31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

KWA KENYA, UKABILA KWANZA UTAIFA BAADAYE

Na MARKUS MPANGALA


AGHALABU mjadala ukipamba moto juu ya katiba mpya na siasa za Kenya. Sehemu inayosifiwa ni uhuru wao katika masuala mbalimbali ya kisheria na taratibu za kuongoza nchi.

Kenya wanasifiwa kutokana na Mahakama kutengua matokeo ya urais yaliyompa ushindi Uhuru Kenyatta.  Jaji Mkuu David Maraga pamoja na wengine watatu walikubali  uchaguzi urudiwe, huku wawili wakipinga.

Sasa uchaguzi wa Kenya unarudiwa. Kwa msingi huo inasifiwa katiba na kulaumiwa tume ya uchaguzi. Tuanzie hapo, inaitwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka.

Kwangu mimi huo ni urembo wa kisiasa ambapo hutumiwa kama kichaka cha kuficha madhaifu mengine. Udhaifu wa kwanza wa Kenya ni siasa za kikabila. Muundo wa siasa zao haifanani na siasa za Tanzania wala Uganda.

Siasa za kutazama kabila kwanza zimetamalaki katika nchi za Sudan Kusini, Burundi, Rwanda na Kenya. lakini mwenendo huo wa kisiasa umekuwa sehemu ya maisha yao kwa miaka mingi sana.

Makabila yenye nguvu na idadi kubwa ya watu ni Wakikuyu na Kalenjing. Makabila hayo ndipo anakotoka Uhuru Kenyatta (Mkikuyu) na naibu wake William Ruto (Mkalenjing).

Uchaguzi wa mwaka 2013, nilikuwa naongea na rafiki yangu mwanahabari na mwalimu raia wa Kenya. Mara kwa mara alisisitiza kuwa kama hakuna maridhiano kati ya Wakalenjing na Wakikuyu kisiasa mambo yanakuwa mabaya zaidi.

Aliniambia ili kuendesha siasa kwa Kenya suala la ukabila ni jambo la kisiasa. Ni kama falasfa yao ya kisiasa (Political Ideology).

Kwa hiyo urembo wa maneno ya “Huru na Mipaka” kuelezea Tume ya uchaguzi halikuwa suluhisho la mambo. Ilikuwa sawa na kuweka urembo tu katika sehemu ambayo weyewe wanaficha uhalisi wa tabia zao kisiasa.

Mfano ni kampeni iliyoanzishwa na mashauri wa kampeni na mratibu wa Raila Odinga na NASA, David Ndii. Mwanazuoni huyo alikuwa akisisitiza juu ya kuanzishwa kwa Kenya mbili. Dhumuni lake lilikuwa kuonyesha kwamba Kenya inatakiwa kutawaliwa kwa misingi ya maelewano ya makabila.

Mchumi huyo alisisitiza Kenya igawanywe kwa misingi ya kikabila alisema, NASA pia wanataka kuuonyesha ulimwengu kwamba ni upinzani jasiri tu unaoweza kukabiliana na vitisho vilivyojaribu kusakama mashirika yasiyokuwa ya kiserikali dhidi ya kwenda kortini.

“Korti haiwezi kutoa suluhu la kisiasa… michakato yote ya kisiasa iliyopatikana tangu uhuru imepatikana kupitia nguvu… wengi wetu hatuna haja na nafasi za kisiasa, lakini ni kwa ajili ya kuifanya Kenya mahala pazuri,” aliongezea Ndii.

Ndii alitoa pendekezo hilo Agosti 22 mwaka huu wakati akihojiwa na kituo cha Televisheni cha NTV katika kipindi cha “Decesion2017”.

Ndii alibainisha kwamba Kenya ina jumla ya makabila 44, ambapo kwa kipindi cha mkiaka 50 tangu ilipopata uhuru wake imetawaliwa na makabila mawili tu; Wakikuyu na Kalenjing.

Kwa mujibu wa David Ndii ambaye alipendekeza sehemu ya kwanza itaitwa Central Republic of Kenya wakati sehemu ya pili itaitwa Pepole’s Republic of Kenya. Ikiwa na maana kwamba Kenya igawanywe kama ilivyokuwa Sudan ambako kumetengenezwa mataifa mawili yaani Sudan na Sudan kusini.

Mgawanyo uwe hivi; Western Kenya; ukanda huo uundwe na maeneo ya Luo, Luhya,Teso, Kisii na Kurial. Halafu upande wa Coastal Kenya; iwe na maeneo ya Swahili, Mijikenda, Pokomos, Giriamas, Taifa, na Taveta. North Wewst Kenya itaundwa na maeneo ya Turkana na Pokot.

Kukamilisha hatua hiyo alitangaza kufungua shauri au madai katika Tume ya Haki za Binadamu ya Afrika (African Commision on Human and Pepole’s Right), yenye makao yake mjini Banjul nchini Gambia.

Sababu kubwa aliyotaja ni kutokana na maelezo kwamba kulingana na tume hiyo wananchi wanao uhuru kulinda haki zao za kujitawala pamoja na kuanzisha taifa lao bila vikwazo vyovyote.

Wafuasi wanaotaka Kenya igawanywe wanaegemea katika Ibara ya 10 ya Mkataba wa Banjul (Banjul Charter) kwa tafsiri isiyo rasmi ya Kiswahili, inasema, “watu wote watakuwa na haki ya kuishi na kutawala, watakuwa huru kuamua mwelekeo wao wa hadhi ya kisiasa na watakuwa huru kutekeleza sera zao za uchumi na maendeleo ya jamii kwa mujibu wa kanuni na taratibu walizozichagua kwa uhuru wao,”.

Aidha, nimeshuhudia mjadala mzito katika ukurasa wa mtandao wa kijamii wa rais Uhuru Kenyatta, ambapo baadhi ya wakenya walihoji kwanini nchi yao imetawaliwa na makabila mawili pekee.

Jambo hilo linanisukuma kuamini Kenya suala la kabila lao ni la kwanza kisha unafuata utaifa. Kwahiyo linapokuja suala la watu wanaosema kuwa Kenya inatufundisha mengi lakini tujue pia hasara ya mafunzo yaliyopo.

Mathalani, kufutwa matokeo ya urais kupambwa kwa namna nyingi. Tume ya uchaguzi inalalamikiwa kikiuka sheria za uchaguzi na katiba ya nchi yao. Wengine wanasema kulikuwa na wizi wa kura ambazo hazikuelezeka. Mahakama ya Juu ilisema baadhi ya kura 11,000 hazikuhesabiwa.

Katika imani yangu tunaagizwa kumbushaneni. Kwamba katika kukumbushana kuna salama itashuka. Hapo ndipo ninapotazama Kenya kwa jicho jingine, kuanzia uchaguzi, kampeni ya Kenya mbili ya David Ndii hadi hukumu ya Mahakama utabaini jambo moja tu; kabila lako ni muhimu.

Endapo wakenya wangewekeza nguvu kutafuta njia ya kutibu mpasuko wa kikabila wasingeendelea kuuana mara kwa mara. Lakini kwa kuwa waliona katiba ndio tatizo wamejikuta hawajatatua tatizo la msingi linalowakabili. Kama nilivyosema awali, mfano tume ya uchaguzi ilirembwa tu kujifurahisha mwonekano ilhali tatizo la msingi halikutatuliwa.

Tumeshuhudia mivutano ya kisiasa yenye “nembo” ya Wakamba (Kalonzo Musyoka) na Wajaluo (Raila Odinga) kwa upande mmoja dhidi ya Wakikuyu (Kenyatta) , Kalenjing (Ruto) na wamasai. Kwamba Wajaluo na wakamba wanaamini makabila ya wakikuyu, wakalenjing na wamasai ndiyo chanzo cha  tatizo. Na makabila mengine yanawatazama Wajaluo na wakamba vivyo hivyo.

Nchi ya hivi hata wafanyeje na kuiremba Katiba yao watakabiliana na jinamizi hilo kila waendako. Ni nchi ambayo inakubali kuona kabila ndicho kitu cha kwanza katika uchaguzi wao, hivyo kuibuliwa watu sampuli ya David Ndii linakuwa jambo la kawaida.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles