23.4 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

Makubwa yaibuka Msikiti wa Mtambani

Msikiti wa Mtambani ukiwaka moto
Msikiti wa Mtambani ukiwaka moto

Hadia Khamisi na Jonas Mushi, Dar es Salaam

SIKU moja baada ya Msikiti wa Mtambani sehemu ya juu kuteketea kwa moto na kuunguza vitu vyote, uongozi umeunda kamati mbili za kufuatilia suala hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Katibu wa Msikiti wa Mtambani, Sheikh Abdallah Mohammed Ali, alizitaja kamati hizo kuwa ni ya maafa na ulinzi.

“Ajali hii ilianza kutokea wakati tunajiandaa kuswali Magharibi, ghafla tukasikia kelele za watu wakisema ‘moto… moto’ ndipo tulipotoka na kuangalia tukakuta sehemu ya juu ya msikiti inaungua huku chanzo cha ajali hii bado hatujakitambua,” alisema Sheikh Ali.

Alisema kutokana na moto huo, hasara iliyopatikana ni ya Sh. milioni 500, ambapo bado wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo.

Alisema sehemu ya juu ya msikiti huo ilikuwa inatumika kwa ajili ya wanafunzi wa Shule ya Mivumoni na ndiyo sehemu iliyoungua yote kutokana na moto huo, lakini moto huo haukuleta madhara kwa binadamu.

“Msikiti una ghorofa mbili na sehemu iliyoungua ni ghorofa ya tatu, hivyo shughuli za ibada zitaendelea kama kawaida, lakini kwa sasa tutaitisha mkutano na wazazi wa wanafunzi kwa ajili ya kulipatia ufumbuzi suala zima la elimu ukizingatia wapo wanafunzi 60 wa kidato cha nne, wanatarajiwa kufanya mtihani wa taifa mwaka huu,” alisema Sheikh Ali.

Alisema vitu vilivyoungua ni pamoja na maktaba, vitabu rejea, madawati,  kompyuta, mashine za kurudufu (photocopy), ofisi ya mkuu wa taaluma pamoja na samani zilizokuwa katika ofisi yake.

“Kwa sasa kuna wahandisi ambao tunashirikiana nao pamoja na Jeshi la Polisi kwa kutupa ushirikiano ili kuweza kujua chanzo cha ajali hii,” alisema.

Alisema uongozi unafanya jitihada za karibu na kwa haraka ili kuweza kuwapatia eneo la kujisomea wanafunzi hao, ambao kwa sasa masomo yamesitishwa hadi hapo watakapotoa agizo mara baada ya kikao cha wazazi kinachotarajiwa kukaa leo (jana).

Mbali na hatua hiyo, alilishukuru Jeshi la Polisi la Mkoa wa Kinondoni, Kikosi cha Zimamoto pamoja na wananchi wa Kinondoni kwa msaada mkubwa walioutoa hadi kufanikiwa kuuzima moto huo.

Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Mvumoni, Dadi Hemed, aliwataka wazazi pamoja na wanafunzi kuwa wavumilivu katika kipindi hiki kigumu walichonacho hadi hapo ufumbuzi utakapopatikana.

Alisema kuungua kwa sehemu ya shule hakutasababisha wanafunzi hao kutofanya vizuri katika masomo yao, kwani walijitahidi katika muhula uliopita kuhakikisha wamemaliza mada zote kwa wanafunzi wa kidato cha nne na cha pili.

“Tumeguswa sana na ajali hii na tupo katika wakati mgumu, japo wanafunzi wetu wamejianda vizuri, hususan wale wanaotarajia kufanya mtihani wa taifa, tulihakisha muhula uliopita tumemaliza mada zote na hivyo muhula huu ulikuwa kwa ajili ya marejeo.

“Tunaomba wahisani mbalimbali wajitokeze kutusaidia kupata vitabu vya marejeo kwani maktaba yetu imeteketea yote na hivyo hatuna kitabu hata kimoja,” alisema Hemed.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles