26.6 C
Dar es Salaam
Wednesday, January 19, 2022

MCHANGA WA MADINI KUONDOKA NA VICHWA

Na MWANDISHI WETU,

UAMUZI wa Rais Dk. John Magufuli kuzuia kontena zaidi ya 260 za mchanga wa madini zilizokuwa zimehifadhiwa katika Bandari Kuu ya Dar es Salaam (TPA) kwa lengo la kusafirishwa kwenda nje kwa hatua zaidi za kuchakatwa, unatafsiriwa kuwa na mwelekeo wa kung’oa vichwa zaidi vya watu kwenye mamlaka za usimamizi.

Taarifa kutoka kwenye mifumo mbalimbali ya kiserikali zinadai kwamba, Rais Magufuli amechukua uamuzi wa kuzuia usafirishaji wa mchanga huo wa dhahabu kwa sababu ya kuwapo hisia za rushwa ambazo zinaelekezwa kwa watendaji wa mamlaka za ndani ya nchi zinazohusika na usimamizi wa masuala ya madini.

Mamlaka zinazonyooshewa kidole katika sakata hilo ni Wakala wa Madini Tanzania (TMAA), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) pamoja na Wizara ya Nishati na Madini (MEM).

Tayari Rais amekwishatengua uteuzi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa, ambaye alipinga madai ya kwamba mchanga huo una kiwango kikubwa cha madini ya dhahabu kama inavyoshukiwa.

Pia hatua ya Rais Dk. Magufuli kuunda kamati ya wataalamu wanane ambao watachunguza mchanga huo ili kupata ukweli kama una kiwango kikubwa cha dhahabu au la, unaweza kutoa mwelekeo wa uamuzi mwingine mpya.

Ndani ya mifumo hiyo ya Serikali zipo hisia kwamba, uamuzi huo wa Rais Dk. Magufuli huenda ukawa umeambatana na kuwako kwa taarifa nyeti za awali zilizomfikia kuhusu madini.

Wakati kukiwa na mtazamo huo, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Madini (TMAA), Gilay Shamika, ameweka bayana kuwa kiwango cha dhahabu kilichopo ndani ya makontena yaliyokamatwa ni 0.02, madini ya fedha ni 0.08 na asilimia 90 ni madini ya shaba.

Akielezea mchakato wa kupakia mchanga huo, Shamika alisema kwamba huwa wanachukua sampuli za mchanga na kufanya vipimo na wanapojiridhisha kiasi cha madini kilichomo ndio wanawaruhusu wawekezaji kulipa kodi TRA.

“Tukishajiridhisha tunalifunga kontena na kuweka alama yetu na ya TRA kama inavyoonekana kwenye kontena,” alisema Shamika.

Mtaalamu wa miamba ambaye amepata kufanya kazi katika migodi mikubwa yote hapa nchini aliyejitambulisha kwa jina moja la Abdul, ameliambia MTANZANIA Jumapili kuwa, mgodi wa Bulyanhulu na Buzwagi asilimia 70 ya dhahabu hupatikana kupitia uchakataji unaofanywa pale pale mgodini kabla ya kupeleka mchanga kwa ‘smelters’ wa nje ya nchi.

Abdul, ambaye kwa sasa anafanya shughuli zake nchini Afrika Kusini, anasema  asilimia 30 ya madini yanayobaki kwenye mchanga baada ya uchakataji wa pale mgodini huwa ni mchanganyiko wa dhahabu ambayo ni asilimia 25, shaba na madini ya fedha.

Kutokana na mitazamo tofauti ya wataalamu kama hiyo, wafuatiliaji wa mambo ambao upande mwingine wanauona uamuzi wa Rais Magufuli wa kuzuia usafirishaji wa machanga wa madini kuwa unakiuka sheria, lakini wanasema huenda kisera akawa sawasawa.

Mbunge wa Igunga, Dk. Dalaly Kafumu (CCM), ambaye ni mtaalamu wa madini, kwa upande mmoja anaunga mkono uamuzi huo wa Rais wa kukagua mchanga wa madini, lakini anatoa tahadhari juu ya uharaka alioufanya wa kuzuia usafirishaji wa mchanga huo kwa sababu unaweza kulisababishia Taifa hasara ya kupoteza mapato.

“Sera ya Madini ya mwaka 2009 (niliyosimamia utengenezaji wake); kifungu 5.11; policy statement No. 3 inasema hivi; (iii) The Government will collaborate with the private sector, regional and international organisations to strategically invest in smelting and refining”.

Jambo linalozua maswali na hata baadhi kudhani kwamba huenda Rais Magufuli anajua analolifanya ni kwamba, suala hilo limeibuka ikiwa imepita takribani miaka tisa tu tangu aliyekuwa Rais wa awamu wa nne, Jakaya Kikwete, aunde Kamati ya ushauri kuhusu madini iliyoongozwa na Jaji Mark Bomani.

Kamati hiyo, pamoja na mambo mengine, ilishauri marekebisho ya sheria ya madini ya mwaka 1998, na kushuhudia sheria mpya ya mwaka 2010.

Mapema mwaka jana, Jaji Bomani akizungumza kama Mwenyekiti wa Kamati ya Uhamasishaji wa Uwazi Katika Mapato ya Madini, Gesi na Mafuta (Teiti), alieleza mafanikio ya ushauri huo walioutoa, akisema kiwango cha Serikali kupoteza mapato ya madini kimeshuka kutoka bilioni 66 mwaka 2009 hadi kufikia bilioni sita mwaka 2014.

Si hilo tu, aliyataja mafanikio mengine kuwa ni mapato ya Serikali kupanda kutoka bilioni 28 hadi trilioni 1.2, ikiwa ni ongezeko la asilimia takribani 10, hata hivyo, alisisitiza kuwa mapato yangeongezeka zaidi kama hatua zingechukuliwa.

Hatua hizo, ambazo zimo kwenye mapendekezo ya ripoti ya kamati yake, ni pamoja na mrabaha unaotolewa na kampuni za madini ya dhahabu kuongezwa kutoka asilimia tatu hadi kufikia tano, ingawa Serikali ya Kikwete iliongeza hadi asilimia nne.

Pili, mrabaha usiwe faida zilizopata kampuni hizo, bali jumla ya mauzo.

Hata hivyo, alisema pendekezo lao la kutaka asilimia 60 ya mauzo ya kampuni za madini yarejeshwe nchini, halikukubaliwa.

Pamoja na kwamba Jaji Bomani amekuwa na mtazamo huo, wakati fulani Mwanasheria kutoka Chuo Kikuu cha Harvard cha nchini Marekani, Dk. Mshala Rugemeleza, aliwahi kunukuliwa na gazeti moja la kila siku hapa nchini akidai sheria ya madini ya mwaka 2010 ambayo ni matokeo ya ushauri wa Kamati ya Jaji Bomani, inalinda kwa kiasi kikubwa wawekezaji wa madini kutoka nje.

Dk. Nshala, ambaye ni Mkurugenzi wa Loyers Environment Action Team (LEAT), alisema vipengele vingi vya sheria hiyo vinabebwa na mkakati madhubuti wa Benki ya Dunia, uliowekwa mwaka 1992 ambao unazipuuza Serikali za Afrika kwa hoja ya kwamba, hazina uwezo wa kumiliki mfumo wa uchimbaji wa madini, hivyo mifumo hiyo iwe chini ya miliki ya makampuni binafsi kutoka nchi za Magharibi.

Machapisho mbalimbali yaliyotolewa mwaka 2007, 2008 na 2009 yanaonyesha namna bara la Afrika linavyoibiwa katika sekta ya madini na kubaki masikini.

 Takwimu zinaonyesha kuwa, nchi ya Ghana, licha ya uzalishaji wa madini kuwa mkubwa mwaka 2001, kodi ya mapato ambayo nchi hiyo ilipata ni Dola milioni 31 tu, ambayo ni asilimia nne ya mapato yatokanayo na makusanyo ya kodi za nchi hiyo kwa mwaka.

Kwa hapa Tanzania, takwimu za kuanzia mwaka 2002 hadi 2007, nchi ilipata Dola milioni 21.7, kati ya madini yenye thamani ya Dola bilioni 2.5 na ndani ya kipindi hicho watu 400,000 walipoteza ajira migodini.

Mambo kama haya ndiyo ambayo wakati huu yamekumbusha kile kilichopata kutahadharishwa na Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, juu ya uharaka wa kuruhusu uwekezaji wa madini hapa nchini.

Nyerere alisema uwekezaji wa sekta hiyo usubiri hadi hapo nchi itakapopata wataalamu wa kutosha ambao wataweza kutunga sheria na kusimamia sera zitakazoisimamia sekta hiyo kwa manufaa makubwa ya Taifa.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
175,234FollowersFollow
531,000SubscribersSubscribe

Latest Articles