amesimama na mtoto wake huwa ni mrefu mno. Mtoto kwa kawaida huwa na kilo zaidi ya 50, ndani ya saa kadhaa mtoto wa twiga huanza kufanya mazoezi ya kukimbia, katika kipindi hiki mama huwa mlinzi mzuri wa mwanawe.

Hapa kwetu Tanzania mnyama huyu ni fahari ya nchi na ndiye mnyama wa Taifa, kama ambavyo wanyama wengine huwakilisha mataifa yao, picha yake hutumika katika vitu mbalimbali vya serikali, mfano fedha, ndege na majengo ya kifahari zikiwamo hoteli.

Inasemekana kuwa nyama ya kiumbe huyu ni tamu kupita kiasi, laiti kama uhifadhi usingekuwapo basi wanyama hawa wangekuwa wameshakwisha. Katika kuthibitisha hilo, si binadamu tu bali karibia wanyama wote wanaokula nyama humuwinda twiga kwa udi na uvumba na kwa sababu ni mkubwa hakamatiki kwa urahisi basi wanyama hao huwawinda watoto wa twiga.

Wanyama wanaomuwinda twiga ni pamoja na chui, simba, fisi, mbwa mwitu pamoja na mamba, kati yao ni wawili tu ndio hupata bahati ya kuwala twiga wakubwa kwa urahisi, nao ni chui na mamba. Bahati waliyonayo ni kwamba chui humkamata twiga pindi anapokula majani katika mti aliopo na mamba humkamata anapokunywa maji, waliosalia hupata tabu kuwakamata na ili wafanikishe azima yao kwa urahisi ni ama wawe katika kundi kubwa au twiga mwenyewe awe dhaifu, mgonjwa au amejeruhiwa.

Kiumbe huyu ana ulimi mrefu mno ambao humsaidia kula majani ya memea katika miti yenye miba, ni mnyama anayehusudu chakula, anaweza kula hadi kilo 30 na zaidi, pia ni wanyama ambao hawaamini katika kuishi mipakani. Kwa lugha nyepesi ni mnyama anayeishi kwa kuhama hama na hii ni kutokana na kutafuta chakula kwani hutumia chakula kingi, hasumbuliwi na kiu, hivyo maji si jambo muhimu kwake, ikiwa kama atapata majani yenye unyevu nyevu.

Ni mnyama mpole anayeamini  katika amani, ila hataki kabisa kusikia mambo ya kuonewa na huwa haogopi kitu. Wakati mwingine huamua kukimbia ili kuepusha shari hata kama lililopo mbele yake analimudu, ana ustarabu uliotukuka.

Ngozi yake ni dili kubwa ila chonde chonde usijaribu kwenda kuitafuta kwani anapewa ulinzi mkubwa mno. Ukimuondoa faru na tembo, yeye pia hupewa daraja kubwa la uangalizi.

Ngozi yake hutumika kutengenezea nakshi ya mavazi ya wakubwa huko duniani, lakini pia ngozi hiyo hiyo ni tiba kwa wataalamu wetu wa mila huku Afrika.

Ukimuona ni mwembamba lakini ni mzito kupita kiasi, ana kilo zaidi ya 500 na umri wake wa kuishi ni miaka 25, ambapo kama atafikisha umri huo basi tayari atakuwa amefikia viwango vya juu vya uzee.

Kwa umri huo, huwa rahisi kukamatwa kizembe na wanyama walao nyama.

Ukiwaona unaweza kuwatofautisha kwa kuwatazama kichwani, dume huwa na pembe fupi ambazo unaweza usizione kama hautakuwa makini kwani huwa na urefu wa nchi tano na jike hukosa kabisa au huchomoza kidogo kutokana na umri.

Twiga ni mnyama mrembo mbali na kuwa na haiba ya kuvutia kwa urefu wake, lakini pia ana ngozi yenye rangi nzuri, macho yake ni makubwa na anajua kuyatumia vyema kutazama jambo ambalo humuongezea sifa, katika umri wake wa miaka mitano huwa tayari amepevuka na yupo tayari kwa kumjua dume. Dume huwatambua kwa kunusa mkojo wake, mnyama huyu ana uwezo mzuri wa kukimbia ila ni miongoni mwa wanyama ambao wanajichochea yaani kwa kadiri anavyokimbia ndivyo spidi yake inaongezeka, wenzie wenye sifa hiyo ni mbuni na tembo.

 

Unaweza kupendekeza mnyama unayehitaji kumfahamu kupitia namba 0715202047.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles