LICHA ya juhudi mbalimbali zinazochukuliwa na serikali na wadau wa maendeleo nchini kuhakikisha inakuwapo sera nzuri na mifumo ya kuwezesha ukuaji uchumi kupitia sekta ya fedha lakini bado mchango wa mwanamke hauonekani.
Hata hivyo, serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT), nayo imeendelea kutoa miongozo ya kuhakikisha Malengo ya Milenia yanafikiwa ifikapo mwaka 2015 ili Watanzania takriban asilimia 50 waweze kufikiwa na huduma za benki.
Ripoti ya Maendeleo ya Watu Afrika ya 2016 kuhusu usawa wa jinsia inafuatia pamoja na ile ya Maendeleo ya Watu Afrika ya mwaka 2012 iliyoangazia umuhimu wa kuhakikisha usalama kwa waafrika wote.
Ripoti zote mbili zina lengo moja la kushughulikia kile kinachoonekana kuwa ni utekelezaji wa ajenda zilizokuwa bado kukamilishwa katika mwelekeo wa maendeleo ya Afrika.
Yote mawili yametambuliwa kama vipaumbele muhimu kwa serikali barani Afrika.
Ili kushughulikia upungufu huo, ripoti hiyo inachukua njia ya uchumi jamii katika masuala ya usawa wa jinsia na uwezeshaji wanawake barani Afrika ikiwamo Tanzania.
Kutokana na hali hiyo, sasa ni wakati kwa Tanzania kuweka mkazo wa sera na programu katika kutumia vipaji vya wanawake kuleta msukumo wa uchumi na jamii kwa maendeleo jumuishi na endelevu zaidi.
Kwa maelezo rahisi, kuongeza kasi ya usawa wa jinsia ni jukumu muhimu la serikali, likihusisha jitihada za sekta mbalimbali zikiwamo taasisi za taifa, watendaji wasio wa kiserikali, vyama vya raia na sekta binafsi.
Vivyo hivyo, kushughulikia usawa wa jinsia kwa namna pana kama hiyo kunaunganisha na kuimarisha ajenda motomoto ya Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), ambayo serikali za Afrika na jamii ya mataifa kwa pamoja wamejiwekea kwa miaka 15 ijayo.
Njia pana katika kuleta usawa wa jinsia pia itaimarisha mafanikio ya Ajenda 2063 ya Umoja wa Afrika. Ripoti hii ya Maendeleo ya Watu Afrika ya 2016, kwa hiyo, inatoa muundo-kazi wa utekelezaji wa SGD.
Hatua hiyo sasa inamfanya Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, kuona umuhimu wa sera za uchumi wa nchi kutambua mchango wa mwanamke kwenye uzalishaji mali na ukuaji wa uchumi wa taifa.
Tunaunga mkono uamuzi huo wa Makamu wa Rais Samia, kwa sababu ni ukweli ulio wazi kwamba wanawake wengi wamekuwa wakishiriki kujenga uchumi kupitia sekta isiyo rasmi lakini bado wamekuwa hawatambuliki kwenye sera.
Hatua ya kuwapo mikakati mbalimbali ikiwamo pia ile ya Benki ya TPB kuja na Akaunti ya Tabasamu ambayo ni mahsusi kwa wanawake ni sehemu ya mkakati wa kumuwezesha mwanamke kama kiungo muhimu kwenye uchumi wa nchi yetu.
Tunajua kwamba wanawake ndiyo wazalishaji wakubwa na wengi wao wanamiliki viwanda vidogo na vya kati lakini bado mchango wao hautambuliki kwenye ukuaji wa uchumi.
Hatua hiyo inaweza kuwa kile alichokiona Makamu wa Rais Samia kwamba hata sera zetu bado hazijatambua hilo na sasa umefika wakati kwa mamlaka za serikali kuliona hilo.