Na Kulwa Mzee-Dar es Salaam
JALADA la kesi inayomkabili Kamishna wa Kodi na Forodha wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Tiagi Masamaki na wenzake, lililopelekwa kwa Manasheria Mkuu wa Serikali (AG), liko katika hatua za mwisho.
Wakili wa Serikali, Christopher Msigwa alisema hayo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shahidi, kesi hiyo ilipokuwa inatajwa.
Msigwa alisema jalada la kesi hiyo liko kwa AG katika hatua za mwisho hivyo aliomba ahirisho fupi na mahakama ilikubali kuahirisha kesi hiyo hadi Desemba 19 mwaka huu.
Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Haroun Mpande wa kitengo cha Mawasiliano ya Kompyuta ICT TRA, Msimamizi Mkuu Kitengo cha Ushuru wa Forodha ICD Azam, Eliachi Mrema, Mchambuzi Mwandamizi wa Masuala ya Biashara TRA, Hamis Omary , Meneja wa Oparesheni za Usalama na Ulinzi ICD, Raymond Adolf Louis na Meneja wa Azam ICD, Ashrafu Khan.
Washtakiwa wote kwa pamoja wanadaiwa kuwa kati ya Juni mosi na Novemba 17, 2015 walikula njama kwa kuidanganya Serikali.
Wanadaiwa kudanganya kuwa makontena 329 yaliyopo katika Bandari Kavu ya Azam (AICD) yalitolewa baada ya kodi zote kufanyika wakati si kweli.
Katika shtaka la pili, wanadaiwa kuwa katika kipindi hicho jijini Dar es Salaam, washtakiwa hao kwa pamoja walishindwa kutimiza majukumu yao na kuisababishia Serikali hasara ya Sh bilioni 12.7.