29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Si kila taka inafaa kutupwa ovyo, nyingine hatarishi – NEMC

Na AVELINE KITOMARY

UTUNZAJI wa mazingira ni sehemu muhimu zaidi katika kuhakikisha afya ya watu pamoja na viumbe hai vinakuwa salama.

Afya na mazingira ni vitu vinavyoenda sambamba kwani uchafu katika mazingira unaweza kusababisha magonjwa mbalimbali hasa ya mlipuko.

Utunzaji wa mazingira unazingatia zaidi suala la namna ya uhifadhi wa taka za kawaida na zile hatarishi.

Endapo taka hasa zile hatarishi hazitadhibitiwa na kuzagaa hovyo, huweza kuleta athari zaidi katika mazingira na afya.

Jiji la Dar es Salaam ndilo linaloongoza kwa kuwa na uzalishaji wa taka hapa nchini ziwe zile za kawaida na taka hatarishi.

Kiwango kinachozalishwa ni tani 4,600 kwa siku, ambapo asilimia 40 hadi 58 ndio huzolewa, hii ni kwa mujibu wa Mganga Mkuu wa mkoa huo, Dk. Rashid  Mfaume.

Hata hivyo, Baraza la Taifa la Uhifadhi wa Mazingira Tanzania (NEMC), limesema kuwa hali ya uzalishaji taka inaweza kuongezeka katika jiji hilo hadi kufikia tani 12,000 kwa  mwaka 2025.

Uongezekaji wa  kiwango cha taka hutokana na ongezeko la idadi ya watu huku ongezeko la viwanda ikichukua nafasi pia.

Mkurugenzi wa NEMC, Mhandisi Dk. Samweli Gwamaka, anasema kutokana na hali hiyo, wanalazimika kuweka utaratibu  ambao ni endelevu ili kuhakikisha mazingira ya Tanzania yanazidi kuhifadhiwa na  kuboreshwa.

“Ni kweli kuwa tunahitaji kuwa na mfumo wa kuhakikisha mazingira yanatunzwa na wadau tunashirikiana kuhakikisha mazingira yetu yanaboreshwa, changamoto kama hizo ndizo ambazo tunazijadili kila tunapokutana wadau wa mazingira,” anasema Dk. Gwamaka.

Kwa mujibu wa Dk. Gwamaka, hivi sasa changamoto iliyopo ni jinsi ya kutenganisha taka kutokana na kuwapo kwa taka ambazo ni hatarishi na  zinazoweza kurejeleshwa na kuwa bidhaa tena.

“Ukizungumzia suala la taka kuna kukusanya, kusafirisha na kutupa kwenye dampo, utakuta wanaozichambua, wengine wanaenda kuzirejelesha lakini wengine wanazichangaya bila kuelewa kama kuna taka za kutupa na zisizofaa kutupwa. 

“Sheria ya mazingira ya mwaka 2014 inazitaka halmashauri zote, jiji na manispaa ziweke mfumo wa kutenga taka tangu pale zinapozalishwa na zinampa mamlaka Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais wajibu wa kuweka mwongozo ambao utatekelezwa na taasisi, masoko, majumbani kwamba ni kwa jinsi gani wanatakiwa kutenga hizo taka,”anabainisha Dk. Gwamaka.

Anasema ni lazima jamii ielewe kuwa taka sio uchafu, bali ni fursa ya kujiingizia kipato, hivyo ni muhimu kutenga taka katika sehemu zote. 

“Ukizichambua na kuzirejeleza taka  zinaleta ajira, pia zinapunguza uletaji wa malighafi toka nje au malighafi mpya ikatumiwa, kwa hiyo utakuta zile taka ni fursa ya kuendeleza hata kwenye uchumi wa viwanda na kupunguza uletaji wa malighafi kutoka nje. 

 “Sasa hivi tunaona kipindi cha Covid-19 kumekuwa na ongezeko la barakoa, chupa za plastiki, kuna taka hatarishi, kwa jinsi watu wanavyoongezeka ndivyo na changamoto zinaongezeka hivyo wakati mwingine mabadiliko ya sera yanahitajika pia,” anasema Dk. Gwamaka. 

TAKA HATARISHI MAJUMBANI Taka hatarishi ni zile ambazo zikitupwa mtaani zinaweza kuleta madhara kwa mazingira na afya ya binadamu mfano taka za hospitali, maabara na kemikali za viwandani na migodini.

Taka hizo ni kama vile sindano, chupa za kuhifadhia dawa, mirija inayotumika kuongezea damu na  maji kwa wagonjwa, vipodizi vyenye viambata vya sumu, dawa zilizokwisha muda wa matumizi, vifaa vya maabara vilivyovunjika, maji maji yenye kemikali toka viwandani na migodini.

Ni hatari zaidi kutupa taka hizo na hatari yake sio tu kwa mazingira bali hata afya ya binadamu ambao wanazunguka mazingira hayo.

Mkurugenzi wa Idara ya Mazingira na taka hatarishi kutoka taasisi isiyo ya kiserikali ya Tindwa Medical  and Health Services (TMHS), Maimuna Salum, anasema zipo taka hatarishi majumbani ambapo wahusika hawajui namna ya utupwaji wake  hivyo kufanya kuchanganya na taka zingine kitu ambacho ni hatari.

“Kwa bahati mbaya watu wengi hawana uelewa juu ya namna nzuri ya kukusanya na kuharibu taka ambazo ni hatirishi kwa afya zao na kujikuta wakizitupa kiholela au kuzichanganya na taka nyingi ambazo hazina madhara makubwa kwa binadamu,” anabainisha.

Anasema taka hatarishi zinatakiwa kuharibiwa kwa njia maalum pindi zinapoharibika kutokana na sumu na kemikali zilizopo katika taka hizo.

“Mfano, Kariakoo kuna maduka makubwa ya dawa hawawezi kuuza zote huwa inafika wakati zinaisha muda kwahiyo sisi tunaenda kuzichukua na kuziangamiza.

“Na Bohari ya dawa  (MSD) sio kila dawa na vifaa vyote hutumika, vinatumika na kuisha kuna baadhi ya  dawa hutumika kutibu magonjwa yanayotokea kwa msimu, chanjo ambazo zinategemea msimu wa magonjwa kwa matumizi endapo mlipuko wa magonjwa hayo haujatokea kwa kipindi kirefu dawa hizo huharibika maana dawa  kwa kawaida zina kipindi maalumu cha kuendelea kuwa salama basi sisi tunaziharibu.

“Kwenye uchimbaji wa mafuta na gesi wafanyakazi wanapofanya upasuaji wa miamba na usafishaji wa madini kemikali hutumika endapo muda wa matumizi wa kemikali zile ukifika nazo zikaendelea kubaki huharibika basi  sisi ndio tunaopaswa kuhusika na namna sahihi ya kuziharibu,” anasema.

UELEWA WA WANANCHI MTANZANIA ilifanya mahojiano na baadhi ya  Wakazi wa jiji la Dar es Salaam kuhusu uelewa wao juu ya taka hatarishi zilizotumika majumbani .

Wengi wao walisema hawana uelewa wowote kwani muda wa matumizi unapoisha wao hutupa  hovyo bila kujali usalama wao.

Mmoja wa wakazi  hao walihojiwa, Anael Thomas anasema kuwa ni kitu kipya kabisa masikioni mwake kusikia kuwa taka hizo zinasehemu maalum ya kuharibu.

“Yaani ndugu mwandishi kwa mara ya kwanza ndio nasikia hilo kutoka kwako ,mimi huwa ndani nawekaga dawa kwaajili ya familia yangu na zikiharibika naenda kutupa dampo na ninafanya hivi kutokana na kutokujua madhara yake.

“Inafaa tukalielewa zaidi hili jambo maana ni muhimu kwa afya zetu wenyewe kwasababu huko dampo kuna watu wengine wanapita kuokota hata hivyo nikisema nichome sijajua madhara ya moshi wa taka hizi,”anasema Anael.

Mkazi mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Husna, anasema kuwa ni vyema serikali ikatoa elimu kuhusu uhifadhi wa taka hizo katika maeneo ya majumbani.

“Kuwepo utaratibu wa kukusanya na kuja kuchukuliwa ili kupelekwa sehemu husika za kuharibiwa na sio mara moja nakutana na dawa au kipodozi hata sindano baada ya matumizi imetupwa tu tunaomba hili liangaliwe,” anasisitiza Husna.

 Naye Maimuna anaishauri serikali kutoa elimu kwa jamii ili waweze kuelewa jinsi ya kutenga taka hatarishi na kupeleka sehemu husika za kuharibu taka hizo ili kuepuka madhara katika mazingira  na afya ya viumbe hai.

 “Watu wengi wanakaa na dawa na sindano majumbani lakini wakimaliza matumizi yake huwa wanazitupa hovyo bila kujua madhara ya hizo taka na hii ni kutokana na kutokuwa na uelewa wowote.

“Hivyo, ni vyema Serikali kutengeneza uelewa kwa jamii mfano watu wanatumia dawa na zikishabaki wanapeleka wapi?” anahoji.
“ Utakuta wengine wanatupa tu hovyo ndio maana serikali inatakiwa kutoa elimu kwa jamii  kuelewa dhana nzima ya taka hatarishi ili wasichanganye na taka za dampo,” anaeleza.

CHANGAMOTO UZOAJI TAKA

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dk. Mfaume anakiri kuwapo kwa changamoto ya uzoji wa taka katika jiji hilo.

Anasema wanaendelea  kufanyia kazi changamoto ya  uzoaji taka angala kufikia asilimia 80 hadi 90.

“Upungufu  wa vitendea kazi za kusafirisha taka unaweza kuleta madhara   kwenye usafirishaji taka, tunaomba halmashauri kuongeza idadi  ya wakandarasi.

“Suluhu nyingine ni kushirikisha wadau mbalimbali ambao tukisaidiana tutaongeza uwezo wa mkoa kuhakikisha taka zinazozalishwa angalau asilimia 80 hadi 90 zinasafirishwa kwa wakati,” anaeleza.

Dk. Mfaume anasema licha ya kuwapo kwa changamoto za magari ya uzoaji taka, pia miundombinu ya jiji ni changamoto kwa zoezi hilo.

Anasema kuwa kuna maeneo ambayo magari ya kuzoa taka yanashindwa kufika kutokana na kutokuwa na barabara hivyo kufanya uzoaji taka kuwa mgumu.

“ Lakini pia kunachangamoto kwa wazoaji ukienda kuzungumza nao wanasema  miundombinu ni tatizo, kuna maeneo hapa Dar es Salaam hayawezi kufikika hata kwa mikokoteni,” anabainisha.

Anataja changamoto nyingine kuwa ni utupaji wa taka katika maeneo ya vyanzo vya maji.

 “Tunaendelea kutoa rai kwa jamii kuwa wasitupe taka katika sehemu za mito au vijito kwani ukienda katika nchi zingine maeneo kama mto msimbazi na maeneo mengine yanakuwa ya kitalii unakuta  kuna vijito vinatiririsha maji vizuri miti imepandwa vizuri, pia inakuwa mazingira rafiki kwa viumbe vingine kama ndege.

Anaongeza: “Serikali imeamua hii mito inajengwa na ujenzi wake unaenda sambamba na utoaji elimu kwahiyo silaha kubwa ni elimu na kuimarisha sheria ndogo kuhakikisha kuwa wanaotupa taka wanatiwa hatiani.

Akiulizwa kuhusuni namna gani wanaweza kutatua changamoto za miundombinu ya jiji la Dar es Salaam anasema:

 “Tunashirikisha mamlaka ya ngazi ya mitaa na kata na katika usombaji wa taka watendaji wa mitaa wanashiriki kwa dhati kusimamia, kama ni kwenye kaya basi kuanzia hatua za uzalishaji na kuhakikisha zinapelekwa na kukusanywa katika sehemu zilizoainishwa  ili baadae zitolewe kwa urahisi na kupelekwa dampo.

KULINDA MAZINGIRA NA AFYA

Dk. Mfaume  anatoa wito kwa wananchi kuthamini masuala ya usafi kwakuwa ndio kinga  kwa  magonjwa mengi yanayotokana  na uchafu, kama magonjwa ya matumbo, ngozi, macho, utapiamlo na mengineyo.

“Niendelee kuwahimiza wananchi wa Dar es Salaam kutumia maeneo ya taka na si kutupa hovyo. Tunaendelea kutoa elimu ya utunzaji wa mazingira kwa sababu tunajua  kuwa tukiwa wasafi tunajikinga na magonjwa mengi, pia mazingira yanakuwa  mazuri,” anashauri Dk. Mfaume.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles