22.5 C
Dar es Salaam
Sunday, July 21, 2024

Contact us: [email protected]

JAJI LUBUVA: MASHINE ZA BVR ZILINIUMIZA KICHWA UCHAGUZI MKUU 2015

Na ELIZABETH HOMBO


JAJI Damian Lubuva ni miongoni mwa majaji waliojizolea heshima kubwa katika Taifa la Tanzania kutokana na utendaji kazi wake uliotukuka.

Mwenyekiti huyo Mstaafu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), alipata kushika nyadhifa mbalimbali serikalini ikiwamo Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Waziri wa Sheria na Mwenyekiti Baraza la Maadili la Tume ya Maadili ya Viongozi, alitumikia nafasi hiyo ya uenyekiti wa NEC kwa miaka mitano.

Huyu ndiye Mwenyekiti ambaye tunaweza kusema alikumbana na changamoto kubwa kwa mara ya kwanza ya Usajili wa Wapiga Kura nchini uliofanyika kwa njia ya Kielektroniki yaani Biometric Voter Registration (BVR), katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Katika mahojiano yake na MTANZANIA yaliyofanyika nyumbani kwake jijini Dar es Salaam hivi karibuni, Jaji Lubuva pamoja na mambo mengine mengi aliyozungumza alieleza namna changamoto hiyo ya BVR ilivyomwumiza kichwa katika uchaguzi huo.

MTANZANIA: Umekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa miaka mitano, Unauonaje mfumo huu wa viongozi wote wa Tume kuteuliwa na Rais, unadhani sasa kuna haja ya kuwa na Tume Huru ili kuondokana na malalamiko kutoka upinzani?

JAJI LUBUVA: Nisingependa sana kulizungumzia hili kwa sasa kwa sababu wenzangu wapo wangelizungumzia, lakini hata hivyo ni kweli Mwenyekiti na makamishna wote wa tume wanateuliwa na Rais, lakini tangu ilipoanzishwa mwaka 1992 tume ilikuwa ikifanya kazi zake kwa Uhuru.

NEC haikuwahi kuingiliwa na mtu yeyote, ni huru na inasimamia uchaguzi kwa Uhuru bila kuelekezwa na mtu yeyote aliyeko madarakani hiyo ndiyo maana ya Tume Huru.

Iko haja usipoandika Tume Huru kama ya Kenya, unaweza kuona kwamba pamoja na kutajwa kwenye sheria ni huru kumbe haziko huru hata kidogo.

Kilichopo ni maono ya watu kwenye fikra zao wanafikiria kwamba mwenyekiti, wakurugenzi na makamishna wa tume wote wanateuliwa na Rais hivyo wanadhani kwamba watapendelea mtu fulani.

Lakini kiukweli tume yetu ni huru pengine kuliko za nchi zingine na Kenya mlishuhudia ilivyokuwa pamoja na kwamba tume yao ina neno huru.

Sasa kama ni kubadilishwa ni suala la kuangalia muda mwafaka kwa sababu ni suala la Katiba, lakini jinsi Katiba na sheria zilivyo nasema kwa nguvu zote kuwa Tume yetu ni huru.

Tumekaa miaka minne na JK (Rais Mstaafu Jakaya Kikwete), lakini hajawahi kuniita hata siku moja akanipa maelekezo yoyote na kuniambia pendelea fulani.  Bila hata neno huru tume iko huru kabisa.

MTANZANIA: Una mtazamo gani kuhusu wakurugenzi wa halmashauri ambao ni makada wa vyama vya siasa kusimamia uchaguzi?

JAJI LUBUVA: Lengo la tume ni kuwa na watumishi wake huko mbele ya safari, uchaguzi wowote unavyokuja wakurugenzi wa halmashauri huwa wanaapa kuwa watazingatia maelekezo ya tume na si ya mtu yeyote.

Azma ya tume ni hatua kwa hatua kuja kuwa na watumishi wao kama ilivyo katika sehemu zingine  kwa sababu nchi hii ni kubwa. Zipo sehemu nyingi wamejiita Tume Huru lakini uchaguzi wao umekuwa na vurugu.

MTANZANIA: Ni jambo gani ambalo umelifanya na hutalisahau ukiwa tume na unajivunia?

JAJI LUBUVA: Najivunia kwamba wafanyakazi wote wa tume niliishi nao vizuri na niliondoka kifua mbele kwa maana kwamba nimefanya kazi inavyopaswa.

Niliingia pale nikitokea Tume ya Maadili, nilienda pale nikapokewa vizuri, tuliishi nao vizuri na nimeacha tume kama kitu kimoja.

Na kwa pamoja tulienda kwenye uchaguzi kwa ufanisi mkubwa na ulikuwa na ushindani mkubwa lakini uliisha kwa amani. Napumzika kwa amani kwa maana kazi nilikamilisha vizuri.

MTANZANIA: Wakati wa mchakato wa uchaguzi na baada ya matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 ulijisikiaje ulipokuwa ukitupiwa lawama na vyama vya upinzani?

JAJI LUBUVA: Ni kweli lawama zilikuwapo wakati ule wa uchaguzi wa mwaka 2015, lakini pamoja na lawama hizo mimi ni miongoni mwa waliopitia ofisi nyingi, kibinadamu lazima zikuumize kwa sababu ukiangalia tume haikumpendelea mtu yeyote lakini nilipata faraja baada ya matokeo yote kutoka.

Tuliendesha uchaguzi kwa ufanisi mkubwa pamoja na ushindani mkubwa lakini uliisha kwa amani hata wenzangu wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wakati ule wa uchaguzi walinieleza awamu hii…wakitegemea kwamba vurugu zingetokea lakini mwishoni wakashangazwa uchaguzi kumalizika kwa amani.

MTANZANIA: Ni changamoto gani ulizokumbana nazo ukiwa NEC?

JAJI LUBUVA: Uchaguzi uliopita changamoto kubwa ilikuwa ni mashine za BVR ambapo ulitumika mfumo mpya, tulikuwa tunahama na zile mashine lakini katika changamoto zote tulizozipata tulipewa ushirikiano mkubwa serikalini.

MTANZANIA: Unauzungumziaje ushindi wa Rais mpya wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), Fatma Karume?

JAJI LUBUVA: Nampongeza sana Fatma Karume. Fatma nimemfahamu wakati nikiwa Mwanasheria wa Zanzibar, nilikuwa nafahamiana na wazazi wake.

Alipoanza kazi ya sheria, mimi nilikuwa Mahakama ya Rufaa alikuwa kijana jasiri pamoja na kwamba hakuwa na uzoefu wa kutosha lakini alifanya kazi zake jinsi inavyostahili huku akisimamia kile anachokiamini.

Pia Fatma ana sifa nyingine kwa kuwa ni Mzanzibari hii inaonesha Tanzania tumekomaa kwa sababu tunadumisha Muungano wetu, wamechagua kwa kutoangalia anatoka wapi.

Nilifuatilia ule uchaguzi wa TLS ambao ulifanyika Aprili 14 mwaka huu na niliona vipaumbele vya Fatma, nakubaliana na vipaumbele vyake sina shaka navyo lakini  ni vyema nikashauri kwamba wazingatie suala la maadili na ujuzi katika taaluma yao.

Kwa maoni yangu, ingefaa wakaongeza pia na suala la maadili katika taaluma kwa mawakili na kuongeza ujuzi wao ambayo inasisitizwa katika kifungu cha 4 (1)(2) ya Sheria ya Mawakili  na ikizingatiwa wanasheria wengi waliopo hivi sasa ni vijana.

Pia TLS ifikirie utaratibu wa kuanzisha rasmi utaratibu au mfumo wa kuwa na mawakili wa ngazi mbalimbali yaani kuwe na mawakili waandamizi.

MTANZANIA: Unaizungumziaje TLS ya sasa na ya miaka iliyopita?

JAJI LUBUVA: Nisingependa kulizingumzia sana, unajua hivi wapo vijana wengi ambao ni wanasheria sasa katika hali kama hiyo lazima maadili yaangaliwe.

Isifike wakati kwamba mtu anazungumza kama mkereketwa wa chama fulani hivyo lazima wazingatie maadili na taratibu za sheria. Lazima kuwe na control mahali. Lazima liangaliwe kwamba mtu anazungumza kama mwanasheria au mwanachama wa chama fulani hilo lizingatiwe.

MTANZANIA: Unayazungumziaje mabadiliko ya kanuni yaliyoletwa na Serikali kwenye TLS,

JAJI LUBUVA: Serikali kuleta zile kanuni ni sawa, sasa iwe namna gani hayo ni masuala yao, TLS na Serikali lazima wakae wakubaliane na kuelewana na lazima kuwe na mamlaka ya kucontrol sasa jinsi hii ilivyo mimi details zake sizijui kama mwanasheria wa zamani na Jaji lazima kuwe na mamlaka ya kucontrol, sasa ni  suala la wao kukaa chini waone wafanyeje.

MTANZANIA: Tumeona baada ya mabadiliko hayo mijadala ilivyokuwa mikubwa, wapo watu wanasema kwamba mabadiliko hayo yamefanyika kwa lengo la kumbana Tundu Lissu ambaye amekuwa akiikosoa Serikali hadharani, hili unalionaje?

JAJI LUBUVA: Binafsi nisingependa kulizungumzia wala kujibu hoja zinazotolewa mitaani lakini ningesema kitu kwamba naona watu wangejielekeza juu ya madhumuni na malengo ya kuanzishwa TLS kutokana na lengo kuu la sheria na si siasa. Baadhi yao hawazingatii malengo ya kuanzishwa TLS si leo ni tangu zamani.

MTANZANIA: Hivi sasa wananchi wamepoteza imani na baadhi ya wanasheria kwa sababu wamekuwa wafanyabiashara badala ya kutoa msaada, hili nalo unalitazamaje?

JAJI LUBUVA: Kama kuna mwanasheria ambaye hazingatii sheria na maadili, TLS yenyewe isisitize kwa wanachama wake ili kurudisha imani ya wananchi kwa baadhi ya wanasheria, ukikosa imani na mwanasheria hata baadaye inakuja kuathiri kazi za mahakama. Kama wapo kwa kweli hawaendani na matarajio ya TLS.

MTANZANIA: TLS ina umuhimu gani kwa sababu wapo wanaoichukulia kama vyama tu vya kawaida

JAJI LUBUVA: TLS ni tofauti na vyama vingine ni ‘purely professional’ kwa maana ya jinsi sheria ilivyo, TLS si chama cha siasa wala cha biashara ni chama kinachoendesha shughuli zake kwa ajili ya kutetea haki, kusaidia wananchi katika masuala yanayohusu mahakamani.

Wakifanya kazi inavyotarajiwa itasaidia mahakama kufanya kazi zake  nzuri, Serikali kufanya shughuli zake kwa maana ya  kupata mchango wao kwenye miswada. Hiyo ndiyo msingi wa kufanya kazi zao kwa mujibu wa sheria.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles