25 C
Dar es Salaam
Friday, November 22, 2024

Contact us: [email protected]

Ikulu yawakatisha tamaa Ukawa

Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wanaunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).
Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wanaunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).

NA SHABANI MATUTU

MKURUGENZI wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Salva Rweyemamu, amesema hata kama viongozi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) wakikutana na Rais Jakaya Kikwete, hakuna kitakachobadilika kuhusu mwenendo wa Bunge Maalumu la Katiba.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Salva alisema katu hatua hiyo haitaweza kusitisha Bunge hilo akiwataka warejee bungeni na kujenga hoja zao.

Alisema kuwa mara kwa mara Ukawa wamekuwa wakiomba kuonana na Rais Kikwete kwa nia ya kumshawishi kusitisha shughuli za Bunge la Katiba zinazoendelea mjini Dodoma.

“Wakati mchakato huu ulipokuwa ukiendelea, Ukawa walikuwa wakimbeza rais kwamba hakuwa na mamlaka ya kuvunja Bunge, lakini hivi sasa nashangaa sababu za wao kuwa wa kwanza kumpatia mamlaka hayo,” alisema Salva.

Alitoa wito kwa Ukawa kutopoteza muda wa kukutana na rais kujadili usitishwaji wa Bunge ambalo linaendelea Dodoma na badala yake wachukue uamuzi wa kurudi katika Bunge hilo kuelezea hoja zao.

Akizungumzia kuhusu tamko la Ukawa lililompa masharti Rais Kikwete ili asitishe Bunge hilo, aliwataka viongozi hao kuacha haraka ya kuwafuata wananchi na badala yake wasubiri wakati wa kupigiwa kura.

Kauli hiyo ya Ikulu ni mwendelezo wa kauli iliyotolewa juzi kwa MTANZANIA na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, kwamba hakuna mpango wa kulivunja Bunge hilo.

Sefue alisema kuwa Bunge Maalumu la Katiba lilianzishwa na linaendeshwa kwa mujibu wa sheria ambayo haina kifungu chochote kinachomruhusu rais kulisitisha.

“Hakuna mpango huo kwa hivi sasa, Bunge Maalumu la Katiba limeanzishwa na linaendeshwa kwa mujibu wa sheria na sheria hiyo haina kifungu cha rais kulisitisha,” alisema.

Kiongozi mwingine aliyepata kuzungumzia kauli hiyo juzi alikuwa Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta, aliyesema kuwa Bunge huendeshwa kwa mujibu wa sheria na wanaosema lisitishwe hawana hoja kwani kila siku wamekuwa wakitoa kauli za kubadilika.

“Bunge hapa linaendesha shughuli zake kwa mujibu wa sheria, hawa watu kila siku wana hoja mpya.

“Vitisho wanavyovitoa havinishtui kwa kuwa kazi yao ni kulishambulia Bunge Maalumu tu, wanasema gharama, hata uchaguzi una gharama zake,” alisema.

Awali akizungumza na Jumuiya ya Wafugaji waliotembelea ofisini kwake mjini Dodoma na kuwasilisha mapendekezo wanayotaka yaingizwe kwenye Katiba mpya, Sitta alisema waliotoka nje ya Bunge hilo na sasa hivi wanapiga kelele wakitaka lisitishwe, hawawatakii mema Watanzania.

“Walioko hapa wanatosha kabisa kuendelea na mchakato mpaka mwisho,” alisema Sitta.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles