22.9 C
Dar es Salaam
Sunday, June 23, 2024

Contact us: [email protected]

Jaji Mutungi avionya vyama vya siasa

mutungiNa Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

MSAJILI wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, amevitaka vyama vya siasa kuhakikisha vinafuata katiba na kanuni katika utendaji wa kila siku ili kuepuka migogoro na migongano ndani ya vyama hivyo.

Hayo ameyabainisha kwenye barua yake yenye Kumb. Na. HA.322/362/01/103 aliyoiandika kwa vyama vya siasa jana.

“Nimeona ni vyema nitumie fursa hii kuviasa vyama vya siasa kuhusu hali hii, kwani hali hii ya kufanya mambo kiholela pasipo kufuata katiba na kanuni kama itaachwa iendelee hivi ndani ya vyama, kwa hakika italeta migogoro na mipasuko mikubwa ndani ya vyama vya siasa husika.

“Wakati huu ambapo nchi yetu inasubiri marudio ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar, nimeandikiwa barua na pia kupata nakala za barua kutoka kwa baadhi ya vyama vya siasa kuhusu migongano ya wanachama na viongozi au viongozi wenyewe kwa wenyewe kuhusu suala la kushiriki Uchaguzi wa Marudio Zanzibar,” alisema Jaji Mutungi.

Barua hiyo ilibainisha kuwa suala hilo la migongano limejitokeza pia kwa wingi kwenye vyombo vya habari, ambapo wanachama na viongozi au viongozi wenyewe kwa wenyewe wametofautiana na kupingana hadharani.

Jaji Mutungi alisema kwa mujibu wa kanuni ya 3(1) ya kanuni za usajili wa vyama vya siasa za mwaka 1992 (GN.No. 111) vyama vya siasa vinaposajiliwa vinapaswa kuwasilisha katiba na kanuni zake kwa Msajili wa Vyama vya Siasa.

“Ikumbukwe kwamba suala la msingi hapa ni kwamba, sharti la kuwapo kwa katiba na kanuni katika chama, kimsingi ni mwendelezo wa kukuza na kudumisha dhana ya kuendesha vyama kitaasisi kulingana na mwongozo uliokubalika na kuasisiwa kichama kwa mfumo wa katiba na kanuni za chama, na si kuendesha chama kiholela kama inavyoelekea kuota mizizi kwa baadhi ya vyama vya siasa hivi sasa,” alisema Jaji Mutungi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles