27.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

IDADI YA VYETI FEKI INATISHA


Rais Dk. John Magufuli akikagua baadhi ya makabati ya nguo baada ya kuzindua majengo mapya ya mabweni ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) eneo la Mlimani jana. Kulia ni Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa Rwekaza Mukandala na katikati ni Mke wa Rais, Janeth Magufuli

 

Na EVANS MAGEGE,

RAIS Dk. John Magufuli amesema anasubiri ripoti ya wafanyakazi wa Serikali ambao wamebainika kuwa na vyeti feki.

Kauli hiyo aliitoa jana, jijini Dar es Salaam, wakati akizindua mabweni mapya ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Alisema anafahamu kuwa idadi ya watumishi wenye vyeti feki ni zaidi ya 9,000 na anaisubiri ripoti hiyo kwa ajili ya kuifanyia kazi.

“Kwa hiyo mnaweza mkaona shida zilizopo katika nchi hii huku wafanyakazi hewa karibu 19,000, wanafunzi hewa ni zaidi ya 56,000, kila mahali unapokwenda ni matatizo, lakini ni lazima niyatatue matatizo kwa sababu mlinichagua kwa ajili hiyo,” alisema wakati akihutubia katika hafla ya uzinduzi huo iliyohudhuriwa pia na Waziri Mkuu Mstaafu, Jaji Joseph Warioba.

Wengine ni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Prof. Joyce Ndalichako, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi na Waziri wa Sheria na Katiba, Prof. Kalamagamba Kabudi.

Wakati Rais akitoa kauli hiyo jana, tayari zipo taarifa zinazodai kuwa orodha ya watumishi wa umma ambao wamebainika kuwa na vyeti feki itawekwa hadharani Aprili 30, mwaka huu.

Zaidi inaelezwa kuwa, sakata hilo la vyeti feki linawagusa pia mabalozi ambao ni wawakilishi wa Watanzania katika mataifa mbalimbali, wakuu wa wilaya na mikoa.

MTANZANIA Jumapili lilifanya juhudi za kumtafuta Waziri wa Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angela Kairuki, ili kuthibitisha taarifa hizo, lakini hakupatikana baada ya simu yake kupigwa mara kadhaa bila kupokewa.

Kauli ya Rais ya kusubiri ripoti ya watumishi waliobainika kuwa na vyeti feki imekuja wakati kukiwa na kelele nyingi juu ya uhalali wa vyeti vya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.

Itakumbukwa watumishi wote walitakiwa hadi kufikia Machi 1, 2017, wawe wameviwasilisha vyeti vyao.

Katika hatua nyingine, Rais aliwataka Watanzania washikane kwa pamoja kwa sababu anajua changamoto zipo.

Alisema kuwa, watu walizoea maisha ya ajabu, hivyo upo umuhimu mkubwa wa kuyabadilisha.

“Nyinyi hamjui, mimi ndiye ninayejua, mniache nishughulike nao ili dunia na Tanzania yetu iende mbele.

“Mabweni kama haya yasingekuwapo, yangekuwa kwenye mifuko ya watu. Watu walikuwa wanafanya kufuru na mimi hizo kufuru nimezifunga  kwa makufuru,” alisema Rais Magufuli.

Awali alimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumsaidia kutimiza kwa ahadi yake ya ujenzi wa mabweni ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Alisema chuo hicho kilikuwa na tatizo la makazi kwa muda mrefu na kwamba mazingira hayo yaliwasababisha wanafunzi kuishi kwenye vyumba vya ajabu mitaani.

“Nafahamu wengine badala ya kupanga vyumba, wanatumia vyumba vya wenzao kwa mtindo wa kubebana, unakuta kitanda kimoja kinabeba wanafunzi wawili au watatu, wanalala kwa zamu.

 “Pia wapo wanafunzi ambao walilazimika kuoa au kuolewa kule mitaani ili wapate huduma ya makazi,” alisema.

Rais Dk. Magufuli pia alifichua jinsi ambavyo wataalamu mbalimbali wamekuwa wakitumia miradi kujinufaisha kwa kuitoza gharama kubwa Serikali.

 “Nilipowapa wataalamu ramani ya mabweni haya wakaniambia hapa kunahitajikia Sh bilioni 150 -170 kukamilisha mradi huu, sasa unaweza kujiuliza una bilioni 10 ambazo ndio unaweza kubangaiza kuzipata mahali halafu unaambiwa gharama ya Sh bilioni 150, ilikuwa ni lugha ya kunikatisha tamaa.

“Lakini kwa bahati nzuri sikukata tamaa, nikaamua kutimiza lengo kwa kumwita Mkurugenzi Mkuu wa TBA, Elius Mwakalinga, nikamuonyesha ramani na akasema Sh bilioni 10 zinatosha,” alisema Rais.

Rais Magufuli aliongeza kwamba, kwa taarifa alizonazo, yale mabweni ya Mabibo yalijengwa kwenye miaka ya 2000 kwa gharama ya Sh bilioni 27 na yanachukua wanafunzi 4,000.

Alisema mabweni aliyoyazindua jana yamegharimu Sh bilioni 10 pekee na yanachukua idadi ya wanafuzi 3,840 .

“Huo ndio uzuri wa mahesabu, mnaweza kuona mabweni ya Mabibo ambayo yalijengwa wakati ule gharama yake ni Sh bilioni 27, lakini mabweni haya mapya gharama yake ni Sh bilioni 10 tu, kwa hiyo tukiamua watu wanaweza wakasema tunafanya miujiza kutoka kutumia gharama ya Sh bilioni 150-170 hadi Sh bilioni 10,” alisema.

Rais Magufuli alisema katika mabweni hayo mapya wanafunzi watatozwa Sh 500 kwa siku badala ya Sh 800.

Alisema kuwa, Serikali yake imeamua kuwekeza kikamilifu katika elimu, hasa kwa watoto wa masikini.

WANAFUNZI  WASIPANGIWE VYUO

Katika hatua nyingine, alitoa wito kwa Wizara ya Elimu kupitia Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) kuacha mpango wake wa kuwachagulia wanafunzi vyuo.

“Wanafunzi wakiwa na mamlaka ya kuchagua vyuo wavitakavyo nina uhakika UDSM kingefurika kwa wanafunzi wote 22,000 au 23,000 wanaotakiwa kuwa hapa. Na hata Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kingejaa kwa wanafunzi wote 43,000 wanaotakiwa kuwa pale.

“Tatizo lililopo sasa sifahamu ni biashara ya aina gani, mtu kafaulu na ana sifa zake anataka kusoma UDSM ili afaidi mabweni ya Magufuli, analazimishwa kupelekwa kwenye chuo ambacho hakina hata jina, hata ukikitafuta kwenye mtandao hakionekani,” alisema.

Rais Dk. Magufuli pia alionyesha shaka tabia ya TCU kukutana na baadhi ya wakuu wa vyuo vikuu ambao wamekuwa wakienda kuomba wapangiwe idadi ya wanafunzi watakaojiunga na vyuo vyao.

Alisema hafahamu kama wanapangiwa kwa rushwa, lakini upo ushahidi unaowaonyesha baadhi ya viongozi wa vyuo fulani waliofunga safari kwenda kuwaona viongozi wa TCU.

“Walikwenda kwa ajili ya kuomba wapangiwe wanafunzi, au kutoa shukrani au hata kuwasalimu tu, sasa kwa Wizara ya Elimu na wengine tambueni kuwa watoto wawe na haki ya kuchagua vyuo wanavyovitaka.

“Kuna baadhi ya vyuo ambavyo havina ubora vinahakikisha vinapata wanafunzi wanaopata mikopo ya Serikali, kwamba wakipata wanafunzi 1,000 hicho chuo nacho kinapata asilimia fulani ya mkopo, ninajua mnanielewa…tuwaache wanafunzi wachague vyuo wanavyovitaka na vile ambavyo havitachaguliwa vife, kwa nini mnalazimisha?” alisema.

Alisema hoja si kuwa na vyuo vikuu 100, bali vichache vyenye kuchukua wanafunzi wengi.

“Kwa UDSM najua mmeanza kufundisha wanafunzi wa Shahada ya ‘Medicine’, siku nitakapofungua Chuo cha Muhimbili Campus ya Mloganzila wanafunzi hawa wahame hapa. Haiwezekani ukawa na UDSM ikawa na tawi Muhimbili,” alisema.

Dk. Magufuli pia alihoji yaliko mabasi ya UDSM yaliyokuwa yakitumika kubeba wanafunzi miaka ya nyuma.

AZUNGUMZIA UBALOZI ISRAEL

Katika hatua nyingine, alizungumzia uamuzi wake wa kurejesha uhusiano wa kidiplomasia na Israeli, ambapo alisema kuwa una manufaa makubwa.

“Nimeamua kurudisha uhusiano na Israel, kwa kumteua Balozi tu umekuja ujumbe wa watalii wapatao 600 kutoka nchi hiyo, fedha zimeingia,” alisema.

AMMWAGIA SIFA SWAHIBA MAALIM SEIF

Baada ya kuzindua mabweni ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Rais Magufuli alikwenda kuweka jiwe la msingi katika ujenzi wa nyumba za wakazi wa Magomeni Kota.

Akiwahutubia wakazi wa eneo hilo, alimshukuru Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Twaha Taslima (CUF), ambaye alisimama kidete kisheria kuwatetea wakazi hao  waliovunjiwa nyumba zao wakati wa utawala uliopita.

“Mateso yenu yanakaribia kufika mwisho, namshukuru ndugu Taslima, yeye ni mbunge anayetokana na CUF, lakini moyo wake ni CCM kabisa, nampongeza sana na huu ndio Utanzania wa kweli,” alisema Magufuli.

Alisema mradi wa ujenzi wa nyumba hizo utagharimu Sh bilioni 20 na yatajengwa majengo matano yenye ghorofa nane kila moja.

Alisema huo ni mwanzo na atajenga kwa mtindo huo kwenye maeneo yote ya Serikali yaliyokuwa na nyumba kama za Magomeni kota, ili kila Mtanzania hata muuza chipsi aweze kupata makazi bora.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles