27.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Junior Scholar kuwagharamia mahitaji muhimu watakaochaguliwa shule za vipaji

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Shule ya Awali na Msingi ya Junior Scholar iliyopo Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro imeahidi kuwagharamia mahitaji muhimu wanafunzi watakaochaguliwa kujiunga na shule za sekondari za vipaji maalumu.

Kikundi cha utamaduni cha Shule ya Awali na Msingi ya Junior kikitumbuiza wakati wa mahafali ya kwanza ya darasa la saba yaliyofanyika shuleni hapo.

Ahadi hiyo imetolewa na Meneja wa shule hiyo Dismas Mbwana, wakati wa mahafali ya kwanza ya darasa la saba yaliyofanyika shuleni hapo.

Amesema wanafunzi wa darasa la saba wameandaliwa vizuri kimaadili, kitaaluma na kokote watakakokwenda wataitangaza vyema shule hiyo.

“Sina wasiwasi wowote na wanafunzi wa darasa la saba, kitaaluma tuna mafanikio mengi sana ambayo wameyafanya lengo letu tunataka tuwe katika shule kumi bora kitaifa, nia tunayo na uwezo tunao.

“Kwa wale wote watakaochaguliwa “special school’ tutagharamia mahitaji yote ya kujiunga na kidato cha kwanza,” amesema Mbwana.

Naye Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Onesmo Brown, amesema ilianzishwa Januari 2012 ikiwa na wanafunzi watatu na kwa sasa ina wanafunzi 386 wakiwemo wavulana 202 na wasichana 184.

“Tumejipanga kupata ufaulu wa watoto wote siyo tu wa madarasa ya mitihani hivyo, tunawaomba wazazi na walezi muwalete watoto waje wapate elimu bora tunayoitoa katika shule yetu,” amesema Mwalimu Brown.

Emmanuel Kadilo akifurahia baada ya kihitimu darasa la awali.

Hata hivyo amesema wana changamoto ya kushindwa kuwafikia watoto wengine ambao wanatoka maeneo ya mbali, ukosefu wa umeme na kuchomwa moto eneo karibu na shule hali inayosababisha usumbufu kwa wanafunzi nyakati za masomo.

Kwa upande wake mgeni rasmi Dk. Pepetua kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe, ameupongeza uongozi wa shule hiyo kwa kukuza kiwango cha taaluma na kuwataka kuboresha mbinu za ufundishaji ili watoto waweze kupata ujuzi na maarifa ambao taifa linategemea.

“Shule za awali na msingi ni muhimu sana kwa maisha ya watoto wetu, kutoka kwa watoto hawa ndipo ambapo tutawapata mawaziri, madaktari, walimu na wanataaluma wengine, hivyo ni jukumu la kila mmoja kushirikiana kujenga miundombinu,” amesema Dk. Pepetua.

Katika mahafali hayo wanafunzi waliofanya vizuri walizawadiwa sambamba na walimu waliofaulisha darasa la nne mwaka jana ambapo wanafunzi wote walipata daraja A.

Aidha uongozi wa shule hiyo pia uliwazawadia wafanyakazi bora wa mwaka 2020/2021, mwalimu bora wa madarasa ya awali, walimu na watumishi wengine waliotumikia shule hiyo kwa muda mrefu.

Shule hiyo ina mkakati wa kujenga jengo la maktaba ili watoto waweze kujisomea, jengo la kompyuta watoto waweze kujifunza kwa nadharia na vitendo huku mipango ya baadaye ikiwa ni kujenga mabweni ili watoto wa darasa la saba wakae hosteli.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles