ISRAEL imedai kuwa Kiongozi wa Wapalestina, Mahmoud Abbas, huenda alikuwa akilifanyia kazi lililokuwa Shirika la Ujasusi la Umoja wa Kisovieti wa Urusi (KBG) miaka ya 1980.
Watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Hebrew mjini Jerusalem, walisema stakabadhi zilizopatikana katika makavazi ya Chuo Kikuu cha Cambridge, Uingereza  zinaonyesha Abbas alikuwa mjumbe wa KGB wakati akiishi mjini Damascus, Syria.
Msemaji wa Abbas ameelezea madai hayo kama yasiyo na msingi yanayotolewa na Israel kiholela.
Alisema kuwa madai hayo yamebuniwa kwa lengo la kuzuia juhudi za hivi karibuni za Serikali ya Urusi kuanzisha upya mazungumzo ya amani baina ya Waisraeli na Wapalestina.
Mapema wiki hii, kiongozi huyo wa Palestina alisema kuwa amekubali kukutana na Netanyahu mjini Moscow siku ya Ijumaa, lakini maofisa wa Israel waliomba mkutano huo uahirishwe hadi tarehe nyingine ambayo haikutajwa.