26.5 C
Dar es Salaam
Sunday, July 21, 2024

Contact us: [email protected]

Jamii yaweka mikakati kuwalinda watoto

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Jamii katika Kata ya Kipunguni jijini Dar es Salaam imeazimia kuwalinda watoto dhidi ya ukatili wa kijinsia ili kuhakikisha wanakua wakijua dunia ni sehemu salama ya kuishi.

Mikakati hiyo iliainishwa Novemba 12,2023 wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia katika Kata ya Kipunguni.

Hafla hiyo ambayo pia ilihusisha bonaza la michezo mbalimbali iliandaliwa kwa ushirikiano wa Kituo cha Sauti ya Jamii Kipunguni na mashirika kadhaa yasiyo ya kiserikali.

Mwenyekiti wa Sauti ya Jamii Kipunguni, Fatma Abdulrahman, amesema watawasimamia watoto ili wajikite zaidi katika kusoma kwa bidii na kutimiza ndoto zao.

Amesema vitendo vingi vya ukatili vinaanzia nyumbani na kuwataka wazazi na walezi kuwa walinzi wa kwanza wa familia zao.

Diwani wa Kata ya Kipunguni, Steven Mushi, akizungumza wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili katika kata hiyo.

“Kipindi cha likizo watoto wanaporudi nyumbani ukatili huwa unaongezeka ndiyo maana katika uzinduzi huu tumeona tukae na watoto tuwape elimu jinsi ya kujilinda na ukatili wakiwa nyumbani kwa sababu ukatili mkubwa unaanzia nyumbani,” amesema Fatma.

Polisi Kata wa Kipunguni, Myeliyeli Kassim, amesema watahakikisha wanaweka madawati kila sehemu ili kutoa elimu na kuwapa fursa wananchi kuripoti vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Amesema kuna changamoto kubwa hasa katika usikilizwaji wa malalamiko ya ukatili kwa sababu yanahitaji usiri na weledi wa kuweza kumhudumia mhanga husika.

“Tutahakikisha tunatoa elimu ya masuala ya ukatili wa kijinsia iweze kuwafikia wananchi wote, nitahakikisha tunapata kituo cha polisi ili wananchi wawe na sehemu ya kukimbilia na kuhudumiwa kwa faragha,” amesema Kassim.

Baadhi ya watoto walioshiriki katika uzinduzi wa maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia Kipunguni wakisoma majarida yenye mafundisho ya watoto.

Diwani wa Kata ya Kipunguni, Steven Mushi, amesema vitendo vya ukatili katika kata hiyo vimepungua kutokana na uboreshwaji wa miundombinu mbalimbali ikiwemo ujenzi wa shule ya sekondari ambao umewapunguzia adha watoto kusafiri umbali mrefu.

“Miaka ya nyuma hatukuwa na sekondari kwahiyo watoto wetu walilazimika kwenda umbali mrefu, njiani walikuwa wanakutana na ukatili wanaporwa, wanakabwa, wanabakwa na mara nyingi walikuwa wanafanyiwa ukatili alfajiri.

“Tunaishukuru Serikali imetujengea sekondari na sasa watoto wako kidato cha tatu, vitendo vya ukatili vimepungua kwa kiasi kikubwa… ukatili Kipunguni unashambuliwa kila kona kuhakikisha unatokomezwa kabisa kwenye kata yetu,” amesema Mushi.

Amesema kupitia uongozi wa mitaa, mashina na chama wamekuwa wakitoa elimu na kuwahimiza wazazi na walezi kuwa makini katika uangalizi wa watoto ili kuepuka kufanyiwa vitendo vya ukatili.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles