24.4 C
Dar es Salaam
Thursday, October 31, 2024

Contact us: [email protected]

ITAKUWA MSHIKE MSHIKE BUNGENI

Na AGATHA CHARLES.

KIKAO cha Bunge la Bajeti kinachotarajiwa kuanza kuketi Aprili 4, mwaka huu mjini Dodoma, huenda kikatawaliwa na hoja kuu 10 zitakazotikisa mhimili huo.

Miongoni mwa mambo ambayo yanatazamiwa kulitikisa Bunge na kuchambuliwa kwa kina na wabunge ni pamoja na mjadala wa Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2017/2018.

Mambo mengine ni Uchaguzi wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), kuvamiwa kwa Kituo cha Clouds, sakata la Nape Nnauye, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, mwenendo wa Serikali pamoja na mchanga wenye madini.

Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2017/2018

Mapendekezo ya mwelekeo wa Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2017/2018 yaliyowasilishwa na Waziri wa Fedha, Dk. Philip Mpango kwa Kamati za Bunge wiki iliyopita, yanatarajiwa kuibua hoja nzito dhidi ya Serikali.

Hoja hiyo inadaiwa itajikita zaidi kuangalia uwiano wa utekelezaji wa bajeti iliyopita ya Sh trilioni 29.5 na ile ya sasa ambayo inakadiriwa kufikia Sh trilioni 32.

Tayari kuna wasiwasi utekelezaji wa bajeti hiyo mpya hasa ikizingatiwa ile ya mwaka huu ni shilingi trilioni 3.9 tu ndizo zilizotolewa kwa ajili ya maendeleo.

Wakati baadhi ya wasomi wakidai kuwa bajeti iliyopita ilishindwa kutekelezwa kutokana na kuwapo matumizi nje ya yaliyopangwa, tayari baadhi ya wabunge nao wameonyesha mtazamo unaoshabihiana na huo na hivyo kutoa mwelekeo wa kile ambacho kitajiri ndani ya Bunge.

Mbunge wa Malindi (CUF), Ally Abdulla Saleh, amekaririwa wiki hii akisema mapendekezo ya bajeti ya 2017/2018 si mbaya lakini utekelezaji unapaswa kufanyika kwa kuwa hata bajeti ya mwaka uliopita haijatekelezwa ipasavyo.

Kwa upande wake Mbunge wa Chumbuni (CCM), Ussi Pondeza, naye amekaririwa akisema mwelekeo wa bajeti mpya bado haujakaa vyema kwa sababu mipango mingi haijatekelezwa katika bajeti iliyopita.

Mbunge wa Nzega Mjini (CCM), Hussein Bashe, licha ya kusema Serikali imefanya kazi kubwa kutimiza matarajio ya Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) ya kukusanya mapato ya ndani ambayo yamefikia zaidi ya asilimia 95, lakini bajeti ya mwaka 2016/2017 inakabiliwa na changamoto ya mapato ya nje na mikopo.

Katika ongezeko la bajeti, alisema limelenga mapato yatokanayo na kodi ambayo yataendelea kuwakamua wafanyabiashara ambao kwa sasa biashara zao zipo kwenye hali mbaya na wengine wamezifunga.

Mwenendo wa Serikali, kuvamiwa Clouds, sakata la Nape

Hizi ni hoja nyingine ambazo zimetoa mwelekeo wa kulitikisa Bunge hili la bajeti kutokana na kauli zilizotolewa hivi karibuni na wabunge.

Mbunge wa Kibamba, John Mnyika, amekaririwa akisema Watanzania watarajie Bunge la Bajeti kuwaka moto.

Hilo alilieleza linatokana na mambo mbalimbali yanayoendelea nchini ikiwemo hali ya siasa pamoja na kushikiwa bastola kwa aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye.

Hoja inayofanana na hiyo ni ile iliyotolewa na Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu (CCM), ambaye yeye ameonekana kuguswa na uvamizi uliotokea Clouds na kitendo cha mtu ambaye tayari Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imekana kuwa si polisi, kumshikia bastola Nape.

Katika ukurasa wake wa Twitter, Nyalandu aliandika: “Katika kutekeleza wajibu wake Kikatiba, Bunge ni sharti lijadili na kutoa azimio kuhusu kilichojiri Clouds Fm na Uhuru wa Vyombo vya Habari.

Zaidi aliandika: “Kupitia Bunge, nitaiomba Serikali ichukue hatua za kinidhamu na kisheria dhidi ya Ofisa aliyemtishia Nape kwa silaha. Kitendo hicho hakikubaliki.”

Uvamizi huo pia ulilaaniwa na Kiongozi wa Kamati ya Huduma ya Maendeleo ya Jamii ya Bunge, Peter Serukamba na Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambao walisema wanasubiri ripoti ya Kamati ya Nape ili nao watoe maoni.

Katika hilo, Mbunge wa Singida Magharibi, Elibariki Kingu (CCM), alisema yuko tayari kufukuzwa uanachama kama kupinga matendo ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam itaonekana ni usaliti.

Mbunge Bashe kupitia Twitter alipongeza namna Kamati iliyoundwa na Nape ilivyowasilisha ripoti yake.

Uchaguzi EALA

Tayari dalili la suala hilo kuteka mijadala ya vikao vya mwanzo vya Bunge zimeanza kuonekana hasa upinzani na wale walioshindwa kwa kura kwa upande wa CCM.

Wakati mapendekezo ya majina 12 ya wagombea kutoka CCM yakidaiwa kugubikwa na figisu figisu, nafasi mbili za Chadema nazo huenda zikaibua msuguano na vyama vingine vya upinzani ndani ya Bunge.

Miongoni mwa wanaolalamikia mchakato wa ndani ya CCM ni Mbunge wa Bunge hilo anayemaliza muda wake, Shy-Rose Bhanji, ambaye amekaririwa akisema Mwenyekiti wa CCM, Rais Dk. John Magufuli, ndiye aliyeshinikiza jina lake likatwe.

Kupitia mtandao wa kijamii, Shy-Rose alisema: “Kwa habari nilizozisikia ni kwamba Mwenyekiti wa CCM, Rais JPM katika kikao cha CC (Kamati Kuu) ilipofikia jina langu kujadiliwa akasema, ‘huyu wala sitaki tumjadili, sitaki hata kumsikia.’

“Naambiwa wajumbe kama wanne walinyoosha mkono lakini akawakatalia na kusema mjadala umefungwa,” aliandika Shy-Rose.

Shy-Rose alikatwa jina lake katika Kikao cha Kamati Kuu ya CCM chini ya Dk. Magufuli sambamba na la Angella Kizigha licha ya kuongoza katika kura za maoni.

Hata hivyo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole, alikana hilo na kudai si kweli kwamba Rais Magufuli alikata jina hilo kwa hila bali majina yote yaliyowasilishwa CC yalikuwa mazuri.

Si CCM tu ambacho kina figisu figisu hizo kwani kwa upande wa upinzani nako kuna sintofahamu kuhusu nafasi zinazogombewa.

Chadema ambao wamepitisha majina mawili kwa idadi kama hiyo ya nafasi zao, tayari vyama vya NCCR-Mageuzi na ACT-Wazalendo navyo vimependekeza jina moja moja.

ACT-Wazalendo kimemteua Profesa Kitila Mkumbo huku NCCR-Mageuzi kikimpitisha Nderakindo Kessy.

CUF ambacho kina mgawanyiko na kinatakiwa nafasi moja kwa mujibu wa mwongozo, tayari upande unaoongozwa na Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad, ulimpitisha Mbunge wa EALA anayemaliza muda wake, Twaha Taslima na upande wa Mwenyekiti anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa Profesa Ibrahimu Lipumba, nao ukidaiwa kumteua mtu.

Zitto Kabwe ambaye ni Kiongozi wa ACT-Wazalendo, ameliandikia Bunge barua kutaka Kamati ya Kanuni za Bunge ikutane kujadili uchaguzi wa wajumbe wa Tanzania kwenye Bunge la Afrika Mashariki.

Wadadisi wanadai barua hiyo inadai mwongozo uliotolewa na Bunge umekwenda kinyume na Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki huku ikielezwa kuwa endapo hoja ya Zitto ikikubaliwa ni rahisi Chadema kukosa nafasi hizo na badala yake nafasi za upinzani kwenye Bunge la Afrika Mashariki zikachukuliwa na wagombea wa ACT na wale wa CUF.

Hilo linaelezwa kuchangiwa na wabunge wengi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano kuwa ni wa CCM, hivyo ni rahisi kuweka msimamo wa kuwapigia kura wale wagombea wa ACT Wazalendo na wale wa CUF badala ya wale wa Chadema kutokana na upinzani wa kisiasa uliopo baina yao.

Kuhojiwa RC Dar es Salaam

Licha ya Mkuu huyo wa Mkoa wa Dar es Salaam kuitwa na kuhojiwa na Kamati ya  Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge juu ya tuhuma zinazomkabili za kudaiwa kuingilia mhimili huo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, George Mkuchika, amekaririwa akisema kuwa taarifa yake ataiwasilisha kwa Spika wa Bunge, Job Ndugai.

Taasisi za Serikali kutumiwa vibaya

Hoja hii inapewa uzito wa hali ya juu, kutokana na yale yaliyowapata wabunge wawili wa Chadema, Godbless Lema wa Arusha Mjini na Peter Lijualikali wa Kilombero.

Wabunge hao ambao hivi karibuni wameachiwa na mahakama za juu mmoja kwa dhamana na mwingine akifutiwa kesi, wameapa kulifikisha jambo hilo katika mhimili wa Bunge.

Kuingiliwa majukumu

Hoja hii inatazamwa kuchukua mjadala hasa baada ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Viwanda na Biashara, Dk. Dalali Kafumu na Makamu wake Vick Kamata (Viti Maalumu (CCM-Geita) kujiuzulu nafasi zao kwa kile walichodai kuwa Serikali imekuwa ikiingilia majukumu yao katika utendaji wao.

Kwa sababu hiyo Spika wa Bunge, Ndugai, atalazimika kuteua viongozi wengine wapya.

Mchanga

Sakata la mchanga wenye madini nalo ni wazi linaweza kuibua mjadala mpana bungeni hasa kupitia wabunge wenye utaalamu wa madini.

Tayari Spika Ndugai ametangaza  kuunda Kamati teule itakayochunguza biashara ya kusafirisha nje ya nchi mchanga huo unaodaiwa kuwa na madini ikiwemo dhahabu inayofanywa na wawekezaji wa mgodi wa Bulyanhulu na Buzwagi.

Itakumbukwa Rais Dk. Magufuli ndiye aliliibua sakata hili baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika Bandari ya Dar es Salaam.

Alisema Watanzania wanahitaji kujua biashara hiyo ya mchanga wa dhahabu inafanywa vipi, nani wanafaidika tangu usafirishaji wake uanze mwaka 1998.

Hata hivyo, taarifa kutoka vyanzo vya ndani ya Bunge zinadai kuwa upo uwezekano mkubwa wa wabunge wa CCM kuwa upande wa Serikali ingawa baadhi yao waliozungumza na gazeti hili wanasema ni vigumu kulitabiri hilo kwa sasa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles