-Dar es Salaam
UPANDE wa Jamhuri umepinga hoja ya mke wa bilionea Erasto Msuya, Miriam Msuya na mwenzake kwamba waliteswa ili wakili kumuua dada wa bilionea huyo.
Jamhuri ikiongozwa na Wakili wa Serikali, Diana Lukondo uliwasilisha hoja hizo jana ukijibu hoja zilizowasilishwa na Wakili wa utetezi, Peter Kibatala mahakamani hapo wiki iliyopita.
Mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Margareth Benkika wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Kibatala alidai baada ya kuzungumza na washtakiwa wote wawili wamemuarifu kwamba waliteswa baada ya kukamatwa.
Alidai washtakiwa walimueleza kwamba waliteswa wakili ushiriki wao kwa kutenda mauaji na kwamba maelezo waliyoandika washtakiwa wote yalikuwa ni kutokana na mateso na wana alama zote ikiwamo kuvimba miguu na wana majeraha sehemu mbalimbali za miili yao.
“Naomba majibu ya uchunguzi wa afya za washtakiwa hao yawasilishwe mahakamani na kuwekwa kwenye kumbukumbu za kesi tuweze kuyatumia baadaye,”alidai Kibala.
Akijibu, Diana alidai hakuna sheria inayoelekeza mahakama kutoa amri kwa Jeshi la Megereza kuwafanyia vipimo washtakiwa na kama waliteswa walitakiwa kutoa taarifa ya tukio lifanyiwe uchunguzi.
“Magereza hawawezi kutibu mtu aliyeteswa ama kupigwa bila kuwa na PF3, kama kweli aliteswa na wanaumwa wasingepokelewa na Magereza.
“Upande wa utetezi wanaanzisha utetezi wao katika masuala ya uchunguzi na wanaitumia mahakama kama sehemu ya huo uchunguzi,”alidai Diana.
Diana alidai hoja kwamba hati ya mashtaka haijitoshelezi si sahihi, hati ya mashtaka inajitosheleza kumwezesha mshtakiwa kuelewa kile alichoshtakiwa nacho.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni Miriam (41) na Revocatus Muyela (40), wote wafanyabiashara na wakazi wa Arusha. Wanakabiliwa na mashitaka ya mauaji ya Aneth Msuya.
Inadaiwa washtakiwa hao walitenda kosa hilo Mei 25, mwaka huu, maeneo ya Kibada, Kigamboni, Dar es Salaam, ambako kwa pamoja walimuua Aneth.
Agosti 9, mwaka huu, Jeshi la Polisi lilitoa taarifa kuhusu kumtia mbaroni mke wa bilionea huyo kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya Aneth.
Aneth, ambaye ni dada wa bilionea Erasto Msuya, aliuawa kwa kuchinjwa na watu wasiojulikana nyumbani kwake eneo la Kibada block 16, Kigamboni, ambako inaelezwa wauaji hao hawakuchukua kitu chochote ndani ya nyumba yake.
Bilionea Msuya, aliuawa kwa risasi katika eneo la Mijohoroni, kando ya barabara ya Arusha – Moshi wilayani Hai mkoani Kilimanjaro.
Alikuwa ameitikia wito wa kwenda kununua madini ya Tanzanite baada ya kupigiwa simu na vijana wawili waliomtaka wakutane maeneo hayo.
Inadaiwa alipofika katika eneo hilo akiwa na gari lake la Range Rover T 800 CKF na kuwakuta vijana hao wakimsubiri, baada ya kuteremka Msuya alikwenda kumsalimia mmoja wa vijana hao na kabla hajamfikia alitoa bunduki ya SMG namba KJ 10520 aliyokuwa ameificha kwenye koti na kumfyatulia risasi.