24.8 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

IEBC KUSIMAMIA SHERIA KUTANGAZA MATOKEO

 

NAIROBI, KENYA

TUME ya Taifa ya Uchaguzi nchini Kenya imesema matokeo itakayoyatangaza yatakuwa ni kwa mujibu wa sheria na si kwa maelekezo ya mtu au kundi fulani la wanasiasa.

Kauli ya IEBC imekuja ikiwa ni saa chache tu zimepita toka muungano wa upinzani nchini Kenya, NASA, utangaze matokeo yake iliyosema yametokana na uhakiki walioufanya kupitia kwenye fomu zilizowekwa kwa kazi data ya IEBC, inayotumiwa kujumuisha matokeo.

Mwenyekiti wa IEBC, Wafula Chebukati, amekiri kupokea barua ya muungano wa NASA ambapo amesema tayari wameshawarudishia majibu ambayo nao wamesisitiza kuwa matokeo waliyo nayo siyo rasmi.

IEBC inasisitiza kuwa matokeo yatakayotangazwa hayatatokana na karatasi peke yake, lakini yatatokana na idadi ya wapiga kura waliojitokeza na kupiga kura kuchagua kiongozi wanayemtaka.

Chebukati amewataka wanasiasa kujiepusha na kufanya kazi za tume yake ambayo ndio yenye mamlaka ya mwisho kumtangaza mshindi.

Tume imejibu barua hii na matokeo sahihi na ya kisheria yatatangazwa baada ya tume kupokea fomu zote za matokeo namba 34 B, kwa mantiki hiyo, tume itatangaza matokeo ya urais kama inavyoelekezwa na ibara ya 138-3C na ile ya 138-10 ya katiba.

Awali, mmoja wa vinara wa muungano wa NASA, Musalia Mudavadi, wakati akizungumza na wanahabari jijini Nairobi, alieleza kuwa muungano wao umefanya uhakiki wa fomu zilizoko kwenye kazi data ya IEBC na kujiridhisha kuwa mgombea wao, Raila Odinga ndiye mshindi.

Mudavadi alikwenda mbali zaidi na hata kuitaka tume ya uchaguzi kutotangaza matokeo ambayo yatakuwa kinyume na yale ambayo wamethibitisha kupitia kwenye mtandao wao.

Mpaka sasa ukweli haujajulikana kuhusu nani ameibuka mshindi kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Raila Odinga, ambapo kwa mujibu wa tume ya uchaguzi, IEBC, matokeo rasmi huenda yakatangazwa leo mchana baada ya kukamilisha uhakiki wa fomu namba 34 A na B kutoka kwa maofisa wa uchaguzi.

Shughuli nyingi zimeendelea kusimama jijini Nairobi na kwenye maeneo mengine ya nchi, ambapo wafanyakazi wachache wa umma walifika ofisini huku maelfu wakishindwa kutokana na hofu ya kutokea vurugu.

Waangalizi wa kimataifa wa uchaguzi pia walitoa taarifa zao za awali, ambapo wengi walieleza kuridhishwa na namna tume ya uchaguzi IEBC ilivyoandaa uchaguzi ambao wamesema kwa kiwango kikubwa ulikuwa huru na haki.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles