WAKURUGENZI watendaji wa halmashauri nchini na makatibu tawala wa mikoa na wilaya wametakiwa kushughulikia majanga yanayotokea katika maeneo yao haraka vinginevyo watawajibishwa ikiwamo kuchukuliwa hatua kali za sheria.
Agizo hilo lilitolewa mjini hapa jana na Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais, Tamisemi, Utumishi na Utawala Bora, Suleiman Jafo.
Aliyasema hayo baada ya kutembelea maeneo mbalimbali ya Halmshauri ya Jiji la Arusha ikiwa ni pamoja na Shule ya Msingi Kisimani ambayo iliezuliwa na upepo mkali.
Jafo akiwa katika shuele hiyo, alionyesha kukerwa na utendaji kazi wa ofisa ununuzi wa halmashauri hiyo pamoja na Baraza la Wataalamu wa Jiji (CMT), katika kushughulikia ukarabati wa madarasa manne ya shule hiyo iliyoezuliwa na Desemba 4 mwaka jana.
“Nawaagiza wakurugenzi na Ma-RAS kote nchini, hii ni shule ya mwisho iliyokumbwa na maafa mimi kutembelea.
“Nikikuta kokote shule imepata majanga halafu mmekaa muda mrefu bila kushughulikia tatizo mtawajibishwa … kufanya hivyo mnaonyesha hamtoshi kwenye nafasi zenu,” alisema Jafo
Alimtaka Mkurugenzi wa Jiji, Juma Idd na timu ya wataalamu wa jiji hilo kuandika maalezo kwa Waziri wa Tamisemi kwa nini ukarabati wa madarasa hayo umechelewa na kwa nini wasichukuliwe hatua.
“Ofisa ununuzi wenu hapa hatoshi inawezekana kazi nyingi anazichelewesha … huu ni uzembe wa hali ya juu na hauvumiliki, ingekuwa ni halmashauri ya vijijini ni sawa.
“Lakini hapa mjini na fedha zipo kwa nini mcheleweshe ukarabati? Shule imeezuliwa Desemba leo ndiyo ukarabati unaanza?” alihoji Jaffo.