26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Simba, Yanga kazi tu

Simba-Yanga*Ni mtanange wa kwanza tangu Magufuli aingie madarakani

*Ubishi wote kumalizwa kwa ‘Mchina’ Jumamosi hii

NA ADAM MKWEPU, DAR ES SALAAM

ZIKIWA zimesalia siku tatu kwa watani wa jadi Simba na Yanga kushuka dimbani kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, mtanange huo utakua wa kwanza kuchezwa tangu Rais wa Awamu ya Tano, Dk. John Magufuli kuingia madarakani.

Magufuli aliingia rasmi madarakani Novemba 5 mwaka jana, baada ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25 na kushinda.

Mahasimu hao wamewahi kukutana mara 79  katika historia ya klabu hizo, mara ya mwisho wamekutana Septemba 26 mwaka jana kabla ya Uchaguzi Mkuu, ambapo Simba walikubali kichapo cha bao 2-0 toka kwa Yanga, wakati huo ukiwepo uongozi wa awamu ya nne chini ya Rais mstaafu, Jakaya Kikwete.

Yanga kwa mujibu wa rekodi za ligi, inaonekana kuwa mbabe kwa kuifunga Simba mara 29, huku Simba wakifanikiwa kupata ushindi mara 23 na kutoka sare mara 27.

Katika uongozi wa awamu ya nne, Yanga ilikubali kipigo cha mbwa mwizi kwa kuchapwa bao 5-0 mwaka 2012 ikiwa chini ya Msebia Kostadin Papic, licha ya kwamba hakua katika benchi siku hiyo aliishuhudia ikifa ikiwa chini ya msaidizi wake, Fred Felix Minziro.

Kuelekea katika mchezo huu wa Jumamosi, Yanga imeonekana kuwa na wachezaji wengi wenye uzoefu katika mechi za watani wa jadi, ambapo ina wakongwe, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Ally Mustapha ‘Barthez’, Deogratius Munishi ‘Dida’, Mbuyu Twite, Haruna Niyonzima, Simon Msuva na Kelvin Yondani ambaye hachezi kwa kuwa anatumikia kadi nyekundu tofauti na Simba ambayo wakongwe wa mechi hizo ni wachache kama Jonas Mkude, Hamis Kiiza ‘Diego’, Said Ndemla na Mwinyi Kazimoto.

Mbali na hilo, wachezaji kama Barthez, Dida na Kiiza wana uzoefu mkubwa zaidi kwa kuwa wamewahi kuchezea klabu zote mbili yaani Simba na Yanga na kujionea fitina na figisu zinazokuwepo.

Presha ya mashabiki imeonekana kupanda katika mechi hii, wakitaka kujua nani ataibuka mshindi kwenye mchezo, ambapo huenda mshindi akaashiria kuwa bingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara kutokana na hali ilivyo kwenye msimamo kwani Simba inaongoza ikiwa na pointi 45 ikiwa imefunga mabao 35 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 11, ikufuatiwa na Yanga yenye pointi 43, mabao 42 na kuruhusu mabao 9.

Simba imekosa ubingwa kwa misimu mitatu, mara ya mwisho kutwaa ubingwa huo ilikua msimu wa 2011/2012, hali ambayo inawanyima raha mashabiki wake.

Timu hizi kongwe zimekuwa na historia ndefu zinapokutana kutokana na kuwa na mashabiki wengi nchini.

Mashabiki hao wakati mwingine wanatia presha kubwa ambayo inashawishi viongozi kutimua makocha wao kama timu moja wapo itakubali kufungwa mfano Yanga iliwahi kumfukuza Ernie Brandts na Marcio Maximo baada ya kufungwa kwenye mechi za Mtani Jembe.

Mbali na hilo, kibarua kikubwa kitakuwa kwa washambuliaji wa timu hizo ambao wanaonekana kuwa na uchu wa mabao msimu huu.

Washambuliaji hao, Kiiza wa Simba anayeongoza  kwa kuwa na mabao 16 na  Amissi Tambwe wa Yanga mwenye mabao 14, watafanya mchezo huo kuwa mgumu pande zote kwani wachezaji hao wana uwezo wa kufunga bao zaidi ya moja kwenye mechi.

Makocha wa timu hizo, Jackson Mayanja na Hans Van De Pluijm, wameonyesha kuwa imara kuelekea katika mchezo huo, huku kila mmoja akionekana kutokua na hofu.

Mayanja ametamba kupata dawa ya wapinzani wao Yanga, huku akiwataka mashabiki wake kusahau uchungu wa bao 2-0 za mchezo uliopita kwa kuwa ana uhakika wataibuka na ushindi.

Anatarajia kutumia mfumo wa 4-4-2 ambao wakati mwingine hucheza kama 4-3-3 kwa kuwa na washambuliaji watatu.

Pluijm kwa upande wake amedai kuwa hana na hajawahi kuwa na hofu wala presha dhidi ya wapinzani wake hao, huku akiamini lolote linaweza kutokea katika mchezo huo. Naye anajipanga kutumia mfumo wa 4-2-3.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles