Na Sheila Katikula, Mwanza
JESHI la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mwanza, limesema limebaini hujuma katika ajali ya moto iliyotokea katika baa ya The Cask iliyopo jijini hapa na kuteketeza mali za mmiliki na wateja.
Hayo yamezungumzwa leo Oktoba 27, 2021 na Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mwanza, Ambwene Mwakibete wakati akizungumuza na waandishi wa habari ofisini kwake.
Kamanda Ambwene amesema uchunguzi uliofanyika umebaini kuna vitendo vya hujuma vilivyofanywa na kusababisha mali ya mwekezaji na wateja kuteketea.
Amesema eneo hilo limefungwa vifaa vya kutolea maji kwa ajili ya kuzima moto pindi ajali itakapotokea hivyo ajali hiyo ingezuilika.
“Magari ya zimamoto yalifika kwenye tukio hilo yakiwa na maji ya kutosha ya kuzima moto na kama kungekuwa na hatua za awali tungeweza kuokoa mali zilizokuwemo kwenye baa hii,”amesema Ambwene.
Amesema asilimia kubwa ya baa hiyo ilikuwa imejengwa kwa mbao za miti na ndio kilikuwa kichocheo cha uharaka wa moto.
Hata hivyo amewataka wananchi kutoa taarifa mapema pindi inapotokea ajali ya moto ili kuepusha kusambaa kwa majanga ya moto.