NA AZIZA MASOUD,Dar es Salaam.
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema Serikali inatarajia kuanza kutekeleza miradi mikubwa mitatu ikiwamo ujenzi wa hospitali za rufaa tano zitakazojengwa katika kanda kwa msaada wa Korea ya Kusini.
Alitoa kauli hiyo Ikulu, Dar es Salaam jana baada ya mazungumzo na Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Lee Nak-Yon ambaye yupo nchini kwa ziara ya kazi ya siku tatu.
Majaliwa alisema miongoni mwa mambo aliyozungumza na kiongozi huyo ni namna bora ya kuendeleza ujenzi wa miradi ya maendeleo ambako walikubaliana kuanza kutekeleza ujenzi wa miradi mitatu mikubwa.
“Mbali na miradi hii iliyopo sasa tunatarajia kutekeleza miradi mingine mitatu ikiwamo ya msisitizo wa kuimarisha sekta ya afya kwa kujenga hospitali nyingine tano za rufaa kwenye kanda zote,nayo ni maeneo ambayo tumeyazungumza leo(jana),”alisema Majaliwa.
Alisema miradi mingine ni ujenzi wa daraja la Kigongo Busisi Mwanza, lenye urefu wa mita 3,200 na kuimarisha mradi wa barabara ya Chaya – Tabora ambayo imebaki kilomita 42.
Viongozi hao pia walijadili namna nzuri ya kuimarisha uhusiano katika sekta mbalimbali kati ya Tanzania na Korea Kusini, alisema.
“Mazungumzo haya yamejikita katika kuimarisha maendeleo ya uchumi, utamaduni, Tehama (Teknolojia ya Habari na Uhusiano), sayansi, sekta ya utalii na biashara kwa ujumla wake,”alisema Majaliwa.
Alisema wameyapa nafasi kubwa maeneo hayo na kwamba kwa sasa Watanzania wataanza kuona matunda zaidi kwa uhusiano mzuri baina ya nchi hizo mbili.
“Tumekaribisha makampuni mengi yaje Tanzania kwa ajili ya uwekezaji, mnajua kuna mradi mkubwa wa reli, tuna Hospitali ya Mloganzila, zote zinajengwa kwa mkopo wa masharti nafuu na nchi hii,”alisema Majaliwa.
Alisema katika mazungumzo hayo na Waziri Mkuu Nak-Yon pia wamekubaliana kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini kupitia Balozi wa Tanzania nchini humo, Matunga Masuka.
Alisema kiongozi huyo pia amefuraishwa na amani iliyopo nchini na Tanzania pia imeipongeza nchi hiyo na nchi jirani ya Korea Kaskazini kwa kukaa pamoja na kuimarisha amani ya eneo hilo.
“Tunaunga mkono juhudi zao na wameendelea kutuhakikishia kuwa watajifunza kutoka kwetu waweze kuimarisha amani baina ya nchi hizo,”alisema Majaliwa.
Katika hafla hiyo pia nchi hizo zilisaini makubaliano ya kuondoa mahitaji ya viza kwa watanzania na Wakorea Kusini wanaotumia pasipoti za diplomasia na utumishi.
Makubabaliano hayo yalisainiwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Dk.Augustine Mahiga na Makamu wa Kwanza wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Korea Kusini, Lim Sang –Nam kuimarisha uhusiano na maendeleo ya nchi hizo mbili.
Baada ya kumalizika kwa ghafla hiyo, Waziri Mkuu Majaliwa na mgeni wake walitembelea kituo cha kuhifadhi kumbukumbu za eletroniki za Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) Kibaha na Hospitali ya Mnazi Mmoja ambavyo vyote vimejengwa kwa ufadhili wa mashirika ya maendeleo ya nchi hiyo.
Mwisho
Uongozi gazeti la Mseto
kurudi mahakamani
Na TUNU NASSOR-DAR ES SALAAM
UONGOZI wa gazeti la Mseto leo unatarajia kurudi katika Mahakama ya Afrika Mashariki kuiomba kutoa amri ya utekelezaji wa kulifungulia gazeti hilo kama ilivyotolewa katika uamuzi wa kesi hiyo.
Gazeti la Mseto lilifungiwa kwa miaka mitatu kuanzia Agosti 11, 2016 na aliyekuwa Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Nape Nnauye.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mwanasheria kutoka Kituo cha Haki za Binadamu na Utawala Bora(LHRC), Fulgence Massawe alisema uamuzi huo ni kutokana na serikali kutoonyesha nia ya kutekeleza uamuzi wa kulifungulia gazeti hilo.
Alisema ni muda mrefu tangu utolewe uamuzi wa kulifungulia gazeti hilo lakini serikali imekaa kimya hivyo wameamua kurudi kuiomba mahakama hiyo kuomba utekelezaji wa uamuzi.
“Kesho Jumatatu (leo), tutarudi tena mahakamani kuiomba iiagize serikali kulifungulia gazeti la Mseto kama hukumu ya mahakama hiyo ilivyoamuru,” alisema Wakili Massawe.