22.1 C
Dar es Salaam
Sunday, June 23, 2024

Contact us: [email protected]

IGP apiga marufuku maandamano

Abdulrahman Kaniki(D_IGP)Na Asifiwe George, Dar es Salaam

KAIMU Mkuu wa Polisi, Abdulrahman Kaniki, amepiga marufuku maandamano nchi nzima hadi Uchaguzi Mkuu upite, akisema sababu za kiusalama zimewasukuma kufanya hivyo.

Hatua hiyo imekuja zikiwa zimepita siku nne tangu vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kufanya maandamano makubwa ya kumsindikiza mgombea wao wa urais, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, kuchukua fomu ya utezi Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Wakati Kaniki akisema hayo jana saa 6:00 mchana, ilipofika saa 8:00 mchana, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,  Suleiman Kova, alipongeza maandamano yaliyofanywa na Ukawa, akisema kama wataendelea hivyo, Uchaguzi Mkuu utafanyika kwa amani.

Kauli hiyo ya Kova, inafanana pia na ile ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe, ambaye juzi alinukuliwa na vyombo vya habari akiwapongeza Ukawa kwa kuandamana kwa amani.
Kaniki

Jana Kaniki alisema maandamano yaliyofanywa yakihusisha watembea kwa miguu, magari, pikipiki, na baiskeli yamekuwa yakisababisha usumbufu usio wa lazima, na malalamiko kwa wananchi walioshindwa kufika kwa wakati katika shughuli nyingine za kiuchumi na kijamii.
“Katika kipindi hiki tumeshuhudia baadhi ya wagombea wakisindikizwa na wafuasi wao kuchukua fomu NEC huku kukiwa na ukiukwaji mkubwa wa sheria za usalama barabarani katika misafara hiyo iliyobeba watu wengi,” alisema.
Naibu Kamishna huyo alisema kwa sasa wataandaa utaratibu wa kuwakutanisha wadau wote wa siasa ikiwamo viongozi ili kuona namna bora ya kuhakikisha mchakato huo unafanyika katika hali ya amani na utulivu.
Alisema pamoja na hatua hiyo ya kukutana na wanasiasa, lakini jeshi hilo halitasita kumchukulia hatua mgombea, chama au mfuasi yeyote atakayekaidi agizo hilo.

Alipoulizwa kuhusu kusitisha maandamano wakati Waziri wa Mambo ya Ndani, Chikawe, aliyasifia ya Ukawa kwamba yalikuwa ya amani, alisema hawezi kuliongelea hilo na lengo lake ni kuhakikisha amani inakuwapo na wananchi wanafanya shughuli zao bila kubughudhiwa.

Kwa upande wa Kaimu IGP Kaniki alipoulizwa kuhusu baadhi ya askari kuambiwa waandike namba za vitambulisho vya kupigia kura pamoja na kuorodhesha  majina yao, alisema kuwa taarifa hizo  anazisikia, lakini hazijatolewa rasmi hivyo suala hilo wanalifanyia uchunguzi.

“Taarifa hizo tunazisikia juu juu lakini hakuna taarifa kamili ambayo tumeletewa hivyo tunafanyia uchunguzi ili kuweza kubaini ukweli halisi,” alisema Kaniki.

 

KOVA ASIFIA
Akizungumza na waandishi wa habari, Kova alisema pamoja na uwapo wa makundi makubwa ya wafuasi wa vyama ambavyo wagombewa wao walichukua fomu vikiwamo CCM na Chadema, hali ilikuwa shwari na hakukuwa na tukio lolote la kihalifu lililojitokeza.
Pia alisema kufuatia maandamano hayo hadi sasa hakuna tukio lolote la uvunjifu wa amani lililojitokeza wakati wa kuchukua fomu za wagombea urais, udiwani wala ubunge.
Kamishna Kova alisema hali ilikuwa shwari kutokana na kuwapo na mawasilino ya karibu kati ya jeshi hilo na hali ya ulinzi na usalama katika maeneo yote yaliyofanyika maandamano hayo.
“Pamoja na makundi hayo, lakini hali ilikuwa shwari kabisa na hakuna tokio lolote la uhalifu lililojitokeza kama ilivyoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari na katika mitandao ya kijamii,” alisema.

 

KAULI YA CHIKAWE

Siku moja baada ya maandamano ya Ukawa, Waziri  Chikawe alinukuliwa na vyombo vya habari akisema alifurahishwa nayo.

Alisema alishuhudia umati mkubwa ukiimba na kucheza   katika hali ya amani na kusema kuwa hilo ni jambo zuri linalopasa kuendelea wakati wote.

Chikawe alisema  anatajaria kuwa hali hiyo itaendelea hata mikoani ambako Lowassa ataenda.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles