23.4 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

HOPE NSALU: Mwanafunzi mlemavu aliyetupa nyimbo akabeba mavazi  

Na Hamisa Maganga, Dar es Salaam

WATU wenye ulemavu wanachukuliwa kuwa wana upungufu katika moja ya viungo vyao mwilini, na hivyo kuhitaji usaidizi wa namna moja au nyingine katika utendaji wao wa kazi.

Ukosefu wa huduma mbalimbali za jamii kwa watu wenye ulemavu, unawafanya waathirike kisaikolojia na wengi wao kukata tamaa.
Tafiti kadhaa zilizofanywa katika baadhi ya mikoa Tanzania bara na Zanzibar, zilibaini kuwa watu wenye ulemavu hawapati fursa sawa katika kupata haki ya elimu kutokana na mila na fikra potofu kwamba kuwasomesha ni uharibifu wa rasilimali.

Lakini, licha ya kukumbana na vikwazo, bado kuna watu wenye ulemavu waliodhihirisha kuwa ulemavu si ugonjwa, mmoja wapo ni Hope Nsalu.

Siku ya kwanza kumuona Hope ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha tano katika Shule ya Sekondari Baobab iliyopo Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani, sikuamini kama ana uwezo mkubwa kuliko hata watu wasio na ulemavu.

Mwanafunzi huyu mwenye ulemavu wa miguu, amekuwa akifanya mambo makubwa ya kushangaza ukilinganisha na hali aliyonayo.

Hope ana mengi ya kuvutia, ikiwamo ubunifu wake wa mavazi, uimbaji na jinsi anavyothamini elimu kuliko kitu kingine chochote, akiamini kuwa ndiyo itakayomkomboa maishani.

Licha ya kuwa ni mtoto wa Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Injinia Stella Manyanya, Hope hajali nafasi aliyonayo mzazi wake, anachoamini ni kwamba elimu ndiyo itakayokuja kumkomboa na si urithi kutoka kwa wazazi.

Akizungumza na MTANZANIA kuhusu historia yake kimasomo na kipaji alichonacho Hope anasema: “Mimi ni mtoto wa mwisho kuzaliwa katika familia yetu, ambapo nina kaka na dada yangu.

“Elimu ya msingi niliipata katika Shule ya Msingi Peninsula iliyopo Masaki, hapa hapa Dar es Salaam, baada ya kuhitimu nikajiunga na Shule ya Sekondari St. Joseph Millenium ambapo nilisoma kuanzia kidato cha kwanza hadi cha tatu ambapo kutokana na changamoto ya ngazi, nikahamia Shule ya Sekondari ya Wasichana Huruma, ambako ndiko nilikomalizia kidato cha nne.”

Hope anasema kuwa kidato cha nne alifanya vizuri ambapo alipata sifa ya kumwezesha kuendelea na sekondari ya juu – kidato cha tano na sita. Akajiunga na Sekondari ya Baobab ambako anachukua masomo ya arts.

Akizungumzia kipaji chake, anasema alianza na uimbaji, ambapo mama yake alikuwa akimtumia sana kuimba nyimbo za mazingira kuhamasisha wakazi wa Jiji la Dar es Salaam kuweka safi mazingira yao, lakini pia kukuza kipaji chake.

Injinia Manyanya alikuwa mdau mkubwa wa masuala ya uzoaji taka katika Jiji la Dar es Salaam, na harakati zake zilisaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza uchafu.

Hope anasema sasa hivi ameacha kuimba, japo kuwa amerekodi nyimbo nyingi na ana ‘tape’ ambazo amezihifadhi kama kumbukumbu yake ya hapo baadaye.

“Nilikuwa naimba katika kundi la Uswahilini Matola na nyimbo zangu zimepigwa sana, lakini sasa hivi nimejikita zaidi katika masomo, hivyo muda wa kuimba sina,” anasema.

Akizungumzia kuhusu ubunifu wa mavazi, anasema alianza kubuni akiwa kidato cha tatu, lakini hakuwa anajulikana kwa sababu shule aliyokuwa anasoma haikuwa na mambo ya mavazi na ubunifu.

“Nilipokuja hapa Baobab nilikuta kuna mashindano ya masuala ya mavazi na ya kumtafuta mlimbwende wa shule (Miss Baobab), nikavutiwa nikaanza kuwabunia mavazi.

“Wanafunzi waliona michoro yangu ikawavutia, wakashawishika kuona jinsi ninavyobuni mavazi. Siku ya mahafali ya kidato cha sita nikabuni mavazi, nikashona kwa kutumia mkono, si mashine, wanafunzi wakavaa na kupendeza mno,” anasema.

Hope anasema kuwa amekuwa pia akimshauri mama yake aina ya mavazi anayopaswa kuvaa anapokwenda katika tafrija mbalimbali.

“Hata vazi alililovaa wifi yangu siku ya harusi mimi ndio nilimshauri na alivyovaa alipendeza mno, akafurahia ubunifu wangu,” anasema Hope.

 

Ndugu zake wanamchukuliaje

Akizungumzia suala la kupata sapoti kutoka kwa familia yake, anasema kaka yake, dada yake, wifi na ndugu zake wanafurahia kipaji chake na kwamba wako tayari kumsaidia.

“Mama yangu anajua mimi ni mwimbaji, lakini hajawahi kuona mavazi yangu ninayobuni, hivyo sijui atafanya nini au atanishauri nini siku akifahamu kama ni mbunifu,” anasema.

 

IMG_6707Ndoto za baadae

Hope anasema ana ndoto nyingi, lakini kubwa zaidi ni siku moja kuwa mwanamitindo wa kimataifa.

“Lengo langu ni kuja kutetea haki za walemavu, hivyo nataka kuwa mwanamitindo wa kimataifa ambaye nitafungua kampuni yangu kubwa ya masuala ya mavazi.

“Katika kampuni hiyo asilimia 60 ya wafanyakazi watakuwa walemavu wa aina mbalimbali, nia yangu ni kutaka kuwakomboa na kuonyesha vipaji vyao kupitia kwangu,” anasema Hope huku akisikitishwa na kitendo cha watu kuwanyanyapaa walemavu bila ya sababu za msingi.

Anasema kuwa walemavu wanateseka na kutengwa na jamii jambo ambalo linamgusa mno, hivyo anasoma kwa bidii ili kuja kuwakomboa hapo baadae.

 

Changamoto

Licha ya kumudu kufanya kazi vizuri, anasema kuna mambo ambayo yanamkwamisha ikiwamo suala la ubovu wa barabara.

“Katika ubunifu wangu wa mavazi wakati mwingine huwa nahitaji kununua vitu kadhaa, lakini huwa nashindwa kuyafikia baadhi ya maeneo kununua vitu hivyo kutokana na ubovu wa barabara, hasa ukizingatia kuwa natumia baiskeli kujiendesha,” anasema.

 

Anavyomudu kujihudumia shuleni

Hope anasema kuwa yeye si tegemezi kwa kiasi kikubwa kwa kuwa kazi zake zote shuleni anafanya mwenyewe jambo ambalo linawapa moyo wanafunzi wenzie na kumuona kwamba si mzigo.

“Wanafunzi wenzangu wananipenda na kunithamini… kwa sababu ya kujituma kwangu huwa wanapata nguvu ya kunisaidia katika baadhi ya mambo na kunipa moyo katika kuendeleza kipaji changu.

“Walimu pia ni msaada mkubwa kwangu, wako vizuri katika ufundishaji. Huwa ninautumia muda wangu wa masomo vizuri kuwasikiliza walimu na unapofika wakati wa kupumzisha akili ndio najikita katika kubuni mavazi,” anasema Hope.

Anabainisha kuwa huwa hafanyi mchezo katika suala la elimu ndiyo maana hathubutu kuchanganya vitu viwili kwa wakati mmoja.

Anasema kuwa awali alikuwa anasoma masomo ya Sayansi akichukua mchepuo wa PCB, lakini baadae alibadili na kuchukua HGL ili asome mambo yanayoendana na kipaji chake.

 

Ushauri kwa walemavu wenzie

Mwanafunzi huyu anawashauri walemavu wenzie wasijibweteke na kuonekana mzigo kwa watu wengine, badala yake wafanye kazi kwa bidii ili kujipatia kipato.

“Kuzubaa kwa walemavu wengi na kujiona kuwa wao hawajakamilika ndiko kunakowafanya wajione kama wanatengwa wakati si kweli.

“Nawashauri wajishughulishe ili kujipatia fedha za kujikimu kimaisha na si kungoja kupewa,” anashauri.

 

Kuendeleza kipaji

Hope anaomba mtu yeyote aliyeguswa na kipaji chake ajitokeze kumpa sapoti kwa njia yoyote ile.

“Nahitaji kupewa moyo ili niweze kufika kule nilikokukusudia, yeyote atakayeamua kunisaidia kwa njia yoyote ile naahidi kuwa sitamwangusha na kamwe hatojuta kutoa fedha zake au ushauri kwangu,” anasema.

Akizungumzia ulemavu alionao, Hope anasema kuwa amezaliwa nao hivyo haoni shida wala hadhani kwamba ni adhabu kuwa hivyo. Ameridhika na anafanya kila linalowezekana kuhakikisha kuwa anakuwa mtu mwenye mafanikio makubwa duniani.

 

Makamu Mkuu wa shule

Akimzungumzia Hope, Makamu Mkuu wa Shule – Taaluma, Alphonce Francis, anakiri kuwa ana kipaji cha ajabu na kwamba kutokana na ubunifu wake amesaidia kuitangaza shule.

“Huyu mtoto yuko vizuri sana, wakati wa mahafali ya kidato cha sita hapa, mgeni rasmi alikuwa Rais Mstaafu Jakaya Kikwete, alipoona yale mavazi yaliyobuniwa na huyu mwanafunzi mwenyewe, alivutiwa.

“Kikwete alipoona mavazi yaliyoshonwa na huyu mwanafunzi alivutika na kutaka kupiga picha na wale wanamitindo.

“Zile nguo ukiziona Kariakoo ni lazima utazinunua kwa gharama kubwa mno, hivyo wanafunzi wa aina hii ni hazina ya baadae,” anasema Francis.

Anabainisha kuwa kipaji cha Hope kimeonekana kwa kuwa shule yao pia inaweza kulea vipaji vya watoto, na kwamba wanafahamu namna ya kuwainua.

Anasema ukimwangalia Hope alikuwa na kipaji hiki tangu zamani, lakini alishindwa kujulikana kwa kuwa huko alikotoka hawakuwa watu wanaothamini vipaji na kuviendeleza.

“Tangu aje Hope hata miaka miwili hajafikisha ndiyo kwanza yuko kidato cha tano, lakini tayari watu wameanza kumfahamu anafanya nini, na ndiyo maana hata wewe mwandishi leo hii umemfuata hapa.

“Hapa tunakuza vipaji, na wapo wengi tu ambao wana uwezo wa kufanya mambo mbalimbali wakiwamo hata wanawake wanaoruka sarakasi,” anasema.

Anaeleza kuwa licha ya kipaji alichonacho, Hope yupo vizuri darasani na anayamudu masomo vema.

 

Wanafunzi wenzake

Wanafunzi wa Baobab wanamzungumzia Hope kuwa amekuwa kipenzi cha wengi shuleni kwa jinsi anavyojua kuishi vizuri na watu.

“Hope ni mtu anayejua kuishi vizuri na watu, hata awe amekuudhi vipi huwezi kumcheka kwa hali aliyonayo… anajiamini kupita maelezo, akilitaka jambo lake ni lazima litimie.

“Kimasomo pia yupo vizuri, anashirikiana na watu katika kila jambo, hajitengi, kwa kweli mambo anayoyafanya yanatuvutia hata sisi wenzie,” anasema Irena Kinabo, anayesoma naye mchepuo mmoja wa HGL.

Naye Vaileth Mgema ambaye analala bweni moja na Hope anasema: “Nampenda sana Hope jinsi alivyo, anavyojichanganya na watu… ni msichana ambaye huwezi kuchoka kumsaidia katika masuala ya shule.

“Yeye ndio msusi wangu, hata hizi nywele unazoziona amenisuka yeye, nampenda kwa kweli, ana uwezo mkubwa wa kufanya mambo mengi licha ya hali aliyonayo,” anasema Vaileth.

 

Injinia Stella Manyanya

Watu wanasema maji hufuata mkondo, mama yake Injinia Manyanya ambaye ni bibi wa Hope, alikuwa mjasiriamali wa kazi mbalimbali na amewahi kutengeneza na kuuza vyungu enzi za uhai wake, kazi ambayo hata Stella aliifanya kwa mapana yake.

Kwa upande wake, Injinia Manyanya ni mmoja kati ya kina mama waliosomea vizuri taaluma zao, na hakuishia hapo tu akachanganya fani ili kujiongezea weledi zaidi.

Kuhusu kipaji cha mwanawe, anasema tangu akiwa mtoto alimuona kuwa anapenda vitu vingi, hivyo hadi sasa hajui kipaji chake ni nini.

Anasema ana vitu vingi vikiwamo vizuri na vingine ni vya hatari, kinachofanyika ni kumshauri na kumuweka sawa.

“Nilipomzaa Hope akiwa na ulemavu nilimpenda na kumpa mapenzi yote kama mzazi. Sikuwa na hofu juu ya maisha yake kwa sababu walemavu huwa hawapendi kudharauliwa.

“Unajua mwanangu alianza kuzungumza mapema, yaani aliita mama na vitu vingine na kuanza kujifunza kutembea kwa magoti akiwa na umri mdogo mno.

“Anapenda kuishi maisha mazuri ndiyo maana huwa anafanya mambo mengi ili kuja kuwa mtu mkubwa hapo baadaye,” anasema Injinia Manyanya.

Anasema kuwa anavyofahamu ni kwamba walemavu wana vitu vingi vizuri, hivyo wakipata sapoti huwa wanafanya mambo makubwa zaidi ili mradi tu afarijiwe ili ajione ni mtu wa kawaida.

Injinia Manyanya anasema jambo ambalo watu wanakosea ni kuwadharau walemavu na kuwaona hawafai.

“Wazazi wengine wakishaona wamezaa walemavu basi wanaona kama wameshaharibikiwa. Mimi si miongoni mwao, mwanangu tangu mdogo niliona kama anaweza kufanya kitu ndiyo maana hata alipoanza kuimba nilimsapoti,” anabainisha.

 

Kaka yake anena

Akizungumzia kipaji cha Hope, kaka yake anayejulikana kwa jina la Lukaluka Innocent, anasema kuwa mdogo wake huyo amezaliwa na kipaji kwa kuwa mambo ya sanaa ameyaanza tangu akiwa mtoto.

Anasema awali alipokuwa akimweleza juu ya adhma yake ya baadaye, alikuwa hamwelewi, na badala yake alimsisitiza kuhusu suala la elimu kwanza.

Lukaluka anasema alikuwa akimshauri kuachana na mambo ya sanaa kwa kuwa hatoweza kushika mambo mawili kwa wakati mmoja.

“Mwanzoni kwa kweli nilikuwa nagombana naye, nilikuwa namsisitiza azingatie suala la elimu kwanza, hayo mengine yatakuja baadaye.

“Mimi ndiyo naishi na Hope nyumbani kwangu, kwa hiyo nilikuwa namfundisha sana pindi anaporudi likizo, awali alikuwa anasoma masomo ya Sayansi, lakini hakuwa vizuri na tulishawahi kuzungumza na walimu wake kuhusu jambo hilo.

“Nilikuwa naumia kwa kuwa nia yangu ni mdogo wangu apate elimu, sasa kitendo cha kuhama kutoka PCB kwenda HGL kiliniumiza na nikamuona hayuko makini na suala la elimu, hasa ukizingatia kuwa alikuwa na ndoto za kuwa daktari hapo baadae… nilimshangaa baada ya kuona anabadilika ghafla.

“Alitueleza kwanini amehamia HGL, baada ya mvutano mkali nikamwelewa, lakini pia tulishauriana na walimu wake tukakubaliana asome ‘Arts’,” anasema Lukaluka.

Anabainisha kuwa walikumbana na changamoto kubwa ya kuhakikisha wanabadili mawazo ya Hope, ambaye pia alikuwa na nia ya kuachana na elimu ya sekondari na kwenda kujiunga chuo kwa ajili ya kusomea masuala ya ubunifu.

“Kwa kweli suala hili nililipinga kwa nguvu zote, nikamwambia soma kwanza, maliza kidato cha sita kwa sababu anaweza kwenda chuo kusomea hayo mambo yake na akashindwa kufanikiwa, akawa amepoteza muda bure.

“Nilichokuwa naangalia ni kwamba asije akajifunga kung’ang’ania kitu kimoja na kuacha masomo halafu hicho kipaji chake kisimsaidie, atakuwa ameharibu mlolongo mzima wa maisha yake.

“Namshukuru Mungu alituelewa na hata sasa yuko vizuri shuleni tofauti na mwanzo,” anasema.

Lukaluka anajivunia kipaji cha mdogo wake na anasisitiza kwamba yupo naye bega kwa bega katika kuhakikisha kuwa anafanikiwa na hata mama yao alijitahidi kumwendeleza katika kipaji chake cha uimbaji.

Aidha, anamshauri mdogo wake asome kwa kuwa dunia ya sasa inahitaji watu wasomi hata kama ana kipaji, elimu ndiyo itakayomsaidia kufika huko anakotaka.

 

Wifi yake na nguo ya harusi

Clare Kahwili ambaye ni mke wa Lukaluka, anasema kuwa anafurahishwa na kipaji cha wifi yake kwa kuwa yeye ndiye chanzo cha kupendeza kwake siku ya harusi.

Anasema kuwa anamfahamu msichana huyo kabla hata ya kufunga ndoa na kaka yake, na alikuwa akisisitiza kwamba angependa kumbunia vazi atakalovaa siku ya harusi.

“Wakati wa maandalizi ya harusi alikuwa akinionyesha jinsi ambavyo wasimamizi wanapaswa kuvaa, na mimi kwa kuwa nina umbo kubwa kiasi alikuwa akiniambia kwamba wifi ukivaa hivi utapendeza sana, nilimsikiliza na kweli nilipendeza.

“Ndoto yake ni kuwa mwanamitindo wa kimataifa na dunia imfahamu, hivyo alipenda mno kwenda kusomea masuala hayo, lakini familia ilikataa na kumuasa asome kwanza hayo mengine yatafuata,” anasema Clare.

Anasema yuko tayari kuwa bega kwa bega na Hope ili aweze kufikia mafanikio anayoyahitaji, hivyo atamsaidia hadi aone amefika kule anakotaka.

Akizungumzia kuhusu upendo alionao kwake anasema: “Nampenda sana Hope kwa sababu ni msichana ambaye anajituma na anafanya kila kitu licha ya ulemavu alionao.

“Unajua mimi ni mama wa familia na nina watoto, sasa kuna wakati nilikuwa sina msichana wa kazi, basi Hope aliniambia wifi usiwe na wasiwasi nitakusaidia.

“Ilikuwa ni kipindi cha likizo, akawa anafanya kila kitu, yaani anapika, anadeki anaosha vyombo, ukirudi kazini watoto unawakuta wamekula na wameoga, kwa kweli anajitambua na najua atafika mbali,” anasema.

 

Jinsi walemavu wanavyochukuliwa

Takwimu za Umoja wa Mataifa za mwaka 2002, zinaonyesha kuwa asilimia 10 ya watu wote duniani wana ulemavu wa aina fulani.

Sera ya Taifa ya Walemavu ya mwaka 2004, inaonyesha kuwa Tanzania kuna walemavu wa viungo zaidi ya milioni tatu.

Nalo Shirika la Afya Duniani (WHO), linakadiria katika nchi nyingi duniani kiwango cha ulemavu ni kati ya asilimia 10 hadi 12.16.
Idadi hii inaweza ikawa imeongezeka kwa sasa.

Matokeo ya utafiti kuhusu watu wenye ulemavu Tanzania ya mwaka 2008, yanaonyesha kuwa ni watoto wanne tu kati ya 10 wenye umri kati ya miaka saba na 13 ndio wanaopata elimu ya msingi na wanaopata elimu ya sekondari ni asilimia tano.
Kwa mujibu wa matokeo hayo waliopata elimu ya juu ni chini ya asilimia moja na asilimia 48 ya watu wenye ulemavu hawajui kusoma wala kuandika ukilinganisha na asilimia 25 ya wale wasiokuwa na ulemavu.
Baadhi ya sababu zinazofanya walemavu wakose elimu ni pamoja na wazazi kuwaficha watoto wao nyumbani, miundombinu isiyorafiki katika shule mbalimbali na ukosefu wa vifaa vya kufundishia na kutokuwapo kwa walimu wa kutosha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles