29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 6, 2023

Contact us: [email protected]

WANNE WAACHIWA KESI YA DK. MVUNGI

new-law

Na PATRICIA KIMELEMETA – DAR ES SALAAM

WASHTAKIWA wanne kati ya kumi wanaodaiwa kumuua aliyekuwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dk. Sengondo Mvungi, wameachiwa huru.

Waliachiwa jana baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kuwaona hawana hatia.

Washtakiwa hao ni Ahmad Kitabu (30), Zacharia Msese (33), Masunga Makenza (40) na John Mayunga (56).

Akisoma uamuzi huo mahakamani hapo jana, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas  Simba, Wakili wa Serikali, Pamela Shinyambala, alidai kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), hana nia ya kuendelea na kesi kwa washtakiwa hao kwa mujibu wa kifungu 91 (1) cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai.

Kutokana na hali hiyo, Wakili Shinyambala alisema DPP ataendelea na mashtaka kwa washtakiwa sita waliobaki.

Aliwataja washtakiwa hao ni Juma Kangungu (29), Paulo Mdonondo (30), Mianda Mlewa (40), Msungwa Matonya (30) na Longishu Losingo aliyewahi kuwa mlinzi wa marehemu Dk. Mvungi.

“Upande wa mashtaka tayari umewasilisha jalada la kesi hiyo Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam ili kuendelea na kesi hiyo kwa kuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, haina uwezo wa kisheria wa kusikiliza kesi za mauaji.

“Kwa hiyo, tunaisubiri Mahakama Kuu ipange jaji  ili kesi iweze kuendelea wakati tukiendelea na taratibu nyingine za kisheria zinazohusu kesi hiyo,” alisema Wakili Shinyambala.

Hata hivyo, Hakimu Simba ameutaka upande wa mashtaka kuhakikisha unapeleka cheti cha kifo cha mshtakiwa wa kwanza, Chibago Chiugati (33) aliyedaiwa kufariki akiwa gerezani ili mahakama hiyo iweze kukiangalia na kujiridhisha.

“Pia cheti hicho kitatusaidia upande wa mashtaka wakati wa mwendelezo wa kesi katika Mahakama Kuu,” alisema.

Washtakiwa hao walipandishwa kizimbani kwa madai ya kumshambulia kwa mapanga na hatimaye kumsababishia kifo Dk. Mvungi, Novemba 3 mwaka 2013.

 NJE YA MAHAKAMA

Baada ya washtakiwa hao wanne kuachiwa huru, walifurahi na kuonekana hawaamini uamuzi wa mahakama kwa kuwa walikaa mahabusu kwa miaka mitatu wakisubiri uamuzi wa mahakama.

Hata familia zao wakiwamo wake zao na watoto, walionekana kukusanyika mahakamani hapo kuwapongeza, huku wakionekana kutoamini kilichotokea kwenye uamuzi huo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles