24.7 C
Dar es Salaam
Saturday, April 13, 2024

Contact us: [email protected]

Tetemeko Kagera ni elimu tosha kwa nchi yetu

dv2a3192

NAPENDA kuanza kwa kutoa pole kwa wote walioguswa na maafa yaliyotufika katika  nchi yetu siku za hivi karibuni kutokana na tetemeko kubwa la ardhi  lililotokea Kanda ya Ziwa hususan Mkoa wa Kagera.

Tetemeko hilo limesababisha vifo kwa watu wapatao 19 hadi sasa na majeruhi 253, kwa mujibu wa vyombo vya habari. Pia  imesemekana maelfu ya wananchi wamekosa makazi kwani nyumba kama 849 zimeanguka huku 1,264 zikiwa zimepata nyufa.

Hili si tetemeko la kwanza nchini bali athari zake zimekuwa kubwa zaidi. Huwa kuna matetemeko madogo madogo ambayo hutokea hapa na pale. Nakumbuka mwaka 2009 nikiwa kwenye utafiti huko Makete Mkoa wa Njombe kwa sasa, lilitokea tetemeko tukiwa ndani ya nyumba.

Tuliogopa lakini hatukujua cha kufanya, iwapo tutoke nje au tubaki ndani. Bahati nzuri lilipita na hapakuwa na madhara yoyote.

Tetemeko la Kagera limetokea na kuleta madhara makubwa zaidi kama nilivyotaja hapo juu. Mara baada ya tukio hilo, ndio tumeanza kusikia taarifa mbalimbali kuhusu matetemeko  ya ardhi na si kabla. Kuna waliohusisha tetemeko na kupatwa kwa jua. Kuna waliohusisha na masuala ya imani na kuwa watu wanaonyeshwa ukuu wa Mungu ili waache maovu na kadhalika.

Jambo ambalo nimejifunza katika tukio hili la tetemeko huko Kagera ni kuwa, kama nchi  tuna uhitaji mkubwa sana wa kuwa na maandalizi ya matukio ya maafa kama hili, hasa elimu kwa kutoa elimu. Ni kweli kuwa zipo nchi nyingi sana ambazo zimeshakumbwa na matukio kama haya na nyingine ni tajiri sana na zenye uwezo mkubwa na pia matukio yaliyotokeo kwao yalikuwa na maafa makubwa zaidi kuliko haya ya kwetu kama alivyoeleza vizuri Rais John Magufuli.

Tofauti pengine kwa hili lililotokea hapa pamoja na kuwa maafa yake kwa ulinganifu si makubwa kama tuliyowahi kusikia huko katika nchi nyingine, ukweli ni kuwa hapa kwetu hili bado ni tukio kubwa kwa ulinganifu na matukio mengine ya aina hii hapa nchini.

Pia tofauti nyingine ni kuwa sisi bado hatuelekei kuwa tayari katika maeneo ya  kitaaluma, kirasilimali na hata uelewa wa wananchi.

Tatizo ni kwamba tulikutwa bila kuwa na utayari wa kutosha. Kwanza tulisikia kuwa hakuna uwezekano wa kujua kuwa tetemeko litatokea kama ilivyo utabiri wa hali ya hewa.

Baadaye tulisikia kuwa vifaa vya kupimia tetemeko vilikuwa vimeibwa. Nilijiuliza hivi vifaa viliibwa lini na mamlaka husika ilipata taarifa lini au waligundua wizi huo baada ya tetemeko hili?

Nilipata jibu kupitia baadhi ya vyombo vya habari kwa maelezo ya mjiolojia mhusika, kuwa vifaa hivyo vilikuwepo sehemu mbalimbali lakini vituo vikubwa vitatu vya kupimia mitetemo vilifungwa kutokana na hujuma na vingine vidogo 38 navyo vilifungwa baada ya wafadhili kujitoa. 

Hivyo ni kweli kuwa tetemeko huweza kupimika ili kujua uwezekano wa kutokea  kwake, ila sisi kwa sababu hizo ndio lilituzukia bila kujua.

Jambo jingine lililokuwa wazi ni kuwa tetemeko lilipopiga wengi walioathirika katika Mkoa wa Kagera kama si wote, walikuwa hawajui nini cha kufanya katika hali kama ile. Hata lingetokea seheme nyingine yoyote huenda haki ingekuwa vile vile.

Tuliwaona watu walionusurika wakielezea jinsi wengine waliokuwa kwenye hoteli walivyokimbilia kwenye ‘lift’ ili washuke. Wengine wakajieleza jinsi walivyokimbilia kwenye kituo cha mafuta ya petroli.

Wengine walirudi katika nyumba zao na tetemeko likarudia wakati wengine waliogopa kurudi nyumbani kwa vile hawakujua litakuja tena au la. Yote haya yanaonyesha kutokuwa na taarifa sahihi kuhusu tetemeko.

Ni baadaye ndipo tumesikia wataalamu walieleza kuwa tetemeko likipiga kama hivyo, ni kawaida kuwepo kwa marudio  ya matetemeko madogo madogo mengine na haya inasemekana huweza kudumu kuanzia   wiki mbili hadi miezi minne.

Kutojiandaa kwingine ni kukosekana kwa misaada ya haraka kwa wahanga. Pamoja na kuwa Serikali iliwahi kuwafikia wahanga mara baada ya tukio na hata kushiriki maziko ya waliopoteza maisha, lakini wale walionusurika wakiwa hawana makazi na mahitaji mengine hawakufikiwa na msaada kwa uharaka uliotazamiwa.

Na bahati mbaya pia siasa zikapata nafasi  kiasi cha watoa msaada wengine kuzuiwa. Ni wazi kuwa hata uwezo wa kusaidia haukuwa tayari kwa kiwango kilichohitajika ndio maana michango ilibidi ianze kutafutwa.

Hakuna lawama hapa ila ni kujifunza na kutumia elimu tuliyoipata na hata tutakayoipata baadaye katika kujiweka tayari kwa haya na mengine kama walivyojieleza wataalamu wa jiolojia kuwa ipo haja ya kukuza tafiti katika eneo hili.

Si kwa hili tu bali kitengo cha maafa kishirikiane na wataalamu mbalimbali katika kujiandaa kwa maafa yanayoweza kutokea ili kupunguza machungu ya uhanga.

Mwandishi ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles