30.1 C
Dar es Salaam
Saturday, June 15, 2024

Contact us: [email protected]

Jacob: Ajenda za Ukawa zimeibeba Halmashauri ya Kinondoni

Boniface Jacob
Boniface Jacob

Na ARODIA PETER,

ILIKUWA tetesi, minong’ono, lakini sasa ni rasmi kwamba Wilaya ya Kinondoni imegawanywa na kuzaliwa nyingine mpya ya Ubungo.

Mgawanyo huo ulihitimishwa wiki iliyopita, baada ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kinondoni,  Aron Kagulumjuli, kutangaza rasmi kugawanywa kwa halmashauri hiyo ambapo madiwani wa kata na viti maalumU kila mmoja atabaki katika wilaya na halmashauri husika.

Akizungumzia mgawanyo huo wa wilaya, Meya wa Halmashauri ya Kinondoni, Boniface Jacob, ambaye anawakilisha vyama vya Ukawa, alisifu mgawanyo huo ambapo alisema unakwenda kusambaza maendeleo yatakayochagizwa na ajenda ya mabadiliko kwa usimamizi wa Ukawa.

Mchakato wa kuigawa Wilaya ya Kinondoni ulianza kuchagizwa na aliyekuwa Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema) bungeni, akijenga hoja kwamba halmashauri hiyo licha ya kuwa na wabunge watatu wakati huo, wasingeweza kuleta maendeleo yanayohitajika kwa kasi.

Wilaya ya Kinondoni ina jumla ya wakazi milioni 2.2, idadi ambayo hairuhusiwi kwa mujibu wa sheria za Serikali za mitaa kuendelea hivyo bila kugawanywa.

Mnyika alisema suluhisho pekee la idadi hiyo kubwa ya wakazi ni kuwa na halmashauri yake ambayo itakuwa na wataalamu wa kila idara.

Akizungumzia uongozi wake katika kipindi cha miezi saba aliyokaa madarakani kama Meya, Jacob anasema kitu ambacho ataendelea kukiwazia ni kutofikia ndoto yake ya kupeleka greda kubomoa maeneo ya wazi ambayo yalivamiwa na kumilikiwa na watu binafsi kinyume cha sheria.

“Ingawa nafurahia kuzaliwa kwa halmashauri mpya ya Ubungo, lakini kiukweli ‘nimemisi’ kupeleka greda ili kumaliza vita ya maeneo ya wazi yaliyovamiwa na baadhi ya vyama vya siasa.

“Lakini pia kutokana na kasi tuliyokuwa tunakwenda nayo kama vyama vya upinzani, kuna barabara tano ambazo zitajengwa kwa kiwango cha lami ambazo ningekwenda kuzizindua, vitu hivyo nilikuwa nikiviwazia sana, lakini naamini meya mwingine ajaye kwa kuwa atatoka Ukawa atafanya kazi hiyo,” anasema Jacob.

Anazitaja barabara hizo kuwa ni Mwananyamala, Mkunduge, Mtogole hadi Viwandani na Msasani soko la samaki ambazo zitajengwa kwa kiwango cha lami.

Katika mazungumzo hayo na MTANZANIA, Jacob anasema katika muda waliokaa madarakani wamefanikiwa kuongeza kiwango cha fedha za mikopo kwa ajili ya vikundi vya vijana na wanawake katika Benki ya Biashara ya Dar es Salaam (DCB) kutoka Sh milioni 200 hadi Sh bilioni 2.

Anasema kasi yao hiyo ilikuwa na lengo la kufikisha Sh bilioni 5, kiasi ambacho wangekitumia kuanzisha benki kwa ajili ya vikundi hivyo.

“Aidha kuongezeka kwa mapato ya halmashauri hiyo kutoka Sh bilioni 45 hadi 67 na kuongezeka kwa vyanzo vya mapato kutoka 35 hadi 41 kumepunguza utegemezi kutoka asilimia 80 hadi 60 kutoka Serikali Kuu. Awali robo ya bajeti ya manispaa ilikuwa inatoka huko.

“Katika kutafuta vyanzo vipya vya mapato kupitia ushuru wa huduma tuliweza kuibua viwanda vidogo vidogo ambavyo vilikuwa mitaani, lakini halmashauri ya Kinondoni haikuwa inapata chochote.

