Na Mwandishi Wetu-Dodoma
JAJI Mkuu, Profesa Ibrahim Hamis Juma, amewataka wanasheria wa serikali kuhakikisha sheria wanazozisimamia zinakidhi matarajio ya maendeleo na ustawi wa wananchi maskini.
Aliyasema hayo jana wakati akifungua mkutano wa siku mbili wa wanasheria walio katika utumishi wa umma, unaofanyika Dodoma.
“Wananchi ndiyo msingi wa mamlaka yote, kupitia Katiba ya Jamhuri ya Muungano, Serikali, Bunge na Mahakama, zinapata mamlaka zao kutoka kwa wananchi.
“Wanasheria katika sekta ya umma hakikisheni sheria zinalenga ustawi wa wananchi,” alisisitiza Jaji Mkuu
Mkutano huo unaowakutanisha mawakili wa Serikali 900 kutoka wizara mbalimbali, idara, taasisi za Serikali na mamlaka ya Serikali za Mitaa.
Alisema wadhifa mpana wa Wizara ya Katiba na Sheria, unampa waziri upeo mpana wa kuhakikisha sheria za Tanzania zinalenga katika ustawi wa wananchi ambao wengi wao ni wenye hali duni ya maisha.
Akitilia mkazo kuhusu sheria zinazolenga kuwasaidia wananchi maskini, Jaji Mkuu alisema sheria hizo lazima ziwasaidie wananchi maskini kunufaika na Malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025.
Jaji Mkuu amewataka mawakili wa Serikali wanaofanya kazi katika sekta ya umma kuhakikisha ubora wa huduma za sheria wanazozitoa zinakidhi mahitaji ya uchumi wa kati.
“Uwakili wa Serikali ni utumishi unaohitaji kuaminiwa na kuaminika, tusitumie kuaminiwa na kuaminika kwetu kwa maslahi binafsi dhidi ya manufaa binafsi ya umma,” alionya Jaji Mkuu
Amewataka wanasheria hao walio katika utumishi wa umma na kama washauri wa sheria kwa viongozi mahali pao pa kazi, kutumia ujuzi, weledi na uadilifu mkubwa kutoa ushauri wao kwa maslahi mapana ya taifa.
“Muwasaidie viongozi kwa kuwashauri kabla hawajatoa amri na maagizo mbalimbali ambayo huzidisha migongano ya sheria na hasara kwa serikali.
Katika hatua nyingine, amewataka wawaziri, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya,madiwani,wakuu wa mashirika ya umma, wakubali ushauri wa sheria kutoka kwa wanasheria wa Serikali.
Alisema endapo hawaridhishwi na ushauri wao basi wafuate ngazi za kufuata hadi kupata ushauri kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Wakili Mkuu wa Serikali.
“Ujumbe wangu kwa mawaziri, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, madiwani, wakuu wa mashirika ya umma, tukubali ushauri wa sheria kutoka kwa wanasheria wa Serikali.
“Endapo ushauri huo hauturidhishi, basi zipo ngazi za kufuata hadi kupata ushauri wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Wakili Mkuu wa Serikali,” alisema.
Naye Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi alisema kutokuwapo mfumo rasmi wa kuwakutanisha wanasheria walioko katika utumishi wa umma, kulisababisha baadhi ya wanasheria wa serikali kufanya uamuzi usio na tija kwa taasisi na taifa kwa kuingia mikataba mibaya.
“Serikali imekuwa ikiingia katika gharama kubwa ya kulipa mabilioni ya fedha inaposhindwa katika mashauri mbalimbali mahakamani kutoka na uamuzi na ushauri mbaya uliotolewa na wanasheria waliopo katika utumishi wa umma,” alisema Profesa Kabudi.