Na Bakari Kimwanga, Aliyekuwa Kilwa
HOFU ya mapigano kati ya wakulima na wafugaji imetanda wilayani Kilwa mkoani Lindi, kutokana na kile kilichodaiwa kuwa ni uvamizi unaofanywa na wafugaji kwa kuingiza mifugo yao mashambani na kuharibu vyanzo vya maji.
Hatua hiyo inatokana na wafugaji waliopewa eneo la malisho kushindwa kuandaa malambo kwa ajili ya kunyweshea mifugo yao.
Wakizungumza na timu ya waandishi wa habari wa za mazingira waliokwenda katika Kijiji cha Hoteli Tatu, kwa ajili ya kuangalia namna sheria namba 4 na 5 za ardhi zinavyofanya kazi tangu ilipotungwa mwaka 1999.
Akizungumzia hofu hiyo kwa niaba ya wana kijiji wenzake, mkazi wa kijiji hicho, Abdallah Maftah, alisema licha ya kijiji kutenga ardhi kwa ajili ya matumizi bora ya ardhi pamoja na eneo maalumu la wafugaji, hali imekuwa tofauti katika kijiji hicho.
“Kwanza naomba niseme sijui kabisa sheria namba 4 na 5 ya ardhi ila nakumbuka tulitenga maeneo kwa ajili ya kilimo na mifugo. Ila hali imekuwa tofauti hivi sasa ng’ombe wanakuja hadi kwenye mazao yetu na hata tunajikuta tukitumia kisima kimoja cha maji na wanyama.
“…wafugaji walitakiwa kuchimba malambo kabla ya kuleta ng’ombe wao ila hapa kwetu Hoteli Tatu imekuwa tofauti, tunakunywa maji na ng’ombe, mbwa hili hatukubali na yaliyotokea Morogoro na hapa kwetu tutayaona,” alisema Maftah.
Akizungumzia madai hayo mmoja wa wafugaji hao, Robert Mboje, ambaye alikiri ng’ombe wake kuingia katika maeneo ya wafugaji alisema.
“Ni kweli ndama wawili waliingia katika maeneo ya wakulima walikwenda kwenye kisima kikubwa ninachoweza kueleza hawa ni wanyama na si binadamu na wakati mwingine hutoroka.
“… sijui sheria ya matumizi ya ardhi ninawaomba wanakijiji wenzangu pindi linapotokea jambo wao wananiambie tu kuliko kudhamiria kutaka kuharibu amani kwa ajili ya wanyama,” alisema Mboje.
Akizungumzia mgogoro huo, Ofisa Ardhi Mteule wa Wilaya ya Kilwa, Ernest Mwakang’ata, alikiri kufahamu tatizo hilo ambapo aliahidi timu ya wataalamu kwenda kwenye eneo hilo haraka na kuchukua hatua.
“Kijiji cha Hoteli Tatu walitenga matumizi bora ya ardhi kwa ajili ya eneo la makazi, kilimo na wafugaji na suala hili tayari lipo ofisini kwetu na tumeanza kulifanyia kazi kwa haraka na hivi sasa tunajiandaa kwenda huko.
“Tayari mkuu wa wilaya ameshatoa maagizo ya kutaka ndani ya kipindi kifupi cha mwezi huu tuwe tumeshatatua migogoro yote ya ardhi ikiwemo pamoja na huu,” alisema Mwakang’ata.
Ziara hiyo iliandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) kwa kushirikiana na Shirika la Care Tanzania.