“Katika kufanikisha hayo tuliwatumia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kujua mapato ya wahusika ambapo tuliweza kupata ushuru wetu halali na hivyo mapato yaliongezeka,” anasema.

Jacob anasema kwa njia hizo za ubunifu walipandisha bajeti ya awali ya Manispaa hiyo kutoka Sh bilioni 172 hadi Sh bilioni 235.

POSHO WENYEVITI WA MITAA

Ili kuwapa motisha ya kufanya kazi kwa kujituma na kuepuka vishawishi vya rushwa, Halmashauri ya Kinondoni kupitia Baraza la Madiwani waliamua kupandisha kiwango cha posho kutoka Sh 50,000 kwa wenyeviti wa Serikali za mitaa hadi Sh 100,000, huku wajumbe wakipandishiwa kutoka Sh 5,000 za awali na kuwa Sh 30,000 kwa mwezi.

“Nataka niwahakikishie wananchi kwamba Kinondoni ya Ukawa ni chungu, tulipiga marufuku na kuvikataa vimemo vya wakubwa.”

Anasema mmoja alikuwa na tenda ya kukusanya fedha za mabango kwa njia za wizi huku kigogo mwingine wa mkoa (anamtaja) alikuwa na kampuni ya usafi iliyokuwa inalipwa Sh milioni 79 kila mwezi.

“Tulibaini ‘open space’ zote (maeneo ya wazi) zinamilikiwa na watu wachache kupitia chama cha siasa, tumepambana nao na nyingine zimerudi na waliozikodisha tuliwaambia wazilipie kupitia halmashauri.

“Eneo la Biafra tumelichukua na sasa mapato yote yanaingia kwenye halmashauri, waliuza hadi makaburi, tumesitisha kibali cha kujenga katika eneo hilo, labda wasubiri kutuondoa 2020 ambako naamini wananchi bado wako na sisi wataendelea kutuamini,” anasema.

UCHAGUZI WA MAMEYA

Akizungumzia uchaguzi wa kuwapata mameya katika halmashauri za Kinondoni na Ubungo, Jacob anasema hakuna muujiza wowote unaoweza kutokea kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuongoza halmashauri hizo kutokana na uwiano wa idadi ya madiwani wa vyama vya CUF na Chadema chini ya mwavuli wa Ukawa.

“Kwa mujibu wa orodha ambayo tumekuwa tukiitumia katika Halmashauri ya Kinondoni na baada ya mgawanyo, Ukawa tuna madiwani wa kata 14 kati ya wawili wa CCM wakati Kinondoni Ukawa ina jumla ya madiwani 23 na wenzetu CCM wanao 16.

“Katika uchaguzi huu ni namba tu zinaongea na nataka niwaambie safari hii tunasubiri kuona kiwango cha ustaarabu wa CCM kama wataendeleza figisufigisu zao.”

Alipoulizwa kama madiwani wa Ukawa hawawezi kununuliwa wakatoa ushindi kwa CCM, anasema:

“Kwanza waelewe Ukawa hivi sasa hatuna njaa za rejareja, tumeridhika, tunachotaka ni kuonyesha utumishi si vinginevyo, wanaodhani kwamba wanaweza kuwahonga madiwani wa Ukawa wabadili fikra na mitazamo yao wajipange upya,” anasema.

CHANGAMOTO

Mbali na mafanikio aliyoyapata akiwa kwenye nafasi hiyo ya umeya, Jacob alikumbana na vikwazo kadhaa ambavyo ataendelea kuvikumbuka.

Mojawapo ya vikwazo hivyo, anasema ni kufanya kazi na watu ambao hawajawahi kwenda ‘jando la kisiasa’.

Anasema watu wa aina hiyo hawajui na hawana ustaarabu wa kuheshimu wenzao ambao wanatokana na wananchi.

“Naweza kusema hawa wateule wa Rais ni kikwazo, wao wanachojua ni kumnyenyekea mtu mmoja tu aliyewateua, lakini kwa watu ambao wanajua kuomba kura kwa wananchi wanajua thamani ya heshima kwa wanaowaongoza.

“Baadhi ya mambo tulishindwa kuyafanya kwa sababu hatukupewa nafasi ya kusikilizwa na viongozi wakuu wa Serikali. Walituona wasaliti, lakini kama wangetupatia nafasi tungeweza kuwaonyesha wale wanaowakwamisha katika utendaji wao wa kazi,” anasema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles