KATIKA kile ambacho kwa wakati huu kinaweza kuonekana kama kimemshtua Rais Jakaya Kikwete, ni hatua yake ya kurejea kauli ambayo imekuwa ikitolewa na viongozi wa Afrika dhidi ya Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC).
Kwamba viongozi wa Afrika hawafurahii kwa namna ambavyo mahakama hiyo inavyofanya kazi zake kwa kuwashughulikia zaidi viongozi wa mataifa ya Afrika.
Kauli hiyo ya Rais Kikwete ambayo aliitoa jana jijini Dar es Salaam wakati akifungua mkutano wa 16 wa Umoja wa Wanasheria wa Jumuiya ya Maendeleo ya Uchumi Kusini mwa Afrika-SADC, imekuja siku moja baada ya ICC kueleza kwamba inafuatilia mwenendo wa uchaguzi nchini.
Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC, Fatou Bensouda, amekaririwa na vyombo vya habari vya Aljazeera na Gambia Today akisema kuwa Mahakama hiyo inatazama kwa umakini mkubwa yanayotokea Tanzania kuelekea Uchaguzi Mkuu kama ilivyofanya katika nchi za Kenya, Ivory Coast na Congo na kwamba itachukua hatua za haraka kama kutakuwa na uvunjaji wa haki za binadamu.
Kauli hiyo ya Bensouda ilitanguliwa na ile iliyotolewa siku chache zilizopita na mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), anayeungwa mkono na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa.
Wiki iliyopita akiwa katika ziara ya kutafuta wadhamini katika mikoa ya Arusha na Mwanza, Lowassa alilitahadharisha Jeshi la Polisi juu ya uwepo wa Mahakama ya ICC kutokana na kitendo chake cha kutumia nguvu dhidi ya wapinzani kwa kuupiga mabomu msafara wake.
Zaidi Lowassa pamoja na viongozi wa Ukawa walisema endapo vyombo vya dola vitakiuka haki za binadamu hawatasita kumshtaki Rais Kikwete katika mahakama hiyo huku wakisema tayari wameanza kukusanya ushahidi wa kwenda kushitaki.
Hata hivyo, Rais Kikwete akizungumza na wanasheria hao wa SADC, aliutaka umoja huo kuwa imara katika kuzungumzia uonevu unaofanywa na ICC dhidi ya viongozi wa Afrika.
“Kuna hizi kauli zinazotolewa na viongozi wa Afrika kwamba Mahakama ya Kimataifa inazionea nchi za Afrika na kuyaacha mataifa mengine ambayo yanaonekana kabisa kuwa na machafuko lakini viongozi wake hawashughulikiwi,” alisema Rais Kikwete.
Alisema mfumo wa Mahakama hiyo unaonekana kuwa ni wa kibaguzi na hivyo kushindwa kutenda haki.
“Kuna viongozi katika sayari hii wanafanya makosa lakini mahakama hizi haziwashughulikii. Mahakama hizi zinatakiwa kutenda haki.
“Haiwezekani viongozi wa mataifa madogo ndio wanaonekana kufanya uhalifu lakini wale wa mataifa makubwa wanaachwa,” alisema Kikwete huku akitolea mfano wa Rais wa Syria, Bashir Al-Asaad, ambapo alisema aliwahi kuzungumza na Luis Ocampo kipindi akiwa Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC kuhusu kushughulikia mataifa haya makubwa.
“Nilimuuliza Ocampo mbona mataifa makubwa yanaonekana waziwazi kufanya uhalifu dhidi ya binadamu lakini ICC haifanyi kitu? Lakini cha ajabu alinijibu itafanya nini…hii inaonyesha hakuna usawa,” alisema Rais Kikwete.
Pamoja na hayo, Rais Kikwete alisema ataachia madaraka kwa amani na kwamba baada ya hapo atarejea kijijini kwake kujishughulisha na kilimo na ufugaji.