KULWA MZEE – DAR ES SALAAM
HUKUMU ya viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), imeendelea kuzua gumzo huku chama hicho kikisema kimekusanya zaidi ya Sh milioni 200 za kuwawekea dhamana viongozi wake, huku Chama cha Mapinduzi (CCM) kikimlipia faini ya Sh milioni 30 kada wake mpya, Dk. Vicent Mashinji.
Dk. Mashinji alikuwa Katibu Mkuu wa Chadema kwa miaka minne tangu 2016 kabla ya kupoteza nafasi hiyo mwaka huu baada ya uchaguzi mkuu wa chama hicho na kisha akajiunga na CCM.
Juzi Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba aliwatia hatiani Dk. Mashinji na viongozi nane wa Chadema, na walihukumiwa kulipa faini ya jumla ya Sh milioni 350 ama kwenda jela miezi mitano kwa kila kosa baada ya kupatikana na hatia kwenye makosa 12 kati ya 13 yaliyokuwa yakiwakabili kwenye kesi ya uchochezi.
Katika hukumu hiyo iliyosomwa kwa takribani saa nne, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alihukumiwa kulipa faini ya Sh milioni 70, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, Sh milioni 40, Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, Sh milioni 40, Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa, Sh milioni 40 na Mbunge wa Bunda mjini, Ester Bulaya, Sh milioni 40.
Wengine ni Mbunge wa Tarime mjini, Ester Matiko, Sh milioni 30, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar Sh milioni 30 na Katibu Mkuu wa chama hicho ambaye pia ni Mbunge wa Kibamba, John Mnyika, Sh milioni 30.
Jana Dk. Mashinji alifanikiwa kutoka gerezani baada ya Katibu Mwenezi wa CCM, Humphrey Polepole kufika katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kufuata utaratibu na kupewa namba maalumu ya kufanya malipo ya Sh milioni 30.
Akizungumza katika viwanja vya mahakama, Polepole alisema alifuata utaratibu ili wamtoe Dk. Mashinji.
Polepole aliambatana na wanachama wengine wa CCM pamoja na Happynes Mashinji ambaye ni mke wa Dk. Mashinji.
“Tayari tumeshapewa ‘control number’, tumelipa tumepewa utaratibu wa kwenda kumtoa gerezani, tunaelekea huko, tunaushukuru uongozi na Chama Mkoa wa Dar es Salaam kwa kujitoa.
“Kulikuwa na mchakato wa ndani wa viongozi na wanachama, nashukuru kwa kusimama pamoja na ndugu yetu Mashinji, utaratibu wa kielektroniki tumeshalipa.
“Tumeridhishwa na hukumu iliyotolewa, chama chetu kikubwa kina wenye uwezo, Mashinji amekuwa mpya, anaaminika katika utawala wa sheria, anatii sheria bila shuruti,” alisema Polepole.
Mke wa Mashinji, Happynes alikishukuru chama hicho na alisema anaufurahia umoja huo kwani haubagui kwa kuwa mwanachama mpya.
“Kama familia hatukutegema kama mambo yataenda haraka namna hiyo, tunashukuru,” alisema Happynes.
DK. MASHINJI
Baada ya kupata dhamana jana mchana, Dk. Mashinji alisema hakutegemea kama wanaCCM watamlipia faini hiyo.
“Sikutegemea wangelifanya jambo hili kwa uzito kama huu, maana hadi jana familia yangu ilikuwa inaendelea kutafuta fedha ili kunitoa, ila leo wana CCM Mkoa wa Dar es Salaam wamejiunga kwa pamoja na kunilipia faini, nashukuru nipo chama dume kwa ajili ya kutoa mchango wangu kwa taifa,” alisema Dk. Mashinji.
CHADEMA NA MICHANGO
Chadema kwa upande wao wamesema wamekusanya zaidi ya Sh milioni 234.7 kutoka kwa wananchi ili kuwatoa gerezani viongozi wao.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Kaimu Mwenyekiti wa Chadema, Said Issa Mohamed, alisema baada ya kutangaza harambee hiyo juzi wanachama wao na wasio wanachama wamejitoa kwa moyo.
“Tuko hapa kwa ajili ya jambo lililowatokea viongozi wetu jana ili kuwapasha habari wanachama wetu.
“Tangu tulipotangaza kuanza harambee hii, mwitikio ulikuwa mkubwa, kuna waliokwenda moja kwa moja kuuza mayai yao ili waweze kuchangia,” alisema Mohamed ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Chadema Zanzibar.
Alisema kuwa kiasi cha fedha zilizochangwa kupitia mitandao ya simu hadi jana wakati wanajiandaa kwa mkutano huo na waandishi wa habari ni zaidi ya Sh milioni 176.9.
Fedha zilizokuwa zimechangwa katika akaunti ya benki ni zaidi ya Sh milioni 52.7, huku fedha taslimu zilizowasilishwa katika ofisi za Makao Makuu ya chama hicho Dar es Salaam ni zaidi ya Sh milioni 4.7.
Mohamed alisema kati ya fedha hizo tayari Sh milioni 100 zimetumika kushughulikia taratibu za kuwatoa wabunge Ester Bulaya (Bunda), Halima Mdee (Kawe) na Ester Matiko (Tarime mjini).
“Tunategemea mawakili wetu watafanikisha hili leo na kama si leo basi kesho mapema. Tunawaomba wapenda maendeleo wote kuungana kumpinga mkoloni mweusi,” alisema Mohamed.
ZITTO ACHANGIA FAINI
Wakati huo huo, chama hicho kilipokea mchango wa awali wa Sh milioni mbili kutoka kwa Kiongozi wa Chama cha ACT wazalendo, Zitto Kabwe, aliyeziwasilisha katika ofisi za Chadema jana mchana huku akiahidi kuendelea kuchangia pamoja na kuwashawishi wanachama wake kuendelea kuchangia.
NYALANDU
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Lazaro Nyalandu, alisema adhabu zilizotolewa na mahakama dhidi ya viongozi wao hazijawahi kutolewa na wakoloni, wakati wa kuungana na Zanzibar na kwamba kama zimewahi kutolewa basi hakuna rekodi zake.
Alisema chama hicho kitakapochukua dola Oktoba mwaka huu, moja ya mambo ambayo kitayarekebisha ni pamoja na mfumo wa utoaji haki ili usimwonee mtu yeyote na kwamba ukirekebishwa utawanufaisha watu wote.
KIGAILA
Kaimu Katibu Mkuu wa Chadema, Kigaila Benson, alisema faini walizotozwa viongozi wao ni uonevu kwa sababu hakuna kifungo cha miezi mitano chenye faini ya Sh milioni 10.
Benson alisema kuwa kitendo cha watu kuchangia zaidi ya Sh milioni 170 kwa muda usiofika saa 24 inawathibitishia Watanzania kuwa wanaweza kupigana na vita ya kubambikiziwa kesi.
Alisema miongoni mwa watu waliochangia ni pamoja na watumishi wa umma na wanachama wa CCM na askari polisi.