27.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Polisi wamzuia Lowassa kuzika

MMGL0471Na Waandishi Wetu

MGOMBEA urais wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, amepata kashikashi baada ya polisi kumzuia kumzika mwasisi wa Chama cha TANU na CCM, Peter Kisumo, kwa madai kuwa wamepata maagizo kutoka juu.

Msafara wa Lowassa ulioanzia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), ulikutana na kizuizi cha polisi katika Kijiji cha Maroro, kilomita moja kutoka Mwanga kuelekea Ugweno, ambako Kisumo alizikwa jana.
Lowassa akiongozana na viongozi mbalimbali, akiwamo Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, Mwenyekiti wa Chadema Kilimanjaro, Philemon Ndesamburo na Mbunge wa Vunjo, Augustine Mrema, walikuwa na msafara wa magari na pikipiki zaidi ya 100.

Licha ya kwamba msafara wa kiongozi huyo ulitoka KIA ukiwa na magari machache, idadi ya magari na pikipiki iliongezeka kadiri safari ilipokuwa ikiendelea kutokana na baadhi kujiunga kila alipokuwa akipita.

 

KIZUIZI

Akizungumza na waandishi wa habari waliokuwapo kwenye msafara huo, Mbatia alisema kuwa alizungumza na Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Ernest Mangu na akawaruhusu kuendelea na safari, lakini Mkuu wa Polisi Mwanga alikataa kutii agizo hilo.
“Nimeongea na IGP akiwa Kibondo, tukakubaliana na kutoa maelekezo kwa RPC, lakini tuliporuhusiwa na kuanza kuondoka, ikaja amri kutoka kwa OC CID akiwa huko juu msibani, ya kwamba hakuna kuruhusu msafara huo, kama kupanda ni gari moja tu la Lowassa na langu,” Alisema Mbatia na kuongeza.

“Lowassa ni Waziri Mkuu mstaafu, huwezi kusema eti iende gari moja tu, na pia siye viongozi wengine wanatunyima haki yetu.

“CCM sasa wameamua kuipasua nchi, Serikali ya CCM inatupeleka kwenye hali ya kutozikana, wametuzuia kwenda kumzika mzee wetu Kisumo, kisa woga tu.”
Wakati yote hayo yakiendelea, Lowassa na  Ndesamburo, walikuwa kwenye magari.

Lakini hata hivyo, baada ya mazungumzo ya muda mfupi, hatimaye majira ya saa 6:53 mchana, msafara huo uliofika eneo hilo saa 6:42, uliruhusiwa kuendelea na safari wakitakiwa kuondoa bendera za Chadema kwenye magari na pikipiki.

WANANCHI WAONDOKA MSIBANI

Mara baada ya kuzagaa kwa taarifa za kuwa Lowassa  amezuiwa kuhudhuria mazishi hayo, baadhi ya wananchi waliondoka eneo la msiba.

Wananchi hao walioonekana kuwa na shauku ya kumwona mgombea huyo urais wa Ukawa, walisikika wakilalamika kuzuiwa kwake, huku wengine wakilalamika kuibwa na kunyofolewa kwa bendera zao za Chadema katika vyombo vya usafiri.
Mbali na hilo pia baadhi ya wanachama wa CCM, walionekana wakiwa wamezaga sehemu mbalimbali msibani hapo, wakiwa na sare za chama hicho na bendera zikipepea katika miti iliyokuwa eneo hilo.

 

UWANJA WA NDEGE

Wananchi wa mikoa ya Arusha na Kilimanjaro, walianza kufika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro saa 1:00 asubuhi kumlaki kiongozi huyo.

Lowassa aliwasili uwanjani hapo saa 2:00 ambapo aliwasalimia mamia ya wananchi waliokuwapo kisha msafara wake ukaondoka.

Baadae msafara huo uliondoka uwanjani hapo kuelekea Moshi ambapo MTANZANIA ilishuhudia baadhi ya wananchi wakitoka eneo hilo kwa miguu hadi mjini humo, ikiwa ni umbali wa takribani kilomita 46.
Baada ya kutua mkoani Kilimanjaro, msafara wa Lowassa ukiongozwa na pikipiki nyingi zikiwa na bendera za Chadema, ulienda moja kwa moja
kwenye Hoteli ya Kiss, iliyoko Kiboriloni, mjini Moshi kwa mapumziko mafupi kabla ya kuelekea Usangi.
Akiwa hotelini hapo, maelfu ya wananchi walivamia wakitaka kumwona Lowassa.
Wananchi hao walizuiwa na walinzi kuingia hotelini humo, kitendo kilicholazimisha Polisi wa Kikosi cha Kuzuia Ghasia (FFU), kuingilia kati kutuliza vurugu, lakini hata hivyo waligoma kuondoka.

Baada ya polisi kushindwa kuzuia hali hiyo, Lowassa alitoka na kuzungumza na wananchi hao huku akiwataka kutofanya fujo yoyote.

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha, Amani Golugwa, alisema wameandaa mapokezi  makubwa ya kuwapokea na kuwatambulisha Lowassa na mgombea mweza, Juma Hadi Duni, ambao watafika  Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro kesho saa 3:00 asubuhi.
Golugwa ambaye pia ni Katibu  wa Chadema Kanda ya Kaskazini, alisema baada ya viongozi hao kuwasili uwanjani hapo, msafara wao utaelekea viwanja vya Tindigani vilivyopo eneo la Kimandolu ambako kutafanyika mkutano mkubwa wa hadhara wa kuwatambulisha.
“Kesho Jumamosi tutakuwa na mapokezi makubwa ya kihistoria ya kumtambulisha mgombea urais wa Ukawa kupitia chama chetu, ambapo watawasili uwanja wa ndege wa KIA na baada ya hapo kutakuwa na msafara kuanzia uwanjani hapo hadi katika viwanja ya Tindigani, eneo la Kimandolu,” alisema Golugwa.
Alisema kuwa mbali na kumtambulisha mgombea huyo, pia atapata fursa ya kutafuta wadhamini ambapo kwenye Kanda ya Kaskazini majimbo mawili  ambayo ni Arusha Mjini na Moshi Mjini yatatoa wadhamini 300 kila moja.
Alisema baada ya kumaliza kuzungumza na wananchi, Lowassa na msafara wake wataelekea wilayani Monduli ambako pia atakuwa na mkutano wa hadhara.
Alisema kuwa mgombea huyo ataongozana na viongozi wengine akiwemo Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, manaibu katibu wakuu John Mnyika na Salum Mwalimu Zanzibar na wenyeviti wenza wa Ukawa kutoka NLD, NCCR Mageuzi pamoja na viongozi wakuu wa CUF.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles