24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, July 20, 2024

Contact us: [email protected]

Pluijm: Tutaichapa Esperanca iwe salamu kwa wengine

Hans-van-der-PluijmNA JENNIFER ULLEMBO, DAR ES SALAAM

KOCHA Mkuu wa Yanga, Hans Van der Pluijm, amesema wamejipanga kupata ushindi mkubwa dhidi ya Sagrada Esperanca ya Angola, ili kufikisha salamu kwa timu nyingine katika michuano ya Kombe la Shirikisho.

Yanga itavaana na Waangola hao katika mchezo wa hatua ya 16 bora ya Kombe la Shirikisho unaotarajiwa kufanyika kesho Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Ushindi katika mechi hiyo na ile ya marudiano itakayofanyika Angola wiki mbili baadaye, utawafanya Yanga kutimiza ndoto yao ya kutinga hatua ya makundi, ambayo inachezwa kwa mfumo wa ligi.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Pluijm alisema malengo yake ni kushuhudia timu yake inaingia hatua ya makundi na hatimaye kutwaa ubingwa wa michuano hiyo ya pili kwa ukubwa ngazi ya klabu barani Afrika.

Pluijm alisema kufanikiwa kuiondosha Sagrada Esperanca, kutakuwa ni salamu tosha kwa timu nyingine watakazocheza nazo hatua ya makundi.

“Dhamira yetu ni kushinda katika mchezo wa Jumamosi utakaochezwa hapa nyumbani na hata ugenini tuendeleze ushindi, nina imani wachezaji wangu hawataniangusha wataonyesha kiwango bora,” alisema Pluijm.

Mholanzi huyo alisema baada ya kuondoshwa kwenye michuano ya Klabu Bingwa Afrika, malengo yake ni kuitumia vema nafasi waliyoipata katika michuano ya Kombe la Shirikisho.

Yanga ilitolewa katika hatua ya 16 bora ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika kwa kupokea kichapo cha jumla ya mabao 3-2 kutoka kwa Al Ahly ya Misri.

Katika hatua nyingine Shirikisho la Soka nchini (TFF), limetangaza waamuzi watakaochezesha mchezo huo Jumamosi ambapo Joseph Odartei Lamptey, anatarajiwa kuwa mwamuzi wa kati

Lamptey kutoka Jiji la Accra, Ghana atasaidiwa na raia wenzake wa nchi hiyo kuchezesha mchezo huo ambao ni mwamuzi msaidizi namba moja, David Laryea wakati mwamuzi msaidizi namba mbili ni Malik Alidu Salifu.

Mwamuzi msaidizi mezani ni Cecil Amately Fleischer, huku Kamishna wa mchezo huo akiwa ni Asfaw Luleseged Begashaw wa Ethiopia.

Viingilio na upatikanaji wa tiketi utatangazwa leo na uongozi wa klabu ya Yanga, mara baada ya mkutano kati ya makocha wa timu zote mbili saa 5.00 asubuhi kwenye Ukumbi wa mikutano wa TFF.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles