Na SUSSAN UHINGA, TANGA
HOSPITALI ya Rufaa ya Bombo mkoani Tanga, haina dawa ya usingizi kwa ajili ya wagonjwa wa upasuaji kwa siku ya tatu sasa.
Kutokana na hali hiyo, baadhi ya wagonjwa waliokuwa wameandaliwa kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji, wamekuwa wakilazwa wodini hospitalini hapo bila kujua hatima yao.
Wakizungumza na MTANZANIA jana kwa sharti la kutotajwa majina yao gazetini katika wodi ya B3 iliyoko jengo la Galanosi, wagonjwa hao walionyesha kukata tamaa kwa kuwa hawajui ni lini watafanyiwa upasuaji.
“Binafsi niko hapa tangu Desemba 28 nilipoambiwa natakiwa kufanyiwa upasuaji kwa ajili ya kumaliza tatizo langu.
“Lakini, tangu siku hiyo ambayo ndiyo nilitakiwa kufanyiwa upasuaji, niko hapa tu na wenzangu hatujui tutatibiwa lini, kwani tumeambiwa dawa ya usingizi haipo.
“Tunachokifanya sasa kusali tu, vinginevyo mambo yanaweza kuwa mengine.
“Mimi ni mmoja wa wagonjwa tuliokuwa tumeshaandaliwa kwa ajili ya upasuaji na hapa unaponiona na wenzangu, sili chakula kwa sababu sijaruhusiwa kula.
“Kibaya zaidi, wenzetu wengine wameshawekewa mipira ya haja ndogo tangu mgonjwa wa mwisho alipofanyiwa upasuaji siku tatu zilizopita,” alisema mgonjwa huyo akiwa na wenzake.
Pamoja na hayo, mgonjwa mwingine anayesubiri upasuaji, alisema juzi usiku waliletwa watoto wawili waliokuwa wakihitaji upasuaji, lakini nao hawakufanyiwa kutokana na ukosefu wa dawa hiyo.
“Kuna watoto wawili waliletwa hapa juzi usiku ikaonekana wanahitaji upasuaji wa dharura, lakini hawakufanyiwa kwa sababu dawa ya usingizi haipo ingawa madaktari walikuwapo,” alisema.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dk. Asha Mahita, alipotakiwa kuzungumzia tatizo hilo, alisema hawezi kusema chochote kwa kuwa alikuwa kwenye ziara ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, wilayani Muheza.
“Niko kwenye ziara ya waziri siwezi kusema chochote kwa sababu ndiyo kwanza nimepata taarifa hiyo,” alisema Dk. Mahita.
Wakati Dk. Mahita akisema hayo, Waziri Ummy alipotakiwa na waandishi wa habari azungumzie taarifa hiyo, alisema analifuatilia suala hilo.