TEHRAN, IRAN
SERIKALI ya Iran inasema imefanyia majaribio kombora la Khorram-shahr. Kombora hilo lilionyeshwa hadharani katika maonyesho ya kijeshi juzi nchini humo.
Aidha, Serikali ya Iran imesema kuwa, kombora hilo linaweza kusafiri mwendo wa kilomita 2,000. Hatua hiyo ni sawa na ile iliyofanywa na Korea Kaskazini, ambayo ilirusha kombora lake kwa umbali wa kilomita 2,300 na kupita katika anga la Korea Kusini na Japan.
Wakati kombora la Iran lilipokuwa linarushwa, kituo cha runinga cha taifa cha nchi hiyo kilionyesha picha za sherehe hizo mubashara. Kombora la kwanza la Khorram-Shahr lilirushwa angani Januari, mwaka huu, lakini likalipuka katikati ya mwendo.
Jaribio hilo limefanyika siku chache baada ya Rais Trump wa Marekani kushambulia Iran katika hotuba yake katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Rais Donald Trump ametishia mara kadhaa kwamba anaweza kuyafuta makubaliano hayo, kutokana na Iran kufanya majaribio ya makombora, akidai yanalenga kuipa ujuzi wa kiufundi wa kurusha kombora la nyukilia, pale muda unaoelezwa katika ibara za makubaliano hayo kuizuia Iran kufanya hivyo utakapomalizika mwaka 2025.
Rais wa Iran, Hassan Rouhani, ametetea hatua ya taifa lake kuimarisha zana zake kwa lengo la kujitetea na kujilinda dhidi ya tishio lolote kutoka nje.
HATIMA YA NYUKILIA YA IRAN
Ifikapo Oktoba 15, mwaka huu, Trump anatazamiwa kuripoti mbele ya bunge, iwapo anaamini Iran inatekeleza upande wake wa makubaliano hayo, na ikiwa anadhani Marekani inayo maslahi katika kuendelea kuyazingatia makubaliano hayo.
Ikiwa Rais Trump atasema Marekani hainufaiki na makubaliano hayo, kauli yake itafungua njia kwa Bunge la Marekani kuvirejesha vikwazo dhidi ya Iran, na hali hiyo itaashiria kusambaratika kwa makubaliano yenyewe. Jumatano iliyopita, Trump alisema tayari amekwishachukua uamuzi, lakini bado muda wa kuutangaza hadharani haujawadia.
Pande nyingine zilizotia saini makubaliano hayo; Uingereza, Ufaransa, Urusi, China, Ujerumani na Umoja wa Ulaya, zimesema zinataka makubaliano hayo yaendelee kama yalivyo.
Iran imesisitiza kuwa imeheshimu upande wake wa makubaliano hayo, na hayo yamethibitishwa na Shirika la kimataifa la nishati ya atomiki, IAEA. Shirika hilo limesema makubaliano hayo hayana kipengele kinachogusa masuala mengine.
Katika hotuba yake mbele ya gwaride kubwa la kijeshi mjini Tehran Ijumaa, Rais wa Iran, Hassan Rouhani, aliapa kwamba Iran itaendelea na mpango wake wa kuunda makombora, bila kujali mfululizo wa maonyo kutoka Marekani.
”Siyo kwamba tutaimarisha mpango wetu wa makombora, tutaboresha pia uwezo wa jeshi la anga, nchi kavu na majini,” alisema Rouhani, katika hotuba hiyo.
Kamanda wa vikosi vya Walinzi wa Mapinduzi, Jenerali Amir Ali Hajizadeh, amesema kombora lililofanyiwa majaribio linaweza kusafiri umbali wa km 2,000, likibeba vichwa kadhaa vya mabomu.