23.5 C
Dar es Salaam
Thursday, May 26, 2022

MWIGULU ASHTUSHWA WANANCHI KIBITI KUFURAHIA POLISI KUUAWA

Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba (wa pili kushoto) akizungumza na Waandishi wa gazeti hili katika kituo cha polisi Bungu, wilayani Kibiti. Wengine pichani ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni (kushoto) na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikiro (wa tatu kushoto)

Na AZIZA MASOUD-DAR ES SALAAM

KIZA kimeendelea kutanda tukio la  mauaji ya askari wanane wa Jeshi la Polisi waliouawa na majambazi eneo la Mkengeni Kijiji cha Uchembe Kata ya Mjawa, Kibiti mkoani Pwani, huku viongozi wa juu wa jeshi hilo wakishangazwa na hatua ya wananchi kufurahia tukio hilo.

Kitendo cha baadhi ya wananchi kufurahia na kushindwa kutoa ushirikiano katika tukio hilo inaonyesha kuna siri nzito imefichika.

 Akizungumza wakati wa kutoa salamu za rambirambi katika eneo la Polisi Barracks ambako miili ya askari hao iliagwa rasmi, Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi, Mwigulu Nchemba, alisema hali inaonyesha wazi kuwa  wananchi wanafurahishwa na tukio hilo  na huenda wakawa wanawajua wahusika waliofanya uhalifu huo.

“Kwa kiasi kikubwa wananchi wameonekana kufurahishwa na jambo hili, hii ni kwa kuwa wanawajua wahusika na ndio maana vitendo hivi vinazidi kuendelea.

“Kitendo hiki si cha bahati mbaya bali kilipangwa, waliofanya hivyo watambue kuwa watashughulikiwa kwa mazingira hayo hayo kwa kuwa hawajatoka mbali wapo eneo hilo hilo, wananchi tunawaomba mtoe taarifa za watu hao kwa hiyari la sivyo tutatumia nguvu kuzipata,” alisema Mwigulu.

Alisema hakuna mtu wa kutoka mbali anayeweza kufika katika eneo fulani na kuua zaidi ya watu wa eneo husika.

Alisisitiza kuwa hata matukio ya mfululizo ya kuuawa kwa wenyeviti wa Serikali za Mitaa ambao wanafuatwa katika maeneo wanapoishi ni wazi  yanafanywa na wenyeji wa maeneo husika.

“Mfano idara ya wanyamapori waliuawa askari, lakini jambo la kushangaza wakati waliohusika wakiwa hapo wananchi waliruka maiti hizo na kwenda kwa ujasiri kuchukua mkaa bila kuogopa.

 “Najiuliza walipata wapi ujasiri huo kama hawawajui wahusika, tulipeleka askari ili kuwalinda lakini kwa kupingana na hilo wakaamua kuwafanyia njama ili kuzuia hilo na kusababisha askari hao kuuawa,” alisema Mwigulu.

Aidha, Mwigulu aliwataka polisi kuhakikisha wanasimamia ukataji wa nyasi zilizopo katika eneo hilo na endapo atabainika mtu yeyote anayeshirikiana  na kikundi hicho cha uhalifu awajibishwe ili kulipa damu ya askari hao.

Mbali na hilo, Mwigulu alivitaka vyombo husika kuhakikisha wanawasimamia askari wanaopata matatizo wakiwa kazini ili waweze kulipwa haraka tofauti na ilivyo sasa.

Aliomba majalada yanayohusu askari kuumia na wanaodai yapitishwe haraka kwakufuata itifaki wakati akiangalia namna ya kuhakikisha anarekebisha sheria iliyopo inayosababisha ucheleweshwaji huo.

Mwigulu pia aliwataka viongozi wote wa jeshi hilo kukutana ili kupangiana majukumu ikiwa ni kuashiria kuanza rasmi kazi ya operesheni. 

Kauli ya IGP

Kwa upande wake Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Ernest Mangu, alisema tukio hilo ni la kusikitisha kwa kuwa ni mara ya pili kutokea kwa askari ambao wanakuwa kazini.

Alisema matukio hayo huwa yanafanywa na watu ambao hawataki nchi iwe na amani na kwamba hawatavumilia kwa kuwa watu hao wanaonyesha wamejipanga kuwakatisha tamaa jeshi hilo.

 “Tutachukua hatua hadi watapatikana waliohusika na kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria, tunatambua wananchi wa Mkuranga, Kibiti na Ikwiriri wanawajua wahalifu wanaotumia maeneo hayo na wanaishi nao lakini hawataki kuwataja,” alisema IGP Mangu na kuongeza:

“Hii ni dalili tosha kwamba baadhi ya wananchi wamegeuka kuwa sehemu ya maficho ya wahalifu kama wao wenyewe (wananchi) hawahusiki na hilo hivyo watambue tutawasaka kila kona tena kwa kutumia nguvu maana hawataki kutupa taarifa.”

IGP Mangu pia aliahidi kuwachukulia hatua watu wote wanaoandika maneno ya kejeli katika mitandao ya kijamii na kusisitiza kuwa watakamatwa na kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria ili iwe fundisho.

Kauli ya RPC Pwani

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Onesmo Lyanga, alisema tukio hilo ni la kusikitisha kwa kuwa jukumu walilokuwa wakitekeleza ni halali na kwamba hiyo inawapa fursa nyingine ya kujipanga zaidi kukabiliana na wahalifu.

“Damu hiyo haiwezi kumwagika bure, tutahakikisha wahusika waliofanya kitendo hicho cha kiharamu wanakamatwa na kushughulikiwa ipasavyo,” alisema.

Askari waliofariki ni pamoja na Mkaguzi Msaidizi, Peter Kigugu, Koplo Francis, PC Haruna, PC Jackson, PC Zacharia, PC Siwale, PC Maswi na PC Ayoub, ambapo pia walipora bunduki 7 zikiwemo SMG 4, katika orodha ya askari hao ambao saba wametokea Morogoro na mmoja Lindi, mtu aliyetajwa kuwa na umri mkubwa anaonyesha amezaliwa 1979 wakati mdogo akiwa amezaliwa 1995.

Tukio hilo lilitawaliwa na vilio na simanzi kutoka kwa ndugu na jamaa waliofika kutoa heshima zao za mwisho.

 Viongozi wengine waliohudhuria tukio hilo ni pamoja na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Biswalo Mganga, Kamishna wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
192,293FollowersFollow
541,000SubscribersSubscribe

Latest Articles