MIONGONI mwa sifa za mwanasiasa madhubuti katika taifa lolote lile duniani, ni uwezo wake wa kutumia ulimi kugeuza dhoruba kwenye tukio linaoonekana kuleta hali ya sintofahamu.
Bila kutafuna maneno sifa hii adimu inawezekana kwa kiasi kikubwa ikawa ipo kwa Mbunge wa Hai na Mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani nchini Chadema, Freeman Mbowe.
Nasema Mbowe anayo sifa hii kwa maana ya kwamba katika tukio lililotokea hivi majuzi la kushambuliwa Mbunge wa Singida Mashariki na Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu imedhihirika hivyo.
Wakati wananchi wakiwa katika hali ya mihemko huku kila mmoja akisema lake kuhusu sababu iliyosababisha Lissu kushambuliwa kwa bunduki, Mbowe aliinuka na kutoa kauli kuwa huu si wakati wa kunyoosheana vidole bali ni kuwasaka waliohusika.
Kauli ya namna hii ya kutonyoosheana vidole, kutolewa na kiongozi mkuu wa chama katika mazingira ya taharuki ambapo aliyeshambuliwa ni mfuasi na msaidizi wake wa karibu katika masuala ya kisheria, ni cha kiungwana na chenye hekima ya hali ya juu.
Ikumbukwe mara baada ya shambulizi kufanyika kwa mtu ambaye ni maarufu kisiasa nchini, ziliibuka hisia nyingi ambazo kama ningeamua kuziandika baada ya kuzisikia kutoka sehemu mbalimbali, ningejaza kurasa nyingi na wakati mwingine muda usingetosha.
Ni wazi Mbowe kutokana na uzoefu wake katika masuala ya uongozi, aliona si wakati muafaka kutumia hisia za mwilini kutambua wahalifu kwani uhalifu unaweza ukajitokeza mahali ambapo hukutegemea.
Ni dhahiri Lissu kutokana na kuwajibika kwake katika masuala ya kisiasa na kisheria ndani na nje ya chama chake, si jambo la ajabu yeye kuwa na maadui wa kutoka ndani au nje ya chama chake.
Ndani ya chama, Lissu anaweza akawa na maadui bila yeye kujua kwani katika hali ya ubinadamu wapo wanachama wenzake wanaoweza kuwa wanamuonea wivu kwa kuhisi anazidi kupata umaarufu hivyo ataziba riziki zao au wakati mwingine kuchukia baadhi ya mambo anayoyafanya.
Wahenga waliosema: ‘‘kikulacho ki nguoni mwako’’ na ‘‘adui wa mtu ni wa nyumbani mwake’’ hawakuwa wajinga kwani katika masuala ya kisiasa lolote linaweza kutokea maana upendo au chuki uko ndani ya nafsi.
Nje ya chama chake cha Chadema, maadui wanaweza kupatikana kutoka chama tawala CCM ambacho kwa mitazamo ya watu mbalimbali wanadai kuwa Lissu amekuwa mkosoaji wake mkubwa au vyama vingine vya upinzani ukizingatia navyo kwa siku za hivi karibuni vimekuwa vikisigina vyenyewe kugombania mkate.
Lakini ikumbukwe pia Lissu ni raia, mwananchi, mtanzania na binadamu kama wengine hivyo si kiroja yeye kuwa na maadui wa nje ya mfumo wa kisiasa kama vile kutoka ndani ya familia, jamii yake, wahuni, majambazi na wengineo ukizingatia mwanasiasa huyo ni wakili na anamiliki mali kadhaa.
Hata hivyo njia panda hii itaondolewa na Serikali yenye wajibu wa kuwalinda watu wake chini ya vyombo vyake vya ulinzi na usalama kwa kushirikiana na raia wema watakaosaidia kutoa taarifa sahihi za kuwabaini wahalifu hawa waliokuwa wamedhamiria kuundoa uhai wa mpendwa wetu.