Na VICTORIA GODFREY-DAR ES SALAAM
UONGOZI wa Klabu ya Ihefu ya Mbeya, umeahidi kuishangaza Simba kwa kupata matokeo chanya licha ya uzoefu mdogo wa kikosi chao.
Ihefu itakuwa mwenyeji wa Simba, katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2020-12, utakaopigwa Jumapili hii Uwanja wa Sokoine, Mbeya.
Timu hiyo ni miongoni mwa timu tatu zilizofuzu Ligi Kuu msimu ujao, zikitokea Ligi Daraja la Kwanza. Nyingine ni Dodoma Jiji na Gwambina ya Misungwi mkoani Mwanza.
Akizungumza na MTANZANIA jana kutoka Mbeya, Ofisa Habari wa klabu hiyo, Peter Andrew, alisema wamefanya usajili makini wa wachezaji wenye uwezo wa kukabiliana na changamoto ligi, licha ya kwamba wengi wao hawana uzoefu wa kutosha.
“Tumejipanga vizuri, ndio maana tumejaribu kuchanganya nguvu za wachezaji waliobaki katika timu na hata waliocheza Ligi Kuu lakini wana uwezo wa kutumika kwa muda mrefu, hivyo kupata matokeo ya alama tatu tukiwa nyumbani hilo ndilo tunalolitegemea.
“Tumepanda Ligi Kuu tukiwa tunajua ugumu wake lakini tuwahakikshie mashabiki wetu, Ihefu ipo kwa ajili ya kuleta changamoto mpya katika ligi pamoja na kuondoa ufalme wa baadhi ya timu katika mpira wa Tanzania,”alisema.
Andrew alitaja orodha kamili ya wachezaji wanaounda kikosi chao cha msimu ujao kuwa ni makipa Andrew Kayuni, Isihaka Josep na Alex Venance, mabeki Mando Mkumbwa , Omary Kindamba, Eliah Salingo, Emanuel Kichiba, Michael Masinda, Geoffrey Rafael, Allen Malele na Wema Sadoki.
Viungo ni Sudi Mlindwa, Samwel Onditi, John Mbise, Willy Mgaya, Daniel Jeremiah, Abdi Kassimu, Ennock Jiah, wakati washambuliaji ni Joseph Kinyozi, Omary Mponda, Malulu Mponda, Cyprian Kipenye, Issa Ally, Geoffrey Kitenga, Paul Luyungu na Jordan John.