24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Waliofungiwa CCM waendelea kubanwa

NapeNA FREDY AZZAH, Dar es Salaam
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) kimetangaza ratiba ya vikao vya chama hicho kuanza mwezi huu ikionyesha mchakato wa kuchukua fomu za kuwania kugombea urais utafanyika wakati makada wake sita waliofungiwa wakiendelea kuwa kifungoni.
Akizungumza na MTANZANIA kwa simu jana, Katibu wa Halmashauri Kuu, Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, alisema baada ya ratiba ya uchaguzi kutangazwa ndani ya chama hicho, wana CCM watatakiwa kuendelea kuheshimu taratibu na sheria za chama chao.
Februari 18, mwaka jana CCM iliwawapa adhabu ya kifungo cha mwaka mmoja makada wake sita wa chama hicho ambao walidaiwa kuanza kampeni mapema za urais nao ni Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushiriano wa Kimataifa Bernard Membe, Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye, Mbunge wa Sengerema William Ngeleja, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira pamoja na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia January Makamba.
Katika mazungumzo yake na MTANZANIA, mahojiano yalikuwa kama ifuatavyo:
Swali: Baada ya kutolewa ratiba utaratibu utakuwaje?
Jibu: Wana CCM watafuata ratiba itakayotolewa kwa sababu haiwapi watu uhuru wa kufanya wanavyotaka na hii ni sawa na mpira. Kwa mfano, leo TFF (Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania) likisema ligi kuu itaanza Juni, hamuwezi mkaanza Mei.
“Sisi tutakachotoa ni ratiba itakayosema tarehe fulani mpaka tarehe fulani ni siku ya kuchukua fomu za udiwani na tarehe fulani mpaka tarehe fulani ni siku za kuchukua fomu za ubunge.
“Ratiba itaonyesha tarehe fulani ni siku za kuchukua fomu za wawakilishi, tarehe fulani ni Rais wa Zanzibar na tarehe fulani ni kuchukua fomu kwa ajili ya mgombea nafasi ya urais wa Jamuhuri ya Muungano.
“Mkishachukua fomu, mnazirudisha, mkizirudisha, mchakato wa kuchuja majina utaendelea mpaka tutakapompata mgombea wetu.
“Hiyo ndiyo ratiba yetu, hiyo ratiba haifuti mambo mengine, kama yapo yaliyokuwa yakiendelea, likiwapo la maadili, mambo ya adhabu, mambo ya nini, taratibu zake ni tofauti.
“Sisi tunashughulika na ratiba, kama hayo mambo ya adhabu yatashughulikiwa lini, basi hiyo ni ajenda nyingine.
Swali: Mnafikia hatua ya kutoa ratiba ya kuanza mchakato wa kugombea wakati makada wenu sita mliowafungia hamjawafungulia, nini hatima yao?
Jibu: Hatima yao kama hawatafunguliwa, wataendelea kubaki kifungoni, wale walio huru wataendelea kushiriki mchakato. Kama kifungo kitaendelea maana yake ni kwamba hawatashiriki mchakato, lakini wakifunguliwa, wataruhusiwa kushiriki. Hii hesabu ni rahisi sana, mimi sijui kwa nini hamuielewi.
Swali: Adhabu yao ilikuwa miezi 12 na ilishakwisha kwa nini wanaendelea kubaki kifungoni?
Jibu: Adhabu haijaisha, kanuni iko wazi, inasema watatumikia adhabu kwa kipindi kisichopungua miezi 12 siyo kisichozidi miezi 12 ni kisichopungua miezi 12.
“Kwa hiyo, inaweza kuwa miezi 12, 13, 14, 15, 20, 25, 30, nenda kasome vizuri kanuni na imeeleza vizuri, kipindi kisichopungua miezi 12.
“Umeuliza kama ratiba ikitoka wanakuwa huru, nasema hapana. Kama wasipofunguliwa maana yake wanaendelea kubaki kifungoni, wakibaki kifungoni maana yake hawaruhusiwi kushirki mchakato, mfungwa hapigi kura, hiyo ndiyo CCM ni zaidi ya ujuavyo.
Jana, Nape alikaririwa na vyombo vya habari akisema CCM itaanza vikao vyake Mei 18 hadi 22 mwaka huu mjini Dodoma.
Alisema vikao hivyo vitajadili ratiba ya mchakato wa uteuzi wa wagombea udiwani, uwakilishi, ubunge, urais wa Zanzibar na urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kazi nyingine itakayofanyika ni kupitia rasimu ya kwanza ya maboresho ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020 na kujadili mapendekezo ya uboreshaji wa mchakato wa kura za maoni ndani ya chama hicho.
Pia vikao hivyo vitajadili jinsi CCM itakavyofanikisha ushiriki na ushindi katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
Kwa mujibu wa ratiba ya vikao hivyo vitaanza rasmi Mei 18 hadi 19, kitafanyika kikao cha Sekretarieti ya CCM chini ya Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana
Mei 20, kikao cha Kamati Kuu ya CCM chini ya Mwenyekiti wa Rais Jakaya Kikwete na Mei 21 mpaka 22 kutakuwa na Kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC).
Vikao hivyo vitafanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Makao Makuu Dodoma maarufu kama ‘Whitehouse’.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles