28.6 C
Dar es Salaam
Monday, December 9, 2024

Contact us: [email protected]

Jafo ataka DC acharaze viboko watendaji

RAMADHAN HASSAN-DODOMA

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Selemani Jafo, amemtaka Mkuu wa Wilaya (DC) ya Chamwino, Vumilia Nyamoga, kuwachapa viboko watendaji wa halmashari yake kwa kushindwa kupima viwanja.

Agizo hilo alilitoa jana jijini hapa wakati wa utiaji saini miradi mikubwa miwili ya ujenzi wa hoteli ya kisasa na kitega uchumi katika Jiji la Dodoma inayotarajiwa kutekelezwa na jiji hilo.

Jafo alisema mkuu huyo wa wilaya anatakiwa kuwaita watendaji wote wa halmashauri hiyo na kuwahoji ni kwanini wameshindwa kupima viwanja wakati Jiji la Dodoma wao wanafanya vizuri.

“Nenda kawachape viboko viwanja vipimwe, watu wamekalia majungu tu eti kwanini Dodoma wao kila siku wanapima, hapo Chamwino hawajapima eneo hata moja licha ya kuwapa Sh milioni 500 kwa ajili ya kupima.

“DC kawaite, waulize kisha washughulikie, wanakutia aibu, pale ndio Ikulu, fedha tumewapa,” alisema Jafo.

Aidha, Jafo alimpongeza Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi kwa kufanya kazi vizuri, huku akizitaka halmashauri na majiji nchini kuiga kutoka Jiji la Dodoma jinsi ambavyo linafanya kazi.

“Mnyonge mnyongeni haki yake mpeni, Kunambi unafanya kazi nzuri sana.

“Licha ya kukusanya mapato, lakini pia wanafanya vizuri katika miradi ya maendeleo, kwani wametenga zaidi ya Sh bilioni 54 kwa ajili ya miradi ya maendeleo, hongera sana mkurugenzi,” alisema.

Jafo aliwataka watendaji kusimamia miradi kuhakikisha inakamilika kwa wakati na ikiwa na ubora.

Aidha, aliwataka watendaji katika wizara yake na baadhi ya vijana kuacha maigizo na kufanya kazi kwa bidii kwani wengi wamekuwa wakipenda waonekane wanafanya kazi kwa kujipiga picha na kuweka katika mitandao ya kijamii ya instagram na whatsapp.

“Watu wanataka tu kusifiwa, waache maigizo, watu wanapenda kuonekana wanapiga picha kisha wanaweka katika instagram na whatsapp, kwamba wao wanafanya kazi, lazima tukubali vijana wa Dodoma wanafanya vizuri, Kunambi na Mavunde wapo vizuri,”alisema

Aidha, alizitaka halmashauri na majiji kuwapa miradi wale ambao wana uwezo, akitolea mfano Kampuni ya Mohammed Builders kwa jinsi ambavyo wamejenga stendi na soko la kisasa mkoani Dodoma.

“Mkurugenzi wape kazi wenye uwezo, mhakikishe mnawasimamia katika utendaji kazi wao,” alisema Jafo.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Binilith Mahenge, alimpongera Rais Dk. John Magufuli kwa kuupa hadhi mkoa huo kutokana na miradi mingi kutekelezwa na Serikali kuhamia mkoani humo.

“Kwa niaba ya wakazi wa Dodoma, tunakushukuru Rais, azma ya kuhamishia Makao Makuu hapa imekuwa na tija kubwa kwetu. Dodoma imepata fursa kubwa katika uchumi,” alisema.

mwisho

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles