Na BADI MCHOMOLO
WASANII wengi nchini Marekani wamekuwa na mafanikio makubwa ndani na nje ya muziki huku wakidaiwa kujihusisha na biashara ya madawa ya kulevya.
Hii ni biashara ambayo haikubaliki duniani kote, lakini watu wanafanya kwa kujificha, wengine wanashindwa kufika mbali kwa kuwa wanakamatwa na kuchukuliwa hatua.
Mbali na wasanii hao kujulikana kuwa wanajihusisha na uuzaji wa madawa hayo, lakini wapo wengine ambao hujulikana kuwa ni watumiaji wa madawa hayo.
Jay ni miongoni mwa wasanii wakubwa nchini Marekani wanaohusishwa na biashara hiyo haramu.
Rapa huyu anayetajwa kuwa na fedha nyingi, alianza kushika fedha akiwa na umri mdogo ambapo alijihusisha na kuuza madawa ya kulevya na vitu mbalimbali mtaani kama vile CD nk.
Jay Z aliamua kufanya hivyo kutokana na baba yake kuikimbia familia hiyo, kwa lengo la kuisaidia familia yao. Hata hivyo mama wa msanii huyo hakutaka kabisa kusikia mtoto wake akijihusisha na biashara hiyo.
Baada ya mama huyo kupata taarifa hizo alizungumza na Jay Z lakini alikanusha na mama yake alimuelewa kwa kuwa alikuwa anafanya biashara hiyo mbali na mazingira ya nyumbani kwao.
Msanii huyo anakiri kwamba biashara hiyo imemfanya awe tajiri mbali na muziki, lakini kwa sasa amedai hana mpango wa kujihusisha tena na biashara hiyo.
Wiki moja iliyopita msanii huyo alionekana akiwa amevaa kofia ya mchezo wa Baseball, ikiwa na ujumbe wa kuachana na biashara ya madawa ya kulevya.
Jay Z alionekana mitaa ya New York akiwa amevaa kofia hiyo ambayo imeandikwa‘Retired Drug Dealer’ ikimaanisha kuwa anastaafu kujihusisha na madawa ya kulevya.
“Ni kweli nilikuwa najihusisha na biashara ya madawa ya kulevya, lakini nataka kuandaa kitabu ambacho kitakuwa kinapinga matumizi na biashara ya madawa ya kulevya,” aliwahi kusema mwaka 2013.
Sasa ni wazi kuwa msanii huyo anaamua kuachana na biashara hiyo, huku akiendelea kufanya biashara nyingine kama vile muziki.
Mbali na Jay Z, baadhi ya wasanii wengine wakubwa nchini Marekani wanaojulikana kuwa waliwahi kujihusisha na uuzaji wa madawa ya kulevya ni pamoja na hawa wafuatao:
IDRIS ELBA
Huyu ni nyota wa filamu kwa sasa ambaye anafanya vizuri, awali kabla ya kuwa na jina kwenye filamu na muziki, aliwahi kujihusisha na uuzaji wa madawa ya kulevya, lakini anaamini siyo kitu kizuri ila alikuwa anafanya hivyo kwa ajili ya kujipatia kipato.
“Siyo sifa kufanya mambo kama hayo, lakini ni kweli nimewahi kufanya hivyo na sasa sitaki kusikia biashara hiyo,” aliyasema maneno hayo mwaka 2013.
50 CENT
Huyu ni rapa ambaye amefanya vizuri katika muziki nchini Marekani, aliwahi kuweka wazi kuwa wakati anakuwa alijihusisha na uuzaji wa madawa ya kulevya, akiwa na umri wa miaka 12 tu.
Alifanya biashara hiyo akiwa anaishi na bibi yake baada ya mama yake kufariki wakati 50 Cent akiwa na umri wa miaka minane. Hata hivyo msanii huyo alisema kuwa hata mama yake alikuwa anafanya biashara hiyo.
“Ukiwa unakua katika familia ambayo ni ya hali ya chini basi utakuwa unafikiria kwamba fedha ndiyo kila kitu katika kutatua matatizo, hivyo kuuza madawa ya kulevya ndiyo ufumbuzi wake, lakini ni hatari kwa kuwa wengi wanaishia kwenda jela,” alisema 50 Cent.
SNOOP DOGG
Wengi wanajua historia ya Snoop Dogg, kuwa alikuwa anajihusisha na uuzaji wa madawa ya kulevya aina ya Cocaine, lakini baadaye akaamua kuuza bangi. Inadaiwa kwamba hadi sasa msanii huyu anaendelea na biashara hiyo ya bangi.
B.I.G
Katika kipindi chake ambacho aliishi, msanii huyu wa Hip Hop, alihusishwa na matukio mbalimbali ya vifo vya watu na alidaiwa kuwa ni mtukutu.
Inasemekana kuwa alianza kuuza madawa tangu akiwa na umri wa miaka 12 tu na aliamua kuachana na shule akiwa na miaka 17, hivyo aliweza kujipatia kipato hadi alipojiingiza kwenye muziki.