32.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

ISRAEL YASALIMU AMRI MPANGO WA KUWAFUKUZA WAHAMIAJI WAAFRIKA

TEL AVIV, ISRAEL


SERIKALI ya Israel hatimaye imefuta mpango wa kutaka kuwatimua kwa lazima maelfu ya wahamiaji haramu wa kutoka Afrika kufuatia shinikizo la ndani na kimataifa.

Katika barua iliyoiandikia Mahakama ya Juu Israel, Serikali imesema kuwatimua kwa lazima wahamiaji kutoka mataifa ya Afrika si ajenda yao kuu.

Hata hivyo, maafisa wa uhamiaji wa Israel bado wanatafuta njia za kuwahamisha wahamiaji hao kwa hiari, ilisema barua hiyo.

Hatima ya wahamiaji haramu takriban 30,000 kutoka mataifa ya Afrika imekuwa ni suala linalozusha mzozo mkubwa.

Awali Mahakama ya Juu nchini hapa iliitaka Serikali kusitisha mipango ya kuwahamisha wahamiaji hao wengi wao kutoka Eritrea na Sudan, ambako hawawezi kurudi kwa hofu ya usalama wao.

Mahakama ilitaka wahamiaji hao wahamishwe iwapo tu watakubali kwa hiari kupokea kitita cha fedha na tiketi ya ndege kutoka Israel.

Kufuatia uamuzi wa Mahakama, Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu, akafutilia mbali makubaliano na Umoja wa Mataifa (UN) kuwatafutia makazi wahamiaji hao katika mataifa ya magharibi.

Chini ya makubaliano hayo, Israel ilitakiwa kutoa makazi ya muda kwa wahamiaji kisha kuwatafutia ng’ambo.

Uamuzi wa Netanyahu kufutilia makubaliano na UN ulishutumiwa vikali ndani na nje ya nchi huku baadhi ya Waisrael wakisema unaitia doa taswira ya nchi hiyo kimataifa.

Siku ya Jumatatu, Wabunge 18 wa Chama cha Democratic nchini Marekani walimuandikia Netanyahu barua wakimweleza kushangazwa na kuvunjwa moyo kwao kwa hatua yake kufutilia mbali makubaliano na UN.

UN imesema uamuzi huo inakiuka sheria za Israel na kimataifa na pia hatua hiyo ilishuhudia maandamano makubwa nchini Israel kumpinga Netanyahu kwa ukiukaji wa sheria na kuitia doa nchi hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles