28.7 C
Dar es Salaam
Sunday, November 28, 2021

MWELEKEO BAJETI 2020/21 Vipaumbele Uchaguzi Mkuu, miundombinu

RAMADHAN HASSAN – DODOMA

SERIKALI imetoa Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na ukomo wa bajeti ya Serikali kwa mwaka 2020/21, ambapo inatarajia kukusanya na kutumia Sh trilioni 34.88, ambazo kwa kiasi kikubwa zitajikita kwenye miradi ya ujenzi na Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, akiwasilisha mapendekezo mbele ya wabunge Dodoma jana, alisema kwa kuzingatia sera za bajeti kwa mwaka 2020/21, Sh trilioni 34.88 zinatarajiwa kukusanywa na kutumika.

 “Mapendekezo ya kiwango na ukomo wa bajeti ya mwaka 2020/21 yamezingatia mahitaji halisi ya ugharamiaji wa miradi mikubwa ya kimkakati, ulipaji wa mishahara na deni la Serikali pamoja na utekelezaji wa vipaumbele vingine vya taifa.

 “Mapendekezo ya kiwango na ukomo yanajumuisha mapato ya ndani ya Sh trilioni 24.07 sawa na asilimia 69 ya bajeti yote, mikopo ya ndani Sh trilioni 4.90, mikopo ya nje yenye masharti ya kibiashara Sh trilioni 3.04 na misaada na mikopo nafuu kutoka kwa washirika wa maendeleo Sh trilioni 2.87 sawa na asilimia 8.2 ya bajeti yote,” alisema Dk. Mpango.

Alisema katika bajeti hiyo, Sh trilioni 21.98 zimetengwa kwa matumizi ya kawaida na Sh trilioni 12.90 za matumizi ya maendeleo sawa na asilimia 37.0 ya bajeti yote.

“Bajeti ya maendeleo inajumuisha Sh trilioni 10.16 fedha za ndani, sawa na asilimia 78.8 na Sh trilioni 2.74 fedha za nje. Matumizi haya yanajumuisha gharama za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020,” alisema Dk. Mpango.

Alisema bajeti ya mwaka 2020/21 inazingatia azma ya Serikali ya awamu ya tano chini na uongozi wa Rais Dk. John Magufuli, ya kujenga uchumi wa viwanda na kuboresha ustawi wa jamii.

Dk. Mpango alisema bajeti ya mwaka 2020/21 ni ya mwisho katika utekelezaji wa ilani ya CCM ya mwaka 2015.

“Hivyo, bajeti hii itaendelea na utekelezaji wa maeneo makuu manne yaliyoainishwa katika ilani, ambayo ni kuondoa umasikini na kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana.

“Mengine ni kuendeleza vita dhidi ya rushwa na ubadhirifu wa mali za umma na kuendelea kudumisha amani, ulinzi na usalama wa maisha ya wananchi na mali zao.

“Ili kufikia malengo hayo, Serikali itaendelea kuongeza na kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani kugharamia shughuli za Serikali, ikiwemo utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati na uboreshaji wa huduma za kijamii kwa lengo la kuleta maendeleo ya haraka.

“Aidha, Serikali itaendelea kusimamia nidhamu katika matumizi ya fedha za umma na kufanya ufuatiliaji na tathmini ya matumizi, hususan katika miradi ya maendeleo.

“Lengo kuu ni kupata thamani halisi ya fedha katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

“Kama mnavyofahamu, mwezi Oktoba mwaka huu tutafanya Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani. Kwa upande wa Serikali, tumejipanga kikamilifu katika maandalizi ikijumuisha mahitaji ya kibajeti kwa ajili ya kufanikisha uchaguzi huo.

“Napenda kuchukua nafasi hii kuwasihi Watanzania wote washiriki uchaguzi huu muhimu na wazingatie umuhimu wa kuendelea kudumisha amani ya nchi yetu.

“Kila anayehusika atekeleze wajibu wake kulingana na nafasi yake tukianzia kwa viongozi wa madhehebu ya dini, wagombea wa nafasi mbalimbali, wapigakura, Tume ya Taifa ya Uchaguzi, vyombo vya ulinzi na usalama, wasimamizi wa uchaguzi, vyombo vya habari na hata waangalizi wa kimataifa watakaokuwepo nchini wakati huo.

“Napenda kuwahakikishia Watanzania na jumuiya ya kimataifa kuwa uchaguzi utazingatia haki na utafanyika kwa usalama, amani na utulivu wa hali ya juu,” alisema Dk. Mpango.

SERA ZA MAPATO NA MATUMIZI MWAKA 2020/21

Dk. Mpango alisema katika mwaka 2020/21, mapato ya Serikali yanatarajiwa kuongezeka na hivyo kuweza kugharamia miradi mikubwa ya kimkakati.

Alisema katika kufanikisha azma hiyo, sera za mapato kwa mwaka 2020/21 zitajielekeza kwenye kuboresha mazingira ya uendeshaji biashara na uwekezaji kwa kutekeleza mpango kazi wa kuboresha mazingira ya biashara nchini ili kukuza biashara ndogo na za kati kwa ukuaji endelevu wa uchumi.

Dk. Mpango alisema zitajikita pia kuboresha mazingira ya ulipaji kodi kwa hiyari pamoja na upanuzi wa wigo wa kodi, kuimarisha usimamizi wa sheria za kodi ili kutatua changamoto za ukwepaji kodi na kupunguza upotevu wa mapato.

Alisema pia zitajikita kuimarisha usimamizi wa ukusanyaji wa mapato ya ndani yakijumuisha mapato ya mamlaka za Serikali za Mitaa kwa kuhimiza matumizi sahihi ya mifumo ya Tehama, kuwianisha na kupunguza tozo na ada mbalimbali ili kuboresha mazingira ya kufanya biashara na uwekezaji.

Alisema zitajikita pia kuendelea kutekeleza Mwongozo wa Ushirikiano wa Maendeleo Tanzania (DCF) na kuendelea kukopa kutoka katika vyanzo vyenye masharti nafuu na mikopo inayotolewa kwa utaratibu wa udhamini kutoka taasisi za udhamini wa mikopo.

“Katika mwaka 2020/21, Serikali itaendelea kusimamia nidhamu ya matumizi ya fedha za umma lengo kuu ni kuziba mianya ya uvujaji wa fedha za umma na kuelekeza kiasi kikubwa cha fedha kwenye miradi mikubwa ya kimkakati na miradi mingine muhimu. Aidha, Serikali itaendelea kuhakiki, kulipa na kuzuia ongezeko la uzalishaji wa madeni ya Serikali,” alisema Dk. Mpango.

Mchanganuo wa mapato na matumizi

A. Mapato ya Ndani – Serikali Kuu Sh trilioni 23.250

(i) Mapato ya Kodi (TRA) Sh trilioni 20.325

(ii) Mapato yasiyo ya kodi Sh trilioni 2.924

B. Mapato ya Halmashauri Sh bilioni 814

C. Misaada na Mikopo nafuu kutoka Washirika wa Maendeleo Sh trilioni 2.874

(i) Misaada na Mikopo nafuu – GBS Sh bilioni 138

(ii)Misaada na Mikopo nafuu ya Miradi Sh trilioni 2.460

(iii)Misaada na Mikopo nafuu ya Kisekta Sh bilioni 275

D. Mikopo ya Ndani na Nje Sh trilioni 7.939

(i) Mikopo ya Nje Sh trilioni 3.035

(ii) Mikopo ya Ndani Sh trilioni 1.588

(iii)Mikopo ya Ndani- Rollover Sh trilioni 3.316

JUMLA YA MAPATO YOTE (A+B+C+D) Sh trilioni 34.879

Matumizi

E. Matumizi ya Kawaida Sh trilioni 21.980

 (i) Mfuko Mkuu wa Serikali Sh trilioni 10.476

-Malipo ya Riba Ndani Sh trilioni 1.630

-Malipo ya Mtaji Ndani (Rollover) Sh trilioni 3.316

-Malipo ya Mtaji Nje Sh trilioni 2.463

– Malipo ya Riba Nje Sh trilioni 1.239

– Michango ya Serikali kwenye Mifuko ya Hifadhi za Jamii Sh trilioni 1.299

-Matumizi Mengine ya Mfuko Mkuu Sh bilioni 527

(ii) Mishahara Sh trilioni 7.762

(iii)Matumizi Mengineyo (OC) Sh trilioni 3.741

– Malipo ya Madeni yaliyohakikiwa Sh bilioni 200

– Matumizi mengineyo Sh trilioni 3.541

F. Matumizi ya Maendeleo (Asilimia 37.0) ya BGT Sh trilioni 12.899

(i) Fedha za Ndani Sh trilioni 10.163

-Malipo ya Madeni yaliyohakikiwa Sh bilioni 400

-Ugharamiaji wa SGR Sh trilioni 2.100

-Ugharamiaji wa Mradi wa Umeme wa Julius Nyerere Sh trilioni 1.600

-Miradi mingine Sh trilioni 6.063

(ii)Fedha za Nje Sh trilioni 2.736

JUMLA YA MATUMIZI YOTE (E+F) Sh trilioni 34.879

NAKISI YA BAJETI (ASILIMIA YA PATO LA TAIFA) 2.6%

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,206FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles