26.9 C
Dar es Salaam
Tuesday, May 21, 2024

Contact us: [email protected]

Ikulu: Ripoti ya Tokomeza, Escrow hazitatolewa

sefueNa Fredy Azzah, Dar es Salaam
KATIBU Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, amesema ripoti za uchunguzi ya Operesheni Tokomeza na suala la Akaunti ya Tegeta Escrow hazitatolewa hadharani.
“Hakuna mpango wa kuweka ripoti hadharani kwa sababu kuna mambo ya kesi zinazoendelea mahakamani, sasa ukianza kutoa hadharani unaharibu hizo kesi mahakamani,” alisema Balozi Sefue.
Ametoa kauli hiyo siku chache baada ya kutolewa ripoti ya uchunguzi dhidi ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliachim Maswi hahusiki katika kutolewa fedha za Escrow pamoja na ile ya Operesheni Tokomeza iliyowasafisha waliokuwa mawaziri wanne wa serikali ya Rais Jakaya Kikwete.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Balozi Ombeni Sefue, alisema mawaziri wanne waliopoteza nyadhifa zao kwa sababu ya Operesheni Tokomeza hawakuwa na hatia ila walilazimika kujiuzulu ikiwa ni kuwajibika katika siasa.
Alipoulizwa kuhusu kitendo cha kusema viongozi waliojiuzulu hawana makosa bila kutaja muhusika anayetakiwa kuwajibika kwa yaliyotokea, Balozi Sefue alisema: “Kuwajibika kisiasa ni kwamba wewe ndiyo kiongozi wa siasa kwenye wizara fulani, watu wa chini yako wakifanya kosa, unawajibika kisiasa.
“Lakini haina maana kwamba wewe mwenyewe una kosa la kuchukuliwa hatua nyingine ya nidhamu … kuondoka kwenye wadhifa wako ndiyo namna pekee naweza kusema,” alisema.
Alipoulizwa hatua ya baadhi ya mawaziri waliojiuzulu kutoa taarifa kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuhusu uhalifu uliokuwa ukitendeka kwenye operesheni hiyo, Balozi Sefue alisema: “hilo mimi sijui na sijaliona popote hata kwenye ripoti halipo”.
Wakati ripoti ya Operesheni Tokomeza iliposomwa bungeni, baadhi ya wabunge akiwamo Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM) alitaka Waziri Mkuu ajiuzulu kutokana na mateso waliyokuwa wakifanyiwa wananchi bila kuwa na hatia.
“Wakati operesheni hii inafanyika, hata siku moja hukuwahi kufika kwenye maeneo inapofanyika, ulikuwa wapi Waziri Mkuu wangu, ulikuwa wapi? Watu wanabakwa, wanakufa, ulikuwa wapi Mheshimiwa Waziri Mkuu? Kwa utaratibu wa nchi yetu tumekupa kila aina ya usafiri, kuanzia ndege, helikopta, magari, ving’ora kila wakati vinalia, ulikuwa wapi Mheshimiwa Waziri Mkuu wakati mambo haya yanatokea?” alisema Lugola.
Katika mapendekezo yake, pamoja na mambo mengine, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, ilisema kuna baadhi wanasiasa waliingilia mchakato wa Operesheni Tokomeza.
Mwenyekiti wake, James Lembeli, aliliambia Bunge kwamba walibaini kuwa baadhi ya viongozi wa siasa na Serikali waliingilia utekelezaji wa operesheni hiyo kwa manufaa yao binafsi.
“Kwa mfano, agizo la kuwataka wahusika wa Operesheni Tokomeza kutowagusa viongozi wa siasa wa ngazi zote, kauli ambayo ilitafsiriwa kuathiri utekelezaji wa Operesheni Tokomeza kwa kubagua Watanzania katika makundi ya viongozi na wananchi wa kawaida.
“Hivyo basi, Bunge linaazimia kwamba, Serikali ihakikishe kuna uwajibikaji wa pamoja inapoamua kutekeleza jambo la kitaifa kama Operesheni Tokomeza,” alisema.
Baada ya ripoti hiyo kusomwa bungeni, Serikali iliunda tume ya chini ya Jaji mstaafu, Hamisi Msumi, ikiwa na hadidu za rejea sita.
Adidu ya rejea ya kwanza ilikuwa kuchunguza namna Operesheni Tokomeza ilivyotekelezwa, kuchunguza iwapo maofisa waliotekeleza Operesheni Tomokeza walizingatia sheria, kanuni, taratibu na hadidu za rejea walizopewa.
Nyingine ilikuwa kuchunguza iwapo maofisa waliotekeleza Operesheni Tokomeza walivunja sheria, kanuni, taratibu na hadidu rejea walizopewa, kuchunguza iwapo kuna watu waliokiuka sheria yoyote wakati wa utekelezaji wa Operesheni Tokomeza na iwapo hatua zilizochukuliwa na maofisa wa Operesheni Tokomeza dhidi ya wakosaji hao na mali zao zilikuwa sahihi.
Tume hiyo pia ilitakiwa kupendekeza hatua zinazostahili kuchukuliwa dhidi ya maofisa wa Operesheni Tokomeza waliokiuka sheria, kanuni, taratibu na hadidu za rejea za Operesheni Tokomeza.
Ilikuwa pia na jukumu la kupendekeza mambo yanayopaswa kuzingatiwa wakati wa kupanga na kutekeleza Operesheni nyingine kama hiyo kuepuka malalamiko mengine yasitokee.
Akikabidhi ripoti yake ya Rais Kikwete, Jaji Msumi alisema kuwa katika kutelekeza majukumu yake, tume ilitembelea mikoa 20 na wilaya 38 na kupokea malalamiko mbalimbali kutoka kwa viongozi wa Serikali ikiwa ni pamoja na mawaziri wanne waliojiuzulu kutokana na suala hilo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles