27.7 C
Dar es Salaam
Monday, February 26, 2024

Contact us: [email protected]

Wagombea wanne wapitishwa urais

Mwenyekiti-Tume-ya-Uchaguzi-Jaji-Damian-Lubuva-620x309Aziza Masoud na Grace Shitundu, Dar es Salaam

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imeteua wagombea urais wanane kati ya 13 waliochukua fomu kwa ajili ya kugombea nafasi hiyo katika Uchaguzi  Mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba mwaka huu.

Idadi hiyo inataka kufanana na ile ya mwaka 2010 ambapo Tume hiyo iliteua wagombea saba kuwania nafasi hiyo.

Wagombea waliokidhi vigezo na kuteuliwa na NEC ni pamoja na Dk. John Magufuli wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Edward Lowassa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) pamoja na Chifu Lutalosa Yemba wa Chama cha ADC.

Wengine ni Machmillan Lyimo wa Chama cha Tanzania Labour Party (TLP), Fahmi Dovutwa wa Chama cha UPDP, Janken Kasambala wa NRA, Hashim Rungwe wa Chauma na Anna Mghwira wa ACT-Wazalendo.

Akizungumza wakati akifanya majumuisho ya kuhakiki fomu za wagombea na kupitisha majina yao, Mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Lubuva, alisema kati ya wagombea 13 waliochukua fomu za kugombea nafasi hiyo wagombea wanane wamepitishwa na watatu ambao hawakupitishwa wameshindwa kutimiza vigezo wakati mmoja hakutokea kabisa.

Aliwataja wagombea hao watatu ambao hawakutimiza vigezo kuwa ni wa vyama vya CCK, ADA-TADEA pamoja na DP.

Alisema wagombea walioteuliwa wataanza kampeni leo na amesisitiza kuzingatiwa kwa maadili ya uchaguzi ili kukamilisha zoezi hilo kwa amani.

CHADEMA WAFUNGUA PAZIA

Pazia la kurudisha fomu hizo lilifunguliwa na mgombea wa Chadema, Lowassa ambaye alifika katika ofisi ya NEC saa 3:40 asubuhi akiwa na msafara wa king’ora wenye magari sita uliokuwa ukiongozwa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad.

Baada ya gari la Maalim Seif kuingia katika geti la ofisi za NEC lilifuatia lile lililokuwa likimsindikiza Lowassa aliyekuwa na mgombea mwenza wake, Juma Duni Haji, wakiambatana na mmoja wa wanasheria na chama hicho, John Malya.

Gari lililofuata baada ya hilo lilikuwa ni lile lililokuwa limembeba mke wa mgombea huyo Mama Regina Lowassa.

Waliposhuka viongozi hao lilikuja gari jingine dogo lililokuwa limembeba aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Hamis Mgeja na aliyekuwa mbunge wa Arumeru Magharibi, Goodluck Olemedeye ambao wote hivi karibuni wamehamia Chadema.

Hata hivyo, watu waliokuwa wakishuhudia msafara huo ambao ulikuwa ukiachana kila gari kwa dakika mbili mbili walishangazwa na staili aliyoitumia Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ambaye alikuja akiwa kwenye gari ndogo nyeusi aina ya Rush ambapo ilimshusha nje ya geti la ofisi za NEC na baadaye kuingia ndani.

Baada ya Mbowe, kwa upande wa viongozi Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia, alikuwa wa mwisho kuingia na baadaye alifuata aliyekuwa mbunge wa Segerea, Makongoro Mahanga.

Msafara huo ulitumia nusu saa ndani ya ofisi hizo ambapo baada ya Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Ramadhani Kailima kujiridhisha mgombea pamoja na wapambe wake alitoka nje.

Akizungumza baada ya zoezi hilo, Lowassa aliwataka Watanzania wamuombee kwakuwa mchakato umeshaanza.

“Kipenga kimeshapulizwa, Watanzania na wana Ukawa naomba mniombee,” alisema Lowassa.

Baada ya hapo msafara huo uliondoka katika viwanja vya ofisi hiyo saa 4:20 asubuhi.

 

CCM NAYO NA KING’ORA

Baada ya dakika kama 40 kupita tangu msafara wa Chadema na viongozi wa Ukawa uondoke, ilipotimu saa 5:01 asubuhi uliwasili msafara wa mgombea wa CCM, Dk. Magufuli akiwa na mgombea mwenza wake, Samia Suluhu Hassan.

Kama ilivyokuwa kwa mgombea wa Chadema, Lowassa msafara wa Magufuli nao uliwasili kwa king’ora cha pikipiki.

Kabla ya gari la Magufuli kuingia lilianza gari la Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Philip Mangula na baadaye lilifuata gari la Magufuli.

Mbali na Mangula, Magufuli pia alisindikizwa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wa chama hicho, Abdallah Bulembo, Zakhia Meghji, Katibu Halmashauri Kuu Idara ya Oganaizesheni, Mohamed Seif Khatib, Mwenyekiti wa Mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhani Madabida, Mwenyekiti wa Wilaya ya Kinondoni, Salum Madenge.

Magufuli ambaye hakutumia lifti kama alivyofanya Lowassa, alipanda kwa kutumia ngazi hadi ghorofa ya saba ambapo baada ya kumaliza shughuli hiyo alitoka saa 5:35 asubuhi ambapo alisema ameteuliwa kugombea baada ya kutimiza vigezo vilivyowekwa na NEC.

“Tumefuzu vigezo baada ya kujaza fomu zote kwa ukamilifu subirini siku ya kampeni,” alisema Magufuli.

Baada ya kutoa kauli hiyo, Magufuli alielekea katika gari hata hivyo kabla ya kupanda alirudi na kuomba kupiga picha ya pamoja na waandishi wa habari waliokuwapo eneo hilo.

MGOMBEA WA TLP NA GARI MOJA

Ilipofika saa 5:40 asubuhi alikuja mgombea wa TLP, Machmillan Lyimo, akiwa ameambatana na mgombea mwenza wake, Hussein Juma Salum katika gari moja.

Akizungumza baada ya kuteuliwa Lyimo, alisema chama chake kimekuja na sera ambayo itaambatana na bajeti utuli ambayo itaendesha nchi na kuwekeza kwa watu kupitia rasilimali zilizopo.

Alisema kampeni za chama hicho zitafanyika nchi nzima na zinatarajiwa kuzinduliwa Agosti 25 mkoani Kilimanjaro.

ADC

Kwa upande wake mgombea wa ADC, Chifu Lutalosa Yemba, akiwa na mgombea mwenza wake, Said Miraji Abdallah, walifika katika ofisi hizo wakiwa na msafara wa gari mbili ambazo zilifuatana.

Akizungumza baada ya kukabidhi fomu, Chifu Yemba alisema lengo la kugombea nafasi hiyo ni kutaka kuwatumikia Watanzania kwa uadilifu pamoja na kuboresha elimu na afya.

ACT

Mgombea wa ACT Wazalendo ambaye ni mwanamke pekee aliyeteuliwa kuwania nafasi hiyo na NEC, Anna Mghwira, alifika saa 7:30 mchana lakini alirudishwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume hiyo kutokana na kutokuwa na hati ya kiapo ambapo alilazimika kwenda kuitafuta.

Baada ya kama dakika 20 kupita Anna ambaye alikuwa na mgombea mwenza wake na maofisa kadhaa wa chama hicho, alirejea katika ofisi hizo akiwa na hati hiyo na kisha jina lake kuteuliwa.

Sababu za kukatwa kwa Mtikila

Mkurugenzi wa uchaguzi wa NEC, Kailima alisema Mtikila alishindwa kutimiza vigezo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kukosa wadhamini.

“Kwanza hana mgombea mwenza, hajatoa tamko la kisheria, amefika baada ya muda uliopangwa, hajawakilisha fomu namba nane yenye maelezo binafsi,” alisema Kailima.

Alisema mgombea huyo pia hakujaza tamko la fomu namba kumi pamoja na kuwasilisha dhamana ya Sh milioni moja.

Alisema kwakuwa tume inaongozwa na kanuni na taratibu zote zimewekwa kwa mujibu wa sheria, Mtikila hatoweza kuwa mmoja wa wagombea wa nafasi hiyo.

VIGEZO VYA WAGOMBEA

Vigezo hivyo ni pamoja na kuwa na taarifa za maelezo binafsi za wagombea wote ambazo zilijazwa vizuri, tamko la mgombea kiti cha urais na makamu wake limejazwa kwa ukamilifu na kuweka saini na tarehe.

Vigezo vingine ni pamoja na kujaza tamko la kisheria lililojazwa na kutiwa muhuri wa Mahakama Kuu, kutimiza majina ya wadhamini kwa mikoa 10 iliyotakiwa.

Vingine ni uthibitisho wa chama, uthibitisho wa msimamizi wa uchaguzi, dhamana ya Sh milioni moja na kujaza kikamilifu fomu namba 10 ya tamko la kuheshimu na kutekeleza maadili ya uchaguzi.

Wagombea waliotimiza vigezo hivyo walikabidhiwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Maadili ya uchaguzi ya mwaka 2015, Kanuni za wagombea urais na ubunge na sheria na kanuni za gharama za uchaguzi na Mwenyekiti wa NEC, Jaji Lubuva.

WALIOENGULIWA WANENA

Mgombea wa CCK, Dk. Godfrey Malisa ambaye alienguliwa baada ya kupoteza fomu ya 8A, alisema wameshindwa kuteuliwa kutokana na urasimu na vikwazo vya wazi vinavyowekwa na Tume inayokibeba chama tawala.

Alisema suala la uadilifu katika mchakato wa uchaguzi halipo hivyo wao wamelipeleka suala hilo mahakamani ambapo hukumu yake itatolewa siku ya Jumanne.

Naye Mchungaji Mtikila alisema si kweli hawakutimiza vigezo bali mgombea mwenza alipata matatizo ambapo mke wake alikuwa mgonjwa.

“Katika sheria hakuna kipengele kinachozuia mgombea mke wake  asipatwe na matatizo, hata hivyo kukosa nafasi ya kugombea sio mwisho sasa nguvu yangu nitaipeleka majimboni,” alisema.

Alisema kushindwa kwake kutamuwezesha kupata wakati mzuri wa kushughulikia masuala ya kudai Tanganyika na kuzuia Katiba iliyopendekezwa.

Kwa upande wake mgombea wa ADA-TADEA, John Lifachipaka, alipoulizwa sababu za kuenguliwa alijibu kuwa waulizwe Tume ya Uchaguzi.

VITUKO VYA WAGOMBEA

Katika zoezi hilo la urudishaji wa fomu lilitawaliwa na vituko mbalimbali ambapo mgombea wa Chaumma, Rungwe alisahau picha ndogo (passport size) aliyotakiwa kufika nayo wakati wa kurudisha fomu hali iliyomfanya kuirudia.

Tukio jingine lililofurahisha watu ni hatua ya wagombea hao wa DP na ADA- TADEA kufika NEC wakiwa na usafiri wa bajaji tofauti na wagombea wengine waliotangulia.

- Advertisement -
Previous article
Next article

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles