20.9 C
Dar es Salaam
Saturday, June 15, 2024

Contact us: [email protected]

India yatetea uamuzi wake kuhusu hadhi ya Kashmir

NEW DELHI, INDIA 

WAZIRI  Mkuu wa India, Narendra Modi ametetea uamuzi wa kuifuta hadhi maalum jimbo la Kashmir akisema hatua hiyo itamaliza miongo kadhaa ya ugaidi na mapambano ya kutaka kujitenga yanayochochewa na Pakistan. 

Katika hotuba yake ya kwanza kwa taifa kuhusiana na uamuzi wa serikali yake  kuiondolea mamlaka jimbo la Kashmir, waziri mkuu Modi ameyaelezea mabadiliko hayo kuwa ya kihistoria na kuwahakikishia wakaazi wa jimbo hilo kwamba hali ya kawaida itarejea taratibu.

Tangu usiku wa Jumapili iliyopita, serikali ya India imeweka ulinzi mkali na kuzifunga karibu njia zote za mawasiliano pamoja na kuwakamata zaidi ya watu 500 katika jimbo la Kashmir lenye wakazi wengi Waislamu.

Serikali ya Modi inayoongozwa na chama cha jamii ya walio wengi ya wahindu ilitangaza wiki hii, kuiondolea mamlaka jimbo la Kashmir uamuzi ambao utapunguza nguvu za jimbo hilo za kufanya maamuzi ya ndani na kuondoa haki ya kuwa na katiba yake.

Modi amesema uamuzi huo ambao unalenga kuliunganisha jimbo la Kashmir na sehemu nyingine za India utachochea maendeleo na kukuza nafasi mpya za ajira kupitia uwekezaji wa kampuni za umma na binafsi.

“Ndugu zangu, ninatumai kuwa chini ya muundo mpya tutakuwa kitu kimoja na kuiondoa Jammu na Kashmir katika ugaidi na madai ya kujitenga. Pepo hii ya hapa duniani, Jammu na Kashmir, itarejea kwa mara nyingine katika mafanikio makubwa na kuwa kivutio kwa ulimwengu. Wepesi wa maisha utaongezeka kwa raia wetu. Raia watapata manufaa wanayostahili bila vikwazo wala changamoto.” alisema modi wakati wa hotuba yake kwa taifa

Katika hotuba yake iliyorushwa moja kwa moja kupitia Televisheni, Modi ameilaumu Pakistan kwa kutumia muundo wa zamani wa Kashmir kama silaha ya kuchochea watu wa eneo hilo dhidi ya utawala wa India.

Chini ya utaratibu uliofutwa, ibara ya 370 ya katiba ya India ilitoa ruhusa kwa jimbo la Kashmir kuwa na katiba yake yenyewe pamoja na haki ya kufanya maamuzi kuhusu masuala yote isipokuwa ulinzi, mawasiliano na mambo ya kigeni.

Uamuzi wa India wa kufuta hadhi hiyo ya Kashmir, uliikasirisha Pakistan ambayo imesema itapunguza mahusiano yake ya kidiplomasia na serikali India, kumrejesha nyumbani balozi wa India pamoja na kusitisha biashara na usafiri muhimu wa treni kati ya nchi hizo mbili.

India na Pakistan zote zinadai umiliki kamili wa jimbo la Kashmir ingawa kila upande unadhibiti sehemu ya jimbo hilo lakini kwa miongo kadhaa sasa waasi wamekuwa wakipambana dhidi ya utawala wa India katika eneo inalolidhibiti.

Waziri mkuu wa Pakistan Imran Khan ameliambia baraza lake la usalama wa taifa kuwa serikali yake itatumia njia zote za kidiplomasia kuanika alichokiita ”ukatili wa utawala wa India na ukikukwaji mkubwa wa haki za binadamu” kwenye jimbo la Kashmir.

Wakati huo huo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa  Antonio Guterres amezitaka  India na Pakistan kujizuia dhidi ya kuchukua hatua zozote zinazoweza kuhatarisha hadhi ya jimbo la Kashmir.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amewaambia waandishi habari kuwa msimamo wa katibu mkuu Guetterres, unaongozwa na makubaliano ya mwaka 1972 kati ya India na Pakistan ambayo yanaelekeza kuwa uamuzi kuhusu hadhi ya eneo la Jammu Kashmir utafikiwa kwa njia amani chini ya mkataba wa Umoja wa Mataifa.

Guetteres pia ameelezea wasiwasi wake kuhusu ripoti za kuwepo vizuizi kadhaa kwenye jimbo la Kashmir akisema hatua hizo zinaweza kulemaza hali ya haki za binadamu katika eneo hilo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles