23.3 C
Dar es Salaam
Sunday, June 16, 2024

Contact us: [email protected]

Jamii yahimizwa kuendelea kujikinga na VVU

Na Mwandishi Wetu, Rukwa

Viongozi wa mikoa nchini wametakiwa kuendelea kuhamasisha jamii kujikinga na maambukizi ya VVU kupitia mikutano na vikao mbalimbali vinavyoendelea katika maeneo yao huku wakihimizwa kuwa pamoja na jitihada zinazofanyika katika kujikinga na UVIKO-19 zisiache nyuma magonjwa mengine ikiwamo VVU.

Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS), Dk. Leonard Maboko(Kulia) akimsikiliza Katibu Tawala Msaidizi (Mipango) wa Mkoa wa Rukwa, David Kilonzo (katikati), alipotembelea mkoa huo kwa lengo la kuangalia utekelezaji wa shughuli za VVU na UKIMWI mkoani humo.

Wito huo umetolewa juzi na Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS), Dk. Leonard Mabok, mkoani Rukwa alipokuwa katika ziara ya kikazi yenye lengo la kufanya ufuatiliaji na tathimini ya utekelezaji wa afua za VVU na UKIMWI katika mkoa huo.

Dk. Maboko amesema kuwa maambukizi ya VVU bado yapo, hivyo pamoja na jitihada zinazofanyika katika kujikinga na UVIKO-19 tusiache kujikinga na magonjwa mengine ikiwemo VVU, kwakuwa mwenendo wa takwimu zinaonesha bado kuna kazi ya kufanya katika mwitikio wa VVU na UKIMWI hapa nchini.

“Tatizo kubwa bado lipo kwa wanaume ambao wamekuwa na mwitikio mdogo wa kupima na kujua hali zao za maambukizi ya VVU, pamoja na hayo bado vijana na makundi maalum wanahitaji kuhamasishwa ili kupima na kujua hali zao kwa kuwa bado hali zao hazijatambulika vizuri wakati bado kuna lengo la kifikia tisini na tano tatu ifikapo 2025.

“Lengo la kuhakikisha asilimia 95 ya watu wanaoishi na VVU wanajua hali zao za maambukizi limefikiwa kwa asilimia 83 tu hadi kufikia mwaka 2019. Katika lengo la pili la kuhakikisha asilimia 95 ya watu wanaoishi na VVU (WAVIU) wanatumia dawa za kupunguza makali ya VVU tumefanya vizuri kama nchi kwani hadi kufikia mwaka 2017 asilimia 95 ya WAVIU walikua wanatumia dawa pamoja na hayo kwa mujibu wa taarifa za UNAIDS takwimu zinaonesha kwamba kwasasa lengo hilo tumelifikia kwa asilimia 98,” amesema Dk. Maboko.  

Aidha, Dk. Maboko amesema kuwa kwa sasa vifo vitokanavyo na UKIMWI vimepungua, ambapo wanaofariki kwa sasa ni wale ambao hawatumii dawa vizuri au ambao hawajapima na kujua hali zao.

Amesema katika lengo la tatu la kuhakikisha asilimia 95 ya watu wanaoishi na VVU wanapunguza makali ya VVU mwilini mwao tumefanikiwa kufikia asilimia 90 hadi sasa.

“Dk. Maboko amesema kuwa kwa kutekeleza hayo malengo matatu, bila shaka tutaweza kufikia pia lengo la sifuri tatu ifikapo mwaka 2030 kwa maana ya kuwa tutakuwa tumemaliza maambukizi mapya ya VVU, vifo vitokanavyo na UKIMWI na kupinga unyanyapaa na ubaguzi kwa watu wanaoishi na VVU,” amesema Dk. Maboko.

Aidha, Dk. Maboko amewasihi wakuu wa mikoa kutoa kipaumbele katika uhamaishaji na utekelezaji wa shughuli za VVU kwenye mikoa yao kwani ni moja ya njia kuu za kufikia malengo ya serikali ya kumaliza maambukizi ya VVU ifikapo mwaka 2030.

Pia Dk. Maboko amesisitiza umuhimu wa kufanyika kwa vikao vya VMAC na WMAC ili kuweza kutatua changamoto zilizopo katika ngazi za chini na hao ndio wanaoishi na wananchi moja kwa moja, katika ngazi za Kijiji na mtaa.

Naye, Katibu Tawala Msaidizi (Mipango) wa Mkoa wa Rukwa, David Kilonzo ameshukuru, Dk. Maboko kwa kufanya ziara katika mkoa wake na kuwakumbusha umuhimu wa kendelea kutoa elimu juu ya maambukizi mapya ya VVU na UKIMWI.

Kilonzo amesema kuwa jitihada hizo zitaendelea na kurekebisha pale palipokuwa na mapungufu, ili kufikia malengo ya 2030 ya kuwa na Tanzania isiyokuwa na UKIMWI inawezekana.

TACAIDS ilifanya ziara katika mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma, Mbeya na Rukwa kwa lengo la kufanya ufuatiliaji na Tathimini ya afua za VVU na UKIMWI zinazotekelezwa katika mikoa hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